Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunifanya niwe wa mwisho kwenye kipindi hiki cha asubuhi. Mimi nianze kwa kumsifu na kumshukuru mtukufu Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwa mdau wa kwanza wa Sekta hii ya Utalii na kujua kwamba, Sekta hii ya Utalii ilitakiwa iwe ni Sekta ya kipaumbele baada ya Sekta ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Utalii pekee ndiyo inaweza ikatuletea ukuaji mkubwa wa Pato la Taifa kwa wakati bila kuwekeza sana. Halafu pia, inaweza ikatusaidia sana kuongeza fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kwamba, unapozungumza kwa mfano Sekta ya Madini ambayo tumeichangamkia. Sekta ya Madini fedha yote ya mapato yake inayopatikana, mapato yake yote makubwa yanaishia nje na fedha za kigeni zinazokuja pengine unaambulia asilimia sita ile ya mrahaba tu. Kwa hiyo, mimi nasema hii ni Sekta muhimu na bila kupoteza muda ninataka nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Utalii, Mheshimiwa Kairuki pamoja na Naibu wake na viongozi wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema hiyo kwa mambo tuliyosikia toka asubuhi yakisomwa kutoka Buchosa, halafu baadaye tukasikia kutoka kwa Kamati na kwenye hotuba yenyewe ya Mheshimiwa Waziri inahitajika pengine tufanye upya tathimini ya sera, sheria na kanuni za hifadhi za wanyamapori na hifadhi za misitu kwa sababu kuna changamoto nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona kwamba tunaendelea kutenga hifadhi bila kujali kwamba wanadamu nao wanahitaji sehemu za kukaa na halafu hizi hifadhi zinakuwa ni heritage ya dunia nzima. Sasa inavyokuwa vile, ni lazima Dunia nzima iwe inachangia kwenye kufidia wale watu au wananchi wanaohamishwa au wale wanaopata athari mbalimbali. Kwa hiyo, somehow tutafute njia ya kuwalazimisha wenzetu kwenye hizo nchi tajiri waweze kuwa wanachangia kwenye athari zinazotokana na uhifadhi huu wa hifadhi za wanyama pamoja na misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, kwa mfano pale kwangu, kwenye Jimbo langu la Vunjo, Kijiji cha Komela, Kitongoji cha Komela, tarehe 09 Mwezi Mei, mwaka huu, askari wa hifadhi walimpiga risasi mbili kijana wangu na mpigakura wangu mwenye miaka 39, Octavian Temba. Baada ya kumpiga kijana huyo alikufa pale pale. Kijana huyo aliacha familia ya watu watano, mmoja akiwa bado hajazaliwa lakini wanne wakiwa ni wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nikasema, kweli nilitakiwa nilete hoja binafsi Bungeni hapa lakini nikajizuia sana. Nikatumia nguvu zangu sana kujizuia nisilete ile hoja wakati ule kwa sababu walisema ngoja uchunguzi ukamilike; lakini zaidi nilisaidiwa na Mheshimiwa Waziri msikivu. Mheshimiwa Waziri alinipigia simu akaniambia subiri tuone sheria itachukua mkondo wake na kweli wale askari walikamatwa na kuwekwa rumande. Sijui wamefikia wapi lakini tunafuatilia jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni kwamba, pamoja na kwamba KINAPA walishiriki katika mazishi ya yule kijana baada ya wananchi kuwa wakali sana na kuvuruga miundombinu lakini nafikiri lazima Serikali itoe tamko lingine, kwamba hata rambirambi hawajatoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe rambirambi kwa familia iliyobakia. Ni watu masikini na ni watoto. Watoe rambirambi na ninaomba kwamba Serikali iweze kutoa neno au kauli kwa suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwamba Kamati na pia hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeelezea kwamba, inataka kuongeza fidia kwenye maeneo hayo yanayotokana na hifadhi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu kijana alikuwa anakata majani tu ya ng’ombe. Kwa hiyo, alikuwa hakati mti au hafanyi chochote. Naomba hicho kifanyike na hiyo Sheria sasa ikiwa reviewed, tuweze kuona ni namna gani tutaingiza masuala mazima ya kuvuna wanyama, masuala mazima ya carbon trade. Hii carbon trade inatakiwa kuleta fedha za kufidia wale watu wanaokaa jirani ambao walikuwa wananufaika kukata majani na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hile concept ya carbon trade mimi niliizungumza hapa baada ya hili suala la nusu maili kushindikana, nikasema basi tufanye carbon trade hela ikipatikana, sehemu ya ile hela iende kwa wale wananchi wa vijiji vinavyozunguka ile milima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa utalii, natoa pongezi sana kwa TATO na TAHOA, ambao wameingia wenyewe wanaanza ku-market. Wanaenda kwenye Soko la Dunia na kwenye mikutano ile mikubwa wanaenda kuuza utalii wetu wakati hapo zamani ni Serikali ndiyo ilikuwa inafanya yenyewe. Sasa hivi binafsi wanaenda na ndiyo sababu wanaleta tija na ongezeko kubwa linatokana na jitihada za kutangaza za watu binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hivi, lazima tuwasaidie. Nashukuru Mheshimiwa Waziri ametangaza kwamba, tozo zinatolewa na leseni zinafanywa upya kwa mfumo mpya. Nasema kwamba, tatizo la watu wanao-operate biashara hapa nchini, wote tunaowasikia wanasema tatizo pamoja na hizo tozo kuwa utitiri lakini zikusanywe na mamlaka moja. Hiyo mamlaka moja izisambaze kwenye zile mamlaka nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa issue ya kwamba mtu mmoja anaenda kulipia leseni au kulipia levy mahali kwa watano na hajui ni wangapi kwa sababu wanaongezeka siku hadi siku inakuwa inaongeza sana gharama ya kufanya biashara hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sasa pamoja na haya yanayofanyika basi kwa kusaidia wafanyabiashara wote basi Mheshimiwa Waziri azungumze na Mheshimiwa Waziri mwenzake ili tuhakikishe kwamba hizi tozo zinakusanywa mahali pamoja. Pia, tozo hizo kuna zingine hata hazi-apply. Kuna hizi mamlaka zote za NEMC, CAMARTEC, LATRA, TBS, TARA kwa upande wa hawa, Local Government Authority na wenyewe wanakusanya service levy, inakuwa very difficult. Kwa hiyo, naomba hilo suala lichukuliwe na litiliwe maanani na mambo haya yakamilike kama inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba niishie hapo. Naunga mkono hoja. (Makofi)