Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika ratiba hii ya jioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye Wizara moja kwa moja naomba nianze kwanza kwa kuipongeza Serikali, hasa kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameweza kukuza utalii na hasa kupitia ile Royal Tour. Tumeona sehemu kubwa mapato ya kitalii yameongezeka sasa maradufu. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi tu pia niseme kuwa ninawapongeza sana Mawaziri katika Wizara hii, Mheshimiwa Kairuki pamoja na Mheshimiwa Kitandula. Wizara hii huwa ina changamoto nyingi sana, lakini wanafanya kazi nzuri sana, hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tulipewa dakika nane mimi niende chap chap kwenye masuala ambayo ninayaona kuwa ninaweza kuyazungumzia ili nisirudie ya wenzangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta yetu ya utalii inakuwa sana, lakini ukiangalia hata kwenye maoni ya Kamati, mimi nipo kwenye Kamati hii ya Ardhi, Maliasili na Utalii, utegemezi bado ni mkubwa, ukiangalia bajeti kwenye maendeleo katika Wizara hii bajeti kubwa ni tegemezi, kwa maana ya kwamba tuna kama 32% ambayo sasa ndiyo mapato ambayo ni ya ndani, lakini asilimia takribani sitini na kitu ni mapato ya nje, hii ni hatari. Tunatakiwa tutoke hapo, Wizara iangalie namna ya kuweka mkakati ili tuweze kupandisha mapato yetu ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 32 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna lile suala la uvunaji wa wanyama wakali na waharibifu. Kuna kitu kimenishangaza kidogo, kwa mwaka 2022/2023 ukiangalia ile orodha nimeshtuka kidogo kwamba wanasema waliweza kuvuna nyani 10, viboko 28, mamba 21 na wanyama wengine, lakini nikiangalia tatizo la nyani lilivyo kubwa mwaka 2022/2023 nyani 10? Hawa kila mimi ninapokwenda Tabora naweza nikakutana nao tu pale Nyahua zaidi ya nyani 100 wapo barabarani wanavizia mahindi ya watu na mazao mengine. Sasa kwa nyani 10 tu sijaelewa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata upande wa viboko, kwa viboko 28 ni kidogo sana. Mimi nina tatizo kubwa sana, kwa mfano kule Tabora tuna Bwawa la Igombe, viboko ni wengi na nimeshawahi kuzungumza hata kwenye Wizara, kwamba tuangalie namna gani ya kuvuna wale viboko ili kuwapunguza, kwa sababu watu wengi sana wanauwawa maeneo yale, hasa Kata ya Kabila na Kata ya Misha - Tabora Mjini kumekuwa na majanga makubwa sana ya viboko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa uvunaji huu niliouona hapa wa kweli Mheshimiwa Angellah pamoja na ndugu yangu, Naibu Waziri Mheshimiwa Kitandula mzidishe speed kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mbuga nyingi ambazo zina upungufu wa wanyama, zipo. Kuna mbuga nyingine unaweza kukuta kuna nyati tu na wanyama wengine, wengine hawapo. Waangalie namna mnavyoweza kuvuna wale wanyama na kuwapeleka mbuga zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanyama kwa mfano tembo, mimi ninavyofahamu tembo ni mmoja kama siyo wa kwanza basi hawezi kuvuka wa pili. Tembo ana kumbukumbu kubwa nadhani kuliko wanyama wengine wote. Zile njia zile ambazo zinaitwa shoroba, tembo hata kama alipita miaka 100 iliyopita leo anaweza kupita tena pale pale. Sasa wangeangalia namna ili sehemu kama zile wakaweka uzio (fence). Uzio uwe katika maeneo yale tu ambayo wanaweza kutoka, inaweza ikasaidia sana, kwa sababu lazima apite pale pale. Hata hapa Chuo Kikuu cha Dodoma wamewahi kuja kwa sababu inaonekana miaka hiyo walikuwa wanakuja kula sehemu zile. Kwa hiyo waangalie namna mnaweza kuwadhibiti wanyama katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malikale, tulikwenda Kilwa na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake wanahudhuria sana ziara za Kamati. Mali kale ni muhimu sana, tume-base sana kwenye wanyamapori zaidi na tunasahau malikale. Ule Mji wa Kilwa, aliongea hata Mheshimiwa Ndulane asubuhi, una historia kubwa sana. Mji kama Kilwa kuwa na currency yake, si tu kwamba ilitumika East Africa, tuliambiwa mpaka Australia. Leo ile misikiti 99 iliyotajwa hapa tulikwenda tukakuta misikiti kama minane tu hivi nayo tunaambiwa ilifukuliwa fukuliwa. Kule chini ya ardhi kuna misikiti isiyopungua 90 ya miaka hiyo kwa mujibu wa watu wa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna historia kubwa, ndugu yangu Mheshimiwa Ndulane naona hakuitaja hapa, wale wazee si tu kwamba walijua kuandika wakati ule, kwa ndugu zetu Waislamu tulipokwenda pale tuliwaambia wale wazee miaka hiyo kuna wazee waliondoka na melikebu walikwenda kuonana na Mtume Mohamad kule Saudi Arabia na walionana naye na wakarudi. Wazee wale hakuna historia yao, wazee wale hata majina yao tulipouliza hayakuhifadhiwa, kitu cha namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala kubwa sana la utalii hata kidini. Ule Mji wa Kilwa tulielezwa kwamba katika miaka hiyo ule mji ndio ulikuwa kati ya miji 200 ya dunia ambayo ilikuwa inaongoza kwa uzuri na biashara. Wakati ule baada ya biashara ya utumwa kuwa ceased, wale walikuwa wnaongoza kwa biashara ya dhahabu na biashara zingine. Haya mambo yamekufa kwa kiwango kikubwa, mji ule unazidi kuwa ni mji ambao sasa vile vyanzo vya utalii vinaendelea kupotea. Kwa hiyo, nadhani ni vizuri, kama inapatikana nafasi, kufukua maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la migogoro ya mipaka; migogoro hii ya mipaka ni lazima iwepo kwa sababu ongezeko sasa ni kubwa, tupo watu milioni 62 plus, watu wameongezeka sana, kwa hiyo na makazi pia lazima yaongezeke. Watu wetu lazima watafutiwe sehemu za kukaa, kuwe na mpango ambao ni endelevu ambao hautaleta vurugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, kengele ya pili hiyo.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)