Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kutoa mawazo yangu. Nianze kwa kusema, kabla sijasahau kwamba, naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukushukuru wewe kwa kuniamini kuwepo kwenye Kamati hii Maalum ya Uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu, Rais Mkapa aliwahi kusema maneno yafuatayo; “lakini uongozi ni kuonesha njia, kuonesha njia ni kuwafanya watu waridhike kukuona wewe uko mbele na wao wako nyuma wanakufuata, wanakufuata si kwa jambo lolote bali kwa matendo yako, uwajibikaji wako, kauli zako na kadhalika.”
Mheshimiwa Spika, kwa hiki ambacho umekifanya…
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge keti, anayezungumza unamkata pale, ahsante.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, kwa hili ambalo umelifanya umeonesha kwamba wewe ni kiongozi. Matatizo haya, niseme sakata hili, suala hili limekuwepo kwa zaidi ya miaka hamsini, lakini sasa hivi tunaona chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini yako tunaamini wanawake wanaweza, wanawake wana huruma, wanawake ni watu ambao utendaji wao unaonekana kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili mimi nilikuwa naomba kusema yafuatayo; baada ya pongezi hizo, mimi nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Rais awawajibishe pale kwenye ule mkoa kuanzia vyombo vya dola na watendaji wake wote. Uzuri ninafahamu kwamba Kamati hii ilivyoundwa, ulivyotuteua Mheshimiwa Rais wetu anafahamu na anafuatilia. Niwatoe mashaka kwenye jambo hili hakuna mtu atapona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninasema hivyo kwa sababu kuna watu ambao kwenye haya maisha wakishakuwa kwenye nafasi za uongozi wanajisahau sana. Tumekwenda pale, tunaambiwa kwamba taarifa za Efatha zipo Polisi, taarifa za wananchi yale madhila yote ambayo wanafanyiwa taarifa hazipo, inauma sana. Wenzangu waliotangulia wameelezea kwa ujumla wake, lakini mimi nataka kusema kitu kimoja.
Mheshimiwa Spika, siku moja niliwahi kusema kwamba, hii nchi kuna baadhi ya watu na baadhi ya vingozi ambao hata kama wamestaafu au wapo huko nje wanaweza kupigwa mawe ukielezewa waliyoyafanya kwa sababu, haiingii akilini. Kwenye hili nampongeza sana Mwenyekiti wetu wa Kamati Mheshimiwa Profesa Shukrani Manya amefanya kazi kubwa, lobbing ya hawa watu ilikuwa ni ya kiwango cha juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge, Wajumbe wa Kamati, ambao hatukukubali kushikwa kwamba, hiki msikifanyie kazi, hiki msikifanyie kazi. Wale wa mkoani pale walionunuliwa wanajijua wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunakaa unamwita mtu alikuwa ni kiongozi pale kwenye mkoa, unamuuliza hili jambo ilikuwaje? Anaishia tu kusema, jamani kusema ukweli naomba mnisamehe, hili jambo ilikuwa tu ni bahati mbaya, inauma sana. Leo watu pale wanashindwa kulima, leo watu pale wanashidwa kufanya shughuli zao za maendeleo na amewahi kutoka kiongozi mmoja akasema kwamba, wale wananchi pale ile ardhi ni kubwa sana. Kwamba, maeneo ya wao kulima yanatosha kufanya shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekwenda tumeona hali halisi, haipo hivyo. Mimi nilikuwa na wazo lingine pia, miaka ya zamani, miaka ya nyuma huko kwenye hii Serikali ilikuwa mtu akiwa mkurugenzi, pengine labda viongozi wengine wakubwa kwa nafasi mbalimbali, moja kati ya adhabu zao ilikuwa ni mtu akifanya makosa, alikuwa Mkurugenzi Dar es Salaam, wanasema huyu tunakwenda kumtupa Sumbawanga huko. Nadhani Watanzania mtakuwa mnakumbuka.
Mheshimiwa Spika, ilikuwa kuna baadhi ya maeneo yanaonekana kama vile mtu ukitolewa sehemu nyingine ukapelekwa kule ndiyo umekwenda kutupwa. Ninaomba Serikali iangalie imetupa watu wa aina gani huko tunawaletea watu matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu, haiingii akilini mnakaa mnaongea na baadhi ya viongozi, RPC yupo pale, Mheshimiwa IGP najua unanisikia, RPC yupo pale unamuuliza hili jambo limekaa-kaa vipi? Anasema mimi bahati mbaya ndiyo nimeingia mgeni, nina muda fulani. Baadhi ya viongozi pale Mkoani, wanaweza kusema sisi wakati mambo haya yanatokea, wakati madhila haya yanatokea tulikuwa wageni, lakini ulivyokuwa mgeni baada ya kufika hujawahi hata kusikia?
Mheshimiwa Spika, kiongozi mmojawapo pale akasema, mimi sikupata nafasi ya kwenda kuongea na wananchi kusikia matatizo yao na mateso yao, ila nilipata nafasi ya kwenda kuongea na huyu mwekezaji nikanywa naye chai. Roho inauma, hiyo chai ilikuwa imetiwa nini?
