Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Maliasili na Utalii. Kwa kweli, na mimi nachangamana na wenzangu waliopita kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi alivyochagiza katika kuleta utalii wa hali ya juu sana Tanzania. Kwa kweli, nchi yetu sasa hivi imefunguka na ninajua kwamba, tutaendelea kupata mapato mengi kutokana na watalii. Pia, ninampongeza Spika wetu, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, maana na yeye kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani amesaidia pia, kututangaza Tanzania kwa hiyo, ni sehemu ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na watendaji wake wote, Waziri, Naibu Waziri, pamoja na watendaji wote wa Wizara hii na mashirika yake. Kipekee pia, naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa ripoti yake ambayo kwa kweli, imetaja maeneo muhimu sana ambayo yanatakiwa yaangaliwe na Bunge hili kwa undani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wakati napitia hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii nilikuwa najiuliza maswali, hivi ni kwa kiasi gani tembo wanaonekana ndiyo wanyama ambao wanatakiwa wahifadhiwe kwa gharama zozote zile, ili watalii waweze kuja? Je, Serikali imeshawahi kufanya hata utafiti kidogo kuona hawa watalii wengi wanaokuja wanavutiwa na kitu gani zaidi? Kwa nini nauliza hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza hivi kutokana na sababu moja kubwa kwamba, kwenye Biblia, Hosea Nne, Mstari wa Sita, imeandikwa “Watu wangu wanaangamizwa kwa kuokosa maarifa.” Pia, ukiangalia Mwanzo Moja, Mstari wa 26, inasema “Mungu ametupa mamlaka ya kutawala wanyama wote na kila kiumbe chenye uhai,” lakini inaelekea kama sasa hivi tunaelekea mahali tutatawaliwa na wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kilio cha wananchi kila sehemu na umetajiwa na kamati yako hapa. Halmashauri ambazo zinakumbwa na tataizo hili la wanyamapori kuingilia wananchi kwenye mashamba yao, kuharibu mimea, mazao, kuua wananchi ni janga ambalo linatakiwa tusilifumbie macho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninauliza, hivi hawa tembo tumeshawahi kufanya utafiti kuona carrying capacity yao kwa maeneo yaliyotengwa itachukua muda gani, ili yasiweze yakazidi lile eneo mpaka ikabidi wananchi watolewe tena, ili tembo wapate nafasi za kuishi? Nimeona ambavyo Serikali au wizara imejitahidi kweli, wanafanya jitihada kubwa, lakini mimi ninaangalia nikiwa pia, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu inayoangalia Matumizi ya Fedha ya Serikali. Ni helicopter ngapi zinahitajika tununue? Ni walinzi wangapi ambao watasimama tu kungojea tembo aje, ili wamrudishe kwenye hifadhi bila kuzalisha? Je, ukiangalia wenzetu wanasema cost benefit analysis ukiifanya, unaweza kuangalia hizi gharama ambazo zinawekwa kulinda tembo au wanyama waharibifu zinalingana na kile tunachopata kwenye utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge aliyepita ameongea sana kuhusu maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuleta watalii wengi. Kwa nini Tanzania tumeonekana kwamba, wanyama sasa ndiyo wana umuhimu na ndiyo wana hadhi au wana thamani kuliko binadamu? Hili ni jambo ambalo lina hatari sana. Itafika mahali ambapo wanyama wanaweza kuzidi binadamu halafu ikawa matatizo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri inapoonesha kwamba, wanyama wanaweza kuvunwa, ili tukaacha kiasi kile kinachotakiwa kutokana na eneo lililopo na kwa muda gani wanyama hawa wanaweza kuishi katika eneo hilo bila kuhitaji kufukuza tena wananchi kwenye maeneo yao. Mimi kweli, ninamefurahi kwamba, tunajitahidi. Wizara ya Serikali inajitahidi, lakini unaposema unampa mwananchi mabomu ya kufukuza hawa tembo, je, wanafukuzwa mchana au wanafukuzwa usiku?