Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa hii kuweza kuchangia ripoti ya Kamati Maalumu ya Shamba la Malonje. Kwa namna ya kipekee kwanza nikupongeze kwa maamuzi yako ya kuunda Kamati ili kuweza kufuatilia mgogoro huu. Mwenyezi Mungu aendelee kukupa maono, aendelee kuwa nawe ili uweze kuona mambo makubwa ya nchi yetu ambayo tunaweza kuendelea kulisaidia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza nikiwa kwenye Kamati kwa jambo ambalo limeweza kutokea kwenye Kamati, Kamati yako kwa mara ya kwanza wakati tunaelekea kwenye Kijiji cha Malonje, tulipata shinikizo la kutoka na viongozi wa Serikali. Walisema nendeni, kama mtayakuta, basi tuleteeni, lakini muda huo Kamati inakwenda huko inaambiwa maneno hayo kwa dhihaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wanaambiwa maneno hayo kwa dhihaka tunakwenda kule tukaanza kuulizana, hivi kweli hilo suala lipo? Mbona viongozi wa Serikali wanatuambia hivi? Tukaanza kupata wasiwasi, tukasema hili suala tuna wasiwasi halipo. Wakati tunakwenda kule tulivyowakuta vijana ambao wamepigwa risasi na wanawake ambao wamedhalilishwa, sikuwahi kumwona Mheshimiwa Mbunge wa kiume akilia, lakini kwa mara ya kwanza nikiwa ndani ya Bunge zaidi ya miaka 10 niliona Waheshimiwa Wabunge wako wakidondosha machozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, walishindwa kuvumilia namna manyanyaso, wananchi wa vijiji hivyo walivyokuwa wakielezea wanavyovipata kwa uwekezaji huu. Tukwambie kwamba umetenda haki kuiteua Kamati kusema wakashughulikie suala hili. Wakati kijana anayeishi na risasi kichwani anakwenda pembeni, nilikuwa na miongoni mwa Katibu wa Kamati nikasema mbona huyu kijana kama ana shida nyingine? Nikawa na wasiwasi labda ana shida ya akili. Kumbe tatizo lililokuwa likimsumbua, anaishi na risasi kichwani.
Mheshimiwa Spika, tufikirie kama Waheshimiwa Wabunge tumekaa hapa tukiisaidia Serikali, lakini kuna mwananachi ananyanyasika na uwekezaji, anaishi na risasi toka alipopigwa risasi mpaka leo. Hili tusilimalize kuzungumza. Kama itahitaji mchango kwa Waheshimiwa Wabunge, basi tuwaombe Waheshimiwa Wabunge tumchangie na risasi ile atolewe ili aweze kuishi vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuna suala la wanawake ambao tulishindwa kuwahoji hadharani, tukawaita pembeni kuwahoji. Kati yao kuna mwanamke alituelezea amebakwa na wanaume watatu lakini mwingine amebakwa na vijana wawili ambao ni walinzi wa Shamba la Efatha.
Mheshimiwa Spika, wakati hawa akina mama wamebakwa, wakati wanatoa maelezo mmoja aliyebakwa ana mimba ya miezi mitatu, anasema ilibidi akimbie kijiji kwenda nyumbani kwao kwa mama yake. Alipomweleza mama yake akampa dawa za Kiswahili ili mimba itoke kwa sababu ya imani zao, kwamba lile tendo lililofanyika kwake mtoto atakayezaliwa hataishi vizuri. Sisi tukiwa kama Wabunge wanawake hatuwezi kuvumilia hali hii ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipokuwa naishi Zanzibar nilikuwa nikisikia na mpaka leo tupo tukijua habari za ukoloni, lakini kwa mara ya kwanza habari ya ukoloni kwenye kichwa changu nimeanza kupata picha yake kwenye Shamba la Malonje lililoko Rukwa. Kilichopo kule ni ukoloni. Leo mfikirie mwanamama ambaye ni mjamzito anataka kwenda hospitali anatengenezewa masafa marefu, lakini njia ipo kwenye shamba hapa mpaka pale unafika hospitali, lakini hawezi. Hatuwezi kukaa kimya kwenye hili.
Mheshimiwa Spika, wanawake, wananchi wanaoishi kwenye yale maeneo wananyanyasika na wanapata shida.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, Taarifa, Kunambi.
SPIKA: Inatokea wapi?
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, niko hapa.
SPIKA: Mheshimiwa Tauhida Cassian kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Emmanuel Kunambi.
TAARIFA
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Tauhida anachosema ni sahihi kabisa na hili shamba ni mfano tu wa matukio yanayoendelea nchini kwa mashamba ya namna hii. Matatizo ya namna hii yako katika maeneo mengi nchini. Hata pale Mlimba kuna Shamba la Kambenga wananchi wamekuwa wakinyanyasika kama walivyonyanyasika wale wengine. Ahsante. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Tauhida unaipokea taarifa hiyo?