Mheshimiwa Spika, niendelee kusema ifuatavyo, maana hizi chai hizi watu huwa wanapewa chai huko wanajisahau wanasaini vitu vya ajabu. Watu huwa wanapewa chai hata huko nje wanatuingiza kwenye matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Taasisi hii ya Efatha, naiomba Serikali kwa ujumla wake ifanye uchunguzi maalumu kwake, lakini pia, vilevile na kwa taasisi zote za uwekezaji Tanzania, aidha ziwe za kidini au wawekezaji wa kawaida na nashukuru sana kwamba kwenye Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ameingia kaka yangu Mheshimiwa Jafo ambaye namwamini sana. Naomba Mheshimiwa Jafo, huu mwavuli wa uwekezaji, in bracket, huu unatutia kwenye matatizo makubwa. Yapo maeneo mengi nchini baadhi ya watu wanalalamika, mashamba yao, maeneo yao ardhi zao, zimechukuliwa na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ifanye tathmini kwa ujumla wake kwenye suala la uwekezaji, lakini kwa huyu mwekezaji huyu, ameshaonesha kwamba, hana roho ya huruma wala hana msamaria mtume. Kwa hiyo, naiomba Serikali huyu mwekezaji imwangalie kwa jicho la kipekee. Maeneo yote ambayo amewekeza nchini, Serikali iweze kuangalia.
SPIKA: Kuna Taarifa, Mheshimiwa Lucy. Inatokea wapi?
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, Taarifa kwa nani tena jamani? Mimi hizi Taarifa. (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Lucy Mayenga kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Francis.
TAARIFA
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ili tuweke Taarifa za Bunge vizuri, uwekezaji haupo tena Viwanda na Biashara, upo kwenye Wizara ya Uwekezaji kuna Wizara yake. Kwa hiyo, nampa Taarifa hiyo.
SPIKA: Mheshimiwa Lucy Mayenga.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ni sahihi ipo chini ya Mheshimiwa Profesa Kitila, lakini na yeye pia, namuamini ni Profesa mzuri, mtendaji mzuri, kwa hiyo, nina uhakika kwamba, mambo yatakwenda sawa sawa, lakini ninachoomba pia, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na masuala ya Uwekezaji na yeye pia, anaingia humo kwa njia moja au nyingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jafo hili pia na yeye yumo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesema kwamba, taasisi hii iweze kuangaliwa upya. Taasisi hii imechukua maeneo mengi sana kwenye hii nchi. Ukiangalia maeneo ya Kilolo taasisi hii ipo, ukiangalia maeneo sijui ya Handeni taasisi hii ipo, lakini katika haya maeneo yote unakuta kila sehemu kuna mgogoro. Kuna kitu gani?
Mheshimiwa Spika, tunaweza tukasema kwamba, baadhi ya hao wenzetu wengine ni taasisi za kidini, kuna baadhi ya mambo labda pengine tuweze kuyanyamazia nyamazia, lakini wanaoumia ni wananchi wetu na wako wengi sana. Nchi za jirani wameshaanza kuchukuwa hatua huko kufungia baadhi ya makanisa, kufungia baadhi ya taasisi za kidini. Wanaamua kufanya namna hiyo kwa sababu, ukilinganisha kinachofanyika na faida kwa wananchi ni mambo ambayo hayaendi katika uwiano unaofaa.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Deus Sangu, kwa jinsi ulivyoweza kusimama bila uwoga katika suala hili. Unapokuwa kwenye jambo kubwa kama hili, hii ilikuwa ni vita maana alishaambiwa kwamba, hatapita, alishaambiwa kwamba, utawekewa watu, alishaambiwa kwamba hutafanikiwa kwenye hili jambo kwa sababu, watu wanawajua wanaokula nao, lakini nampongeza Mheshimiwa Deus Sangu kwa kusimamia hili bila uoga na huu ndiyo uongozi unaotakiwa. Kiongozi ukiwa muakilishi wa wananchi, usipokubali kununuliwa, hakuna jambo litashindikana hata Mwenyezi Mungu atakuwa upande wako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu yupo hapa, Mheshimiwa Dotto Biteko, kwa niaba ya wale wengine ambao hawapo hapa. Naomba na naomba pia, na Mheshimiwa Rais afanye uchunguzi kuhusu viongozi ambao wanafaidika na yule mwekezaji pale Sumbawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi tumefika pale, mtu anaanza kukuita, unajua hili jambo lipo hivi na hivi, unajua hili jambo lipo hivi na hivi. Kuna watu wanafaidika pale, wanalimiwa. Inauma pale ambapo mtu amekaa yupo Wizarani halafu kuna watu wanamlimia kule, wanakuja kumwambia kuna mzigo wako wa magunia 500 ya mahindi, this is not fair and this can only happen somewhere else not in Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja, naomba Waheshimiwa Wabunge waunge mkono, tumefanya kazi nzuri bila kumwonea mtu, ahsante sana. (Makofi)