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni usiku, mwanchi amelala na mabomu yake, tembo huyo anamuamsha kwamba, amka nakuja, ili bomu lifanye kazi au atamvamia kabla hata hajatumia lile bomu? Kwa hiyo, unaangalia wananchi wetu usiku wapigane na tembo, mchana, ngedere na ndege kweleakwelea, sasa huyu mkulima kweli, maisha yake yatakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kwamba, tuna haja ya kuangalia pia, njia nyingine za kuweza kudhibiti hawa wanyama. Kwa mfano, tukitumia traditions au njia za asili, kuchimba mitaro yale maeneo ambayo tembo hawezi kuvuka naamini kwamba, mitaro ile itasaidia wale tembo hawavuki kuingia kwenye maeneo ya wakulima maana watajua kwamba, wakishuka wanaakili, tembo wanajua wakiingia kwenye mitaro hawatatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu jambo lingine ni sisi jana tulikuwa na kikao na semina na wenzetu wa Mamlaka ya Usimaizi wa Bima Tanzania (TIRA). Tukaongelea kama kuna wadau wa bima ambao wanaweza kusaidia wakulima wakipatwa na maafa ya mafuriko au jua kali, ukame; je hawawezi kuwa na bima ya kusaidia hawa watu, wakulima, ambao wanapata adha ya kuliwa mazao yao na kuuwawa, hasa na Tembo? Wenzetu TIRA walisema hilo linaongeleka na wakasema wapo tayari kukaa na TANAPA kuongea na kuona jinsi ambavyo wanaweza kuwasaidia hao wakulima, ili kuona kwamba, mazao yao yatakapoharibiwa na hawa Wanyamapori watawezaje kuwasaidia, pamoja na wale watakaouwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana kama mlivyosikia kamati ikisema kwamba, wakulima wanataka wafidiwe sawasawa na thamani ya mazao yao more than kusema nampa laki au nampa ngapi, laki moja ni sawa na mbolea ya nusu ekari tu. Sasa huyo mkulima amepoteza, kwa mfano kule kwetu mpunga ambao akiuza mazao ya eka moja anapata shilingi milioni tatu, leo unampa shilingi laki moja kwa kweli, hilo ni uonevu mkubwa sana kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri TANAPA, kupitia Wizara hii, wakae na wenzetu wa TIRA waone jinsi ambavyo wanaweza kuwasaidia hawa wakulima. Kama kuna bima ya afya kwa wote pia, inawezekana kuwa na bima ya maisha kwa wote. Ripoti ya CAG imeonesha kwamba, katika Mwaka 2022/2023 TTB ilikuwa na bajeti ya shilingi bilioni moja na milioni 100.13 na hiyo ilikuwa kwa ajili, ya kuwa na matamasha mbalimbali, mikutano mbalimbli huko Ulaya, Bara la Asia, Marekani, Kusini na Kasikazini, lakini haikutolewa hata senti moja ya hawa wenzetu wa TTB kufanya shughuli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunajiuliza hili shirika lipo, kwa ajili gani? Kama hatuwezi kuliwezesha liendeleza promotion ya watalii sasa lipo, kwa ajili ya kufanya nini? Kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo, ili kuona jinsi ambavyo wataweza kuisaidia hii TTB iweze kufanya kazi yake kikamilifu. Pia, kuongeza walimu wa lugha katika vile vyuo vya ufundishaji watalii kwa mfano, sasahivi tunapata watalii wengi wanaongea Kifaransa, Kichina, Kirusi na Kijerumani. Inatakiwa na sisi tujipange vizuri kwamba, wale wanaoongoza utalii na wao wawe competent katika hizi lugha, hii itatusaidia sana kutoa impression kwamba, tupo serious katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nawapongeza pia, Wakala wa Misitu kwa kazi wanayoifanya. Tunaomba waendelee kupanda misitu kila sehemu inayowezekana, ili tuongeze ukaa ambao utatuletea fedha kitaifa na kupunguza gharama nyingine katika bajeti zetu. Naomba kusema kwamba, nakushukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa, ahsante sana. (Makofi)