Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Taarifa hii ya Kamati yako Maalum. Kipekee kabisa kama kijana, nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuwa kwenye Kamati hii. Hakika nimejifunza, na nikwambie haukunipeleka kimakosa, nimeiva. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani zangu hizo, dhumuni la shamba kugawanywa kwa mwekezaji ama kubinafsishwa kwa mwekezaji, taarifa yetu imejieleza vizuri sana na nimshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuwasilisha taarifa kwa niaba yetu. Lengo lilikuwa ni jema sana na dhamira ilikuwa ni njema sana juu ya ubinafsishaji ama uwekezaji wa shamba lile. Taarifa imeshiba, imejitosheleza.
Mheshimiwa Spika, kilichofanyika ni mwekezaji kuchukua shamba na kutokwenda kwenye malengo na dhamira lililodhamiriwa kupitia Wizara ya Mifugo ambalo lilipeleka Baraza la Mawaziri na Waheshimiwa Mawaziri wakaridhia shamba lile madaraka yakasimishwe kwa Mkoa wa Rukwa ili waweze kubinafsisha na baadaye mrejesho urudi kwenye Baraza la Mawaziri, na ninaamini likiwa limekamilika kwa kuhakikisha kwamba limetenda haki.
Mheshimiwa Spika, tumekwenda Rukwa, tumekwenda uwandani, tumewasikiliza wahusika. Tunaujua vizuri ubinafsishwaji, ugawanywaji na haki ambayo haitendeki ndani ya Mkoa wa Rukwa kupitia shamba la Efatha. Madhumuni yalikuwa ni ufugaji ambao utawasaidia vijiji vya jirani ama wananchi wanaolizunguka shamba kufanya Mkoa wa Rukwa kupitia Shamba la Malonje kuwa ni kitovu cha kiuchumi kupitia mwekezaji, na wananchi katika ufugaji wa nyama pamoja na maziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati shamba lile linakwenda kubinafsishwa wakati mwekezaji anatafutwa, wananchi pia walipewa fursa, lakini walipewa masharti maalum kwamba sharti ni ufugaji na siyo kilimo. Wananchi nao walitafuta fedha za kuweza kulimiliki shamba lakini walikataliwa kwa kigezo kwamba hawaruhusiwi kulima, ni suala la ufugaji peke yake. Jambo la kushangaza na cha ajabu mwekezaji amekuja kupewa ambaye amekidhi vigezo, lakini kwa 99% amekwenda kulima na siyo kufuga jambo ambalo wananchi walikataliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkanganyiko, wakati tunawaita viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Rukwa, ni ukweli usiyopingika kwanza wamekuwa ni wafichaji wa taarifa, lakini ni waonevu hasa kwa upande wa wananchi. Inasikitisha na inashangaza Mheshimiwa RC anasema yeye alipokea maagizo kutoka kwa sekretarieti yake kwa maana ya Katibu Tawala na timu nzima kwamba linatakiwa liuzwe shamba kwa shilingi milioni 600, lakini RC hakuwa na nafasi ya kujua na kutaka kwamba barua hiyo aione, aipitie ili aweze kupata mamlaka.
Mheshimiwa Spika, kitu cha ajabu, tulipokutana na Mwanasheria wa Mkoa wa Rukwa alikiri kwamba halifahamu wala hakushirikishwa katika uuzaji wa shamba hili. Katika uuzwaji wa shamba hili hata hizo shilingi milioni 600 bahati mbaya sana kwamba Manispaa ya Sumbawanga ilitakiwa ipate shilingi milioni 400, lakini manispaa ya vijijini ilitakiwa ipate shilingi milioni 200. Tulitumia nguvu na jasho kutafuta uhalali wa hizo fedha na account zilizopitia. Tulinyimwa takribani siku mbili taarifa za fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri tulipopata hizo fedha katika Manispaa ambayo ilitakiwa ilipwe shilingi milioni 400, tulipata risiti ya shilingi milioni 50. Halmashauri ya vijijini ambayo tumeambiwa imegawanywa shilingi milioni 200 hatukupata risiti ya shilingi milioni 200, tulipata risiti ya shilingi milioni 50 peke yake. Fedha hizi zimeenda wapi? Mimi na wewe nadhani hatujui, lakini lipo vyombo vya Serikali.
