Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi na nashukuru kwa hizi dakika tano. Naomba niwapongeze Wanakamati kwa taarifa hii nzuri ambayo imemgusa kila mmoja wetu.
Mheshimiwa Spika, Wanakamati ambao wamekwenda site wamejionea mambo mengi. Kwa sisi ambao tunasomewa hapa naamini ni mambo machache tu ndio wanayotusomea. Umefanya busara kubwa sana kutuma Kamati hii. Naomba kwa moyo wa dhati tukupongeze kama ambavyo wenzangu wamekupongeza.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye mioyo yetu Wabunge tunatamani Kamati hii ifike kwa kila jimbo ambako migogoro hii ipo. Mimi binafsi natamani Kamati hii iwe endelevu, iende kwenye maeneo yote ambayo matatizo haya yapo. Ni kwa vile tu muda ni mchache, lakini haya ambayo yameelezwa kwenye shamba hili la Malonje na Mheshimiwa Condester amezungumza hapa kwa jimbo lake na maeneo mengine. Naamini kila Mbunge akisimama, ambao wana mashamba haya makubwa ya wawekezaji wanakutana na matatizo haya, ni dhahiri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi langu ni kwamba kazi hii imefanyika chini ya kiti chako na maelekezo yako na Wanakamati wamefanya vizuri. Pia kimsingi wameepukana na rushwa labda na vishawishi kama ambavyo wamesema.
Mheshimiwa Spika, niombe ikupendeze, Wizara ya Ardhi wakae watafakari. Kuna move ilikuwa imeanzishwa ya kuhakiki mashamba ya wawekezaji ambayo hayatumiki. Ile move naona imeishia hewani. Kuna wawekezaji ambao wanamiliki mashamba, lakini hawafanyi kile ambacho walipaswa kufanya. Nadhani wenzetu wa Wizara ya Ardhi wana Makamishna kila Mkoa, hebu sasa wamalizie pale ambapo kuna kazi ilikuwa imeshaanza ya kuchambua yale mashamba ya wawekezaji ambayo hayatumiki.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwenye nchi yetu kuna wawekezaji wana mashamba lakini hawayatumii ipasavyo. Mimi binafsi jambo hili la Malonje linanigusa kwenye Jimbo langu la Babati Mjini. Kuna Shamba la Dudumera ambalo nimshukuru Mheshimiwa Waziri Lukuvi aliwahi kulitolea maamuzi. Wananchi wa Dudumera lakini na wananchi wa Singu, mashamba mawili haya nimekuwa nikiyasema na natolea mfano. Mheshimiwa Waziri Lukuvi alilitolea maelekezo Shamba la Singu kwamba wananchi wapewe ekari 829, lakini mpaka leo hakuna maamuzi, mpaka leo yaliyoagizwa hayatekelezwi. Katika shamba hili kulikuwa na maelekezo ya Wizara, lakini kule chini kwenye mikoa maamuzi haya hayafanyiwi kazi, wananchi wanateseka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi langu kutoka moyoni hii kazi iliyofanyika ni kubwa na ni nzuri. Hebu tuombe sasa iwe ni wakeup call kwa ajili ya maeneo yale ambayo kazi hii haijahitimishwa ili wale wananchi wapate haki kwa sababu huu unyanyasaji wa kupiga wananchi risasi siyo jambo jipya, lipo katika mashamba haya. Wawekezaji kutokufanya uwekezaji siyo jambo jipya. Nadhani huu mzigo Waziri wa Ardhi sasa akae chini na achukue data ya maeneo yote ili waweze kuona nini cha kufanya.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kauli imezoelekea, tuwe wakweli. Mbunge anaposema matatizo ya wananchi wake anaonekana mchochezi. Mimi binafsi nilishawahi kuitwa mchochezi. Unapokwenda site unachukua maumivu ya wananchi, unayapeleka kwenye Serikali, Mbunge anaonekana mchochezi. Pia, baadhi ya viongozi hawa wamekuwa wakirudia kauli hizi hizi.
Mheshimiwa Spika, ombi langu viongozi wa aina hii wachunguzwe. Mtu anasema nilikuwa nimekaa na mwekezaji lakini kwenda kwa wananchi ambao Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amempa dhamana hiyo kwamba nenda ukanisaidie kwenye mkoa huu na kwenye wilaya hiyo, hakai na wananchi. Yuko tayari kukaa na mwekezaji kunywa chai, halafu mwananchi ambaye kupitia Mbunge au Diwani akiomba kwamba wananchi watendewe haki, Diwani anaitwa mchochezi, Mbunge anaitwa mchochezi, lakini mtu yuko tayari kukaa na huyo mwekezaji na hakai na wananchi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana, kengele imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)