Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA – MWENYEKITI WA KAMATI MAALUM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja ambayo imeletwa mbele ya Bunge lako Tukufu. Nitambue kwamba hoja hii imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 14 na kwa kadri ya michango ya Wajumbe wote walikuwa wana-support mapendekezo ya Kamati Maalum.
Mheshimiwa Spika, nianze pale ambapo Mheshimiwa Musukuma ameongea habari ya valuation, kusema ukweli pendekezo letu la kwanza linatokana na mtiririko wa mapungufu katika manunuzi na mauzo ya Shamba la Malonje.
Mheshimiwa Spika, kwanza Baraza la Mawaziri maelekezo yake kwa Mkoa wa Rukwa yalikuwa ni shamba hili ligawanywe katika vipande vya hekta 50 na wapewe wafugaji wadogo wadogo. Maelekezo ilikuwa ni kugawa katika hekta 50 na iwapo Mkoa ungepata changamoto yoyote katika kushughulikia jambo hili walikuwa wameelekezwa waweze kurejea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mchakato wote wa kulipata shamba una mapungufu makubwa ambayo ndiyo yamepelekea Kamati yako Maalum kufikia pendekezo lake la kwanza. Kwa sababu Mkoa badala ya kwenda kupima shamba hili kwa hekta 50, 50 badala yake wakatangaza tangazo la ekari 3,000 kuuza na baada ya tangazo hili kutolewa, mwekezaji akapendekeza yeye mwenyewe kwamba atahitaji 10,000.
Mheshimiwa Spika, Mkoa ukamkubalia kumuuzia 10,000, Kamati yako ilipotamani kupata valuation report, tathmini haikupatikana, sasa milioni 600 ilipatikanaje? Haikujulikana badala yake yaonekana kabisa kwamba mkoa ulikaa na mwekezaji wakapanga mezani hatimaye wakafikia bei ya milioni 600 na mchakato huo unapata kasoro zaidi pale ambapo shamba linakubaliwa kwamba hekta 10,000 zitauzwa, lakini upimaji haukufanywa kabla, kwa maana ya kwamba upimaji umekuja baada ya mauzo kufanyika.
Mheshimiwa Spika, sasa hayo mapungufu hayawezi yakahalalisha yale yote yaliyokuja kuendelea na iwapo matokeo yake yangekuwa bora basi tungesema mapungufu haya yamejijenga, lakini mapungufu haya yanatoa matokeo ambayo ni mabaya kwa sababu mchakato tangu mwanzo ulikuwa umekosewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa manunuzi yamefanyika, upimaji ukaja baadaye, lakini Kamati yako pia ikagundua kwamba ukubwa wa shamba ulipokuwa umekabidhiwa kutoka Wizara ya Mifugo ilikuwa ni ekari 37,000 (hekta 15,000) lakini inapokuja sasa kwenye hali halisi baada ya mwekezaji kupewa 10,000 ambazo zilipimwa post-manunuzi, zinabaki 3,400 peke yake badala hata ya zile 5,000, kwa maana ya kwamba hata kama makadirio yalikuwa ni kwamba wananchi wapate hekta 5,000 bado walipata 3,400 na ukiondoa zile za Gereza la Mollo wakaja kuishia kupata 2,600.
Mheshimiwa Spika, wale wa Halmashauri ya Sumbawanga DC. walipendekeza kwamba basi hivi vitalu 51 vilivyopatikana wapewe wananchi wetu bure kwa sababu hata uwezo wao wa kununua si mkubwa. Jambo hili halikukubalika badala yake vikauzwa na vikauzwa kwa shilingi milioni 2.5, lakini kwa watu ambao ni nje ya wale wananchi wanaozunguka vijiji. Kwa hiyo, watu wa Mjini Sumbawanga, wafanyabiashara na viongozi wa Serikali pamoja, kitu ambacho Kamati ilisikitika kidogo niki-point out kwamba hata baada ya mwekezaji kuwa amepata hekta10,002 bado katika vile vitalu pia anaonekana akiwa ananunua na vitalu, rekodi hizo zipo na zilitia mashaka juu ya mchakato mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mchakato huu wa manunuzi ulikosewa na baada ya hapo, mkataba pamoja na hati ya umiliki ya mwekezaji ilikuwa ni kufuga, nakumbuka kile kipengele ni kifungu cha sita na saba cha ule mkataba, ambao kimsingi kwa tathmini ya Kamati ulikuwa ni mkataba ambao nao haukidhi viwango vya mkataba.
