Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, Mwenyekiti makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati kabisa niipongeze Kamati ya Maliasili na Utalii, imefanya kazi ya Kibunge, imetusaidia kazi, wajibu wetu Wabunge, Bunge hili kuiheshimisha Kamati ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwenye taarifa ya Kamati ukurasa wa 33 ongezeko la bajeti kwa Wizara ya Maliasili na Utalii bilioni 19. Bilioni 5 iende kwenye miradi ya maendeleo, bilioni 14 OC. Maombi ya hovyo ambayo Bunge hili tusikubali kuyapitisha. Maombi ya matumizi mabaya ya fedha za umma, maombi ya kifisadi, maombi ya anasa. Mnaleta maombi kama haya? Kuna taasisi chini ya Wizara hii haina ofisi? Mnatuletea maombi kama haya ya kwenda kuzurura, kuna taasisi chini ya Wizara hii ina madeni? Mnatuletea maombi kama haya kwenye hotuba ya Waziri ametenga bilioni mbili kwenda kulipa wananchi fidia walioathiriwa na tembo? Mnatuletea maombi kama haya tumetoka kwenye bajeti ya maji mmepunguza pesa za wananchi kutopata maji, mnatuletea maombi kama haya kwenda kwenye OC?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa bajeti ya Ujenzi ilikuwa hatari, barabara zimeharibika huko wananchi wanashindwa kupita? Mnataka Bunge kama hili tupitishe anasa hizi, no, Hapana! Hizi pesa za walipa kodi zitalindwa zikafanye mambo ya msingi katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naangalia hapa hii Wizara, Bodi ya Utalii imejenga kituo kizuri kabisa cha kutangaza utalii kidijitali, imetumia bilioni moja, huu mwezi wa 20 hakitumiki. Halafu kuna watu wanataka kwenda kuzurura tu huko. Wenye kazi yao hapa ya kutangaza utalii mnawanyima hela, haya Kamati wamewaambia huko tangu mwaka jana hamsikii, kwenye ripoti ya CAG ameandika aibu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka miwili kituo kimekamilika mmeshindwa kulipa milioni 228 kwa ajili ya kuanza kazi. Mnategemea tu Mheshimiwa Mama Samia na royal tour yake nyinyi mnashindwa kutimiza majibu yenu ya msingi, halafu mnataka tufikie idadi ya milioni 5 ya watalii katika Taifa letu kwa mambo haya ya hovyo. Hatuwezi kuruhusu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Bodi ya Utalii imetengewa bilioni 4 hawajawapa yote, wamewapa bilioni 3 wanatuletea huku maombi ya bilioni 14 ya anasa huku vitu vya msingi vya kuongeza utalii Serikali yetu, nchi yetu ipate mapato mnashindwa kupeleka pesa huku? Mnatuomba bilioni 14 sisi ya OC huko? Hii si sawa, hili ni Bunge la wananchi tufanye kazi ya wananchi. Mnatenga bilioni mbili watu huko wamekatwa miguu na tembo wenu, hamuwalipi fidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja Nyatwali, Kata ya Nyatwali yenye mitaa mitatu, mtaa wa Tamau, mtaa wa Serengeti na Nyatwali iliyopo Jimbo la Bunda Mjini Mkoa wa Mara. Hatukuzaliwa Mkoa wa Mara kwa bahati mbaya, sikuzaliwa Bunda Mjini kwa bahati mbaya, nimezaliwa kutetea haki za wananchi mnaowanyanyasa, wananchi wa Nyatwali. Aibu, Serikali kwenda kutaka kupora ardhi kwa dhuluma ili tembo wapiti! Hatukatai tutawaachia ardhi lakini hatutaki muwaache wananchi wa Nyatwali na umaskini wa kutupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kaya 1,200, kuna wakazi 13,000. Mmefanya tathmini miaka miwili, mmewaacha na umaskini kule. Mnataka kwenda kuwatoa kwa square meter shilingi 490? Ardhi ambayo ni lango kuu la kuingia Serengeti. Maeneo ya jirani kwenye Halmashauri ya Mji wa Bunda wametangaza square meter moja inauzwa shilingi kuanzia 2,200 - 5,000. Mnawachukuwa ardhi yao wawe maskini? Mnawalipa 470? Shilingi? Hata hela ya coca ni kubwa kuliko ardhi yetu ya Bunda. Wananchi mmewaacha kwenye umaskini, mmewafanyia tathmini hawawezi kufanya maendelezo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zimechakaa mmewakataza kujenga zaidi ya familia 300 zinalala nje, yamepita mafuriko wengine mmewasaidia, watu kule wanakaa juu ya bati kwa sababu mnataka kutwaa ardhi yao. Mmefanya tathmini hamjawaandalia mahali pa kwenda, mnataka kuwaondoa kwa gharama ndogo kwa ajili ya tembo. Sawa, mnawapeleka wapi? Tumesikia sijui wapi huko, mmewajengea nyumba, mmewafanyia nini. Wale hata pa kuwapeleka hamuwaambii. Eneo mnawapa square meter shilingi 470, waende wakanunue ardhi kwa square meter shilingi 5,000, waende wakanunue ardhi kwa mita shilingi 2,200? Kwa nini mnataka kunyanyasa wananchi maskini? Why? Hili halitakubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wale wapo kama kwenye kisiwa halafu mnaenda kuwatisha tisha na wamesema hawataki ziara za viongozi tena kwenda kuwatumia kisiasa, wanataka muwalipe pesa kwa hadhi na thamani ya ardhi yao. Leo hawajui hatima yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza daftari la kuandikisha wapiga kura enhe! wao wanaenda wapi? Wakose haki yao ya kupiga kura? Mtawapeleka wapi? Hili halitakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya tembo, Halmashauri ya Mji wa Bunda wamefanyiwa tathmini mwaka 2021, zaidi ya wananchi 1,200 mpaka leo hamjawalipa fidia halafu mnataka tuwapitishie bilioni 14 hapa kwenda kuzurura? Sisi hatuwezi kukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao tangu mwaka 2021 wanadai, sasa leo mfugaji akosee kidogo tu hatusemi waingie kwenye hifadhi, akosee kidogo tu aingie kwenye hifadhi milioni moja, akichelewa mnaenda kuuza akiingia kwenye hifadhi. Hili hatuwezi kukubali. Tulipeni fidia, mpaka sasa ivi jumla ya wananchi 2,000 wanadai waliofanyiwa tathmini ni hawa hawa 1200 na zaidi, 1,008 bado hamjafanyia kazi, hamjawaingiza kwenye mfumo wa malipo. Hatuwezi kukubali mnyanyase wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tutafutieni maeneo kama maeneo mengine na mtulipe fidia kutokana na thamani ya ardhi yetu. Wale siyo takataka wale. (Makofi)