Mheshimiwa Spika, tumekwenda uwandani, risasi wananchi walizopigwa, matukio yote yaliyofanyika, cha ajabu na kushangaza kuna taarifa za mwekezaji, lakini taarifa za wananchi kwenye Jeshi la Polisi hazipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama kijana, Jeshi la Polisi kupitia Mkoa wa Rukwa linapaswa lijitafakari mara mbili. Jambo hili kule uwandani wananchi hawana haki ya kwenda kushtaki Kituo cha Polisi, hukuti taarifa hizi kwenye kata, hukuti wilayani, taarifa hizi zipo Jeshi la Polisi Mkoa peke yake. Ameeleza hapa Mjumbe aliyepita, wale wananchi kwenye lile shamba, shamba lile lilikuwepo enzi na enzi na lilikuwa lina barabara za asili.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana yupo mama mmoja tulipata historia yake pale ambaye alikuwepo na alikuwa ana mtoto mdogo, walimkamata yule mama wakambaka. Walivyomaliza wakamfungia kwenye majumba mawili, lakini yule mtoto mdogo walimtelekeza shambani.
Mheshimiwa Spika, yule mama alipelekwa Magereza na hapa ni kwa sababu ya muda, tungekuonyesha risiti za siku alipotoka Magereza, risiti ipo lakini mtoto alitekelezwa na baadaye mtoto aliokotwa akaenda kupelekwa kijijini. Mtoto amekaa bila mama yake mpaka mama alipotoka Magereza. Haivumiliki! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda kuuliza Halmashauri ya Manispaa itakwambia taarifa nyingine; ukienda kuuliza vijijini watakwambia jambo lingine. Tunakubali uwekezaji, mwekezaji huyu sawa tumekubali alime shamba, lakini shamba hili kwa zaidi ya 80% linakodishwa na wananchi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati unakodisha shamba unakodisha kwa shilingi 10,000, lakini mwisho kuna fungu la 10. Nje ya fungu la 10 wapo wananchi wanaokodishwa shamba kwa shilingi 100,000 au shilingi 200,000. Ikitokea kuna kiongozi mkubwa ameshafika pale, anapewa lile shamba na wewe mwananchi wa chini hupewi shilingi 100,000 yako; hurudishiwi shilingi 200,000 yako na wala haulimi shamba na utaondoka kwa kipigo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tarehe 17 ya mwezi wa Saba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alikwenda Mkoa wa Rukwa, alipofika alikutana na hii changamoto. Hata hivyo, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu alisema ipo Kamati ambayo imeundwa na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge anaisubiri ifanye kazi yake. Ahsante Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, jambo hili limekuwa la miaka mingi lakini Mama ulifika na ulijibu kwa kutulia, tunakushukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania una haki ya kuwa Rais wa Mabunge Duniani Mungu amekuchagua. Unatosha. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatosha. Watendaji wachache ambao hawana nia njema na Serikali yetu hawamwelewi Mheshimiwa Rais nia yake na dhamira yake kwa wananchi wake. Hatutakubali waendelee kutia doa Serikali kwa uzembe wao.
Mheshimiwa Spika, unamwuliza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, hajui; unamwuliza RPC, hajui; unamwuliza mtendaji wa Serikali, hajui; unamwuliza nani, hajui. Wamewekwa kwa sababu gani? Kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja shamba hili lichukuliwe na lirudi kwenye utaratibu. Hatuna shida na mwekezaji, hatuna shida na wananchi, tunachokihitaji ni haki ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)