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili na Bunge lako litende haki pale Waheshimiwa Wabunge wanapoleta malalamiko kama haya, liendelee kutenda haki.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo ambalo pia lilijitokeza, kuna suala la utozwaji wa wananchi wanaokodi maeneo yale kutozwa fungu la kumi. Tanzania watu wake wanaishi wakiwa na dini, lakini Serikali haina dini. Unapozungumzia fungu la kumi linahusu upande mmoja wa imani, kuna baadhi ya imani haiishi kwenye fungu la kumi, leo unashurutisha?
Mheshimiwa Spika, nilimuuliza mhusika, nikamuuliza unapotoza fungu la kumi hudhani kama unahusisha imani? Unamshurutishaje Hamisi Kigwangala na suala la fungu la kumi? Akanijibu, hatukuwaita, wamekuja wenyewe. Haiwezekani wananchi wa Tanzania washurutishwe kwa sababu ya kutafuta kula yao. Haiwezekani washurutishwe kuishi ndani ya nchi yao kwa sababu ya kutafuta tonge lao, anachokitafuta ni mahindi kwa ajili ya kusonga ugali, huwezi kumshurutisha. Kama Serikali yetu haiwezi kushurutisha watu wake kwenye masuala ya imani, hatuwezi kukaa kimya kuwaacha wawekezaji wakashurutisha watu kwenye masuala ya imani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala hili wakati ulipotupa hii kazi, tulipokwenda kuripoti kwa wenzetu wa Serikali, walitupa picha kutuonesha kwamba ni suala la kisiasa. Hata leo watu wanaweza kukwambia kwamba hili suala ni la kisiasa.
Mheshimiwa Spika, kwenye masuala ya maslahi ya wananchi hakuna suala la kisiasa na nikuthibitishie kwa kuwa ni mjumbe wa NEC nilifanya kujiridhisha, Mbunge aliyekuwepo pale kati ya vijiji vinavyolalamika ni Mbunge wa CCM, lakini wakati tunaenda kuhoji, Mheshimiwa Ester Bulaya atathibitisha, vijana na viongozi wa CHADEMA walikuwa wakija kumsalimia. Niliwauliza, nikawaambia, vipi mbona mko hapa na hili suala tunaambiwa ni la kisiasa? Wakasema kwenye hili hatuna siasa, wananchi tunataka haki kwa wote. Kati ya watu waliofanya kuandika ripoti, mmoja aliyekuwa anazungumza ni mtu wa CHADEMA, ndiye aliyeandika, anasema wakati wanaandika ripoti, sasa siasa hii ni ya chama gani? Siasa hii ni ya chama gani?
Mheshimiwa Spika, Mbunge anafikia kudharaulika na viongozi wenzie wanaotawala, anasema anatafuta kura. Nafuu Mbunge ukubali kushindwa Ubunge lakini wananchi wapate kuishi vizuri. Wabunge wako hatuwezi kuwa waoga, hatuwezi kuwa Wabunge wa kununuliwa, hatuwezi kuwa Wabunge tulioweza kukaa kuishi ndani ya fedha…(Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Tauhida, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.
TAARIFA
MHE.ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naongezea taarifa kwa Mheshimiwa Tauhida kwamba Mbunge huyu pale mkoani ametengwa, anaonekana mchochezi na wakati tumefika hata Mkuu wa Mkoa alilisema hivyo, lakini tunamshukuru Mheshimiwa Rais amemteua kuwa Naibu Waziri. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Tauhida unaipokea taarifa hiyo?
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, nimepokea kwa sababu kwenye suala la kujenga nchi ni lazima twende hivyo.
Mheshimiwa Spika, tumshukuru Rais wetu kwa namna anavyoiongoza Tanzania na kupenda watu wake. Tunakushukuru na wewe kwa kumsaidia Rais kwa kiti ambacho umekikalia, unakitendea haki, unastahili pongezi na unastahili sifa.
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa Wabunge waoga, hatuwezi kuwa Wabunge tunaingia kwenye Bunge lako kuogopa kuzungumza kwa sababu kuna watu wanamiliki fedha, hicho kitu hakiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, cha ajabu ndani ya mkoa kutoka juu mpaka chini, hakuna kiongozi anayeyaona madhaifu hayo, hayupo. Ni kitu ambacho kama Kamati ya Bunge tumeshangaa, kwamba haiingii akilini, hakuna hata kiongozi mmoja na Mbunge anathubutu kupaza sauti yake, lakini anaonekana kiroja.
Mheshimiwa Spika, tunakushukuru, tuendelee kusema tunashukuru kwa mambo makubwa ambayo unatusimamia ndani ya Bunge na kwa hayo, naomba kuunga mkono hoja ya Kamati, ahsante. (Makofi)