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 6 na 7 kinasema ni kwa ajili ya kufuga na malisho kama dhamira ya kwanza ya Baraza la Mawaziri kuashiria kwamba haya mambo yalijulikana Mkoani pale ndiyo maana yanaingia kwenye mkataba na hati ya umiliki, lakini mwekezaji anafuga kidogo, Kamati mtakumbuka tulikuta ng’ombe wasiozidi 200, walisema ni 140 hivi na hii ni miaka 17 ya ufugaji. Hata kama huwa wanauza na kula nyama, lakini ng’ombe 170 na kama dhamira ilikuwa ni kufuga, sasa wakafuga na hati ya umiliki na mkataba wa mauziano ukarejea dhamira ya Baraza la Mawaziri. Kwa maana ya kwamba haya mambo yalijulikana lakini badala yake kilimo kikatiliwa mkazo. Serikali ikaacha kufuatilia utekelezaji wa mkataba, mwekezaji akaendelea na kilimo.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya Kamati inakazia tu kusema kwamba inawezekana baada ya kugundua kwamba masharti ya mkataba hayatekelezeki vizuri, mwaka 2021 Hati ikaongezea kilimo, mifugo pamoja na upandaji miti ili sasa mambo yawe halali, lakini hiyo hata kama imefanyika mwaka 2021 ni baada ya miaka 14 baadaye. Kwa hiyo masharti ya mkataba hayakutekelezwa na Serikali haikumsimamia vizuri.
Mheshimiwa Spika, nirejee kusema kwamba pendekezo la Kamati la kwanza ambalo ni kubatilisha, Serikali ibatilishe umiliki wa Shamba lote la Malonje ikiwa na maana ya Shamba la Efatha pamoja na mashamba yanayozunguka vikiwemo vitalu 51.
Mheshimiwa Spika, wazo hili siyo jipya, wazo hili na dhamira hii ilishakuwepo mwaka 2015 ambayo ilikuwa ni kubatilisha shamba hili, lakini kama ambavyo taarifa yetu imesema ni kweli kwamba kukaingiwa na utendaji mbaya upande wa Serikali kwa sababu Kamishna wa Ardhi ndiye aliyepaswa kushtakiwa, lakini akashtakiwa Mkurugenzi wa Manispaa, Mkurugenzi wa Manispaa naye akaingia hati ya maridhiano huku akijua kwamba siyo mwenye ardhi! Kilichokuwa na sintofahamu kubwa ni pale yule aliyetia saini kusema kwamba hii si saini yangu kwa maana ya kwamba hati hiyo imegushiwa. Pia kimekuwa ndiyo kigezo nakumbuka barua ziliandikwa nyingi kuelekeza kwamba mwekezaji asisumbuliwe na asibugudhiwe baada ya ile Hati ya Maridhiano.
Mheshimiwa Spika, mambo haya ndiyo yaliyoipelekea Kamati yako kwamba tunaona mapungufu makubwa upande wa mwekezaji, lakini pia na upande wa Serikali wa jinsi ambavyo mgogoro huu umekuwa ukishughulikiwa. Kwa hiyo kwa sababu Wajumbe wote waliochangia wamekubaliana na mapendekezo ya Kamati naweka msisitizo kwamba pendekezo letu la kwamba shamba hili libatilishwe umiliki wake liendelee kusimama.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali ijue kwamba ina sababu ya kutokukubaliana na ile amri ya Mahakama kwa sababu kuna kughushi pale ndani na kwa hiyo inaweza ikafanya marejeo kwa sababu mhusika Kamishna wa Ardhi siye aliyeshtakiwa badala yake alishtakiwa mtu mwingine.
Mheshimiwa Spika, tumesisitiza pia habari ya kusimamia Kanuni za Ardhi, lakini pia na usimamizi wa kampuni za ulinzi nchini, maana tumegundua kwamba kampuni zaweza zikatoa mafunzo tena ya kutumia silaha za moto kwa watu wake na hao wakaenda kutekeleza bila kuwa na weledi wa mafunzo ya mgambo wala JKT vitu ambavyo ndivyo vigezo halisi vya wanaopaswa kuajiriwa katika kampuni binafsi za ulinzi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo na ufafanuzi huo naliomba Bunge lako sasa likubali kupokea taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na vijiji vinavyolizunguka shamba hilo kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)