Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru sana na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kupata afya njema na kuwepo hapa. Vilevile, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa nafasi aliyoipata ya kuwa Makamu wa WTO Duniani, yeye sasa hibvi ni Makamu Mwenyekiti. Hii ni nafasi kubwa sana atakuwa amekaa kule akitutangazia utalii wetu wa Tanzania. Pia ninaamini kwa kazi na nafasi aliyoipata ni eneo sahihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia siyo hivyo tu, sasa hivi naona Tanzania inaanza kusisimkwa kwa ajili ya Royal Tour. Tumemuona mama ametangaza Royal Tour vizuri sana na kutokana na kuitangaza Royal Tour ndiyo maana sasa hivi tunaona mapato ya utalii wa ndani yameruka mpaka 161%, mapato ya Kimataifa imeruka kwa 276%, haya ni mafanikio makubwa sana. Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu Dkt. Abbas Mwenyezi Mungu awabariki sana. Kwa kweli Dkt. Abbas alifanya kazi kubwa sana akiwa katika Wizara ya Michezo. Mimi baada ya kuja hapa nikasema kweli nimepata jembe, maana yake natamani angerudi kule, lakini huku nako naona mambo yamezidi kuwa mazuri. Kwa mafanikio haya Mwenyezi Mungu awabariki sana na muendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Watendaji, Wakurugenzi Wakuu wa TANAPA, Ngorongoro, pamoja na matatizo makubwa tuliyokutana nayo ya Covid, lakini naona uchumi umekuwa sana kwa asilimia kubwa sana. Tuwapongeze kwa kazi kubwa wanayofanya na wanakutana na changamoto nyingi, lakini Mwenyezi Mungu hii Wizara ni Wizara ya kuitegemea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi ina mapungufu sana ya foreign currency (fedha za kigeni), lakini kwa kupitia watalii wa nje tunapata fedha za kutosha. Pia hii inaweza kusaidia yale mapengo tuliyokuwa nayo yakasababisha na sisi kuweza kutatua Wizara hii. Pia mimi nasema kazi inahitajika kuendelea. Kazi iendelee ili mapato makubwa katika hii wizara yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Rais ya kutangaza Royal Tour na mimi ninaamini tuna Royal Tour kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Katika dunia siyo watu wote ambao wanahitaji na walemavu wanatkiwa wawepo katika Utalii. Kwa vile katika Sheria ya 2024 ya Disability and Tourism ni lazima isimamiwe, inclusion. Sasa tunatamani sana na sisi tuwe na Royal Tour na tuaalike wenzetu walemavu duniani. Kuna maprofesa, kuna watu wameingia katika vita, lakini walikuwa na pesa za kutosha na bado ni haki yao ya kimsingi ya kupata utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona sasa hivi walemavu mpaka wanapanda Mlima Kilimanjaro, wanatembea na kuna mazingira mazuri ya mahoteli ambayo kwa kweli ni lazima tuseme ahsante kwa Wizara yako kwa kazi kubwa mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la migogoro; hii nchi kuna sheria, taratibu na kanuni. Tukisimama na sheria migogoro mnayoiona yote hii haitakuwepo, lakini kama hatusimamia na sheria, tukajichukulia sheria kama tunavyotaka sisi, basi kwa kweli migogoro hiyo haitakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tujifunze na tujiulize na kama kila mtu akijiuliza hivi ninachokifanya basi atajiona kabisa kuwa kuna mambo mengine tunafanya ni ya makusudi kusababisha migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naitwa Mama Riziki Said Lulida, Mama Tembo, Mama Mjusi, Mama Mazingira, lakini vilevile mimi ni Mama Selous. Selous National Park au Selous Game Reserve ilikuwa ni reserve ya nchi na ilikuwa ina wanyama wengi hasa tembo, lakini ninachokwambieni sasa hivi ningetamani ututoe Wabunge hapa utupeleke ukaone vurugu la ng’ombe liliko ndani ya Selous na Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unajiuliza yule ng’ombe ameingia Selous, yule tembo amabaye alikuwa amehifadhiwa kule Selous atakwenda wapi? Ni lazima atakwenda vijijini mwa watu. Ina maana mlimharibia njia yake ya kupita ndani ya Selous na siyo katika mashamba ya watu, wafugaji wako Selous. Wafugaji wametoka walikotoka mpaka wamefika Selous na sasa hivi wanataka kuvuka Mto Ruvuma kwenda Mozambique, sasa huu ni uvunjifu wa taratibu na sheria na ndiyo matokeo yake migogoro ambayo haifuati sheria itaendelea kuwa mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukimaliza Bunge namuomba Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri twende Tendeguru, lile ni eneo la hifadhi ambalo tayari walishapima wakinamama Jane Goodall, wafugaji wamepewa maeneo yao makubwa Mkoa wa Lindi na Pwani yote, wako Tendeguru na pale wanahakikisha wanamaliza msitu wa mipingo ambao ni indigenous species ambayo tunaitegemea duniani kwa sababu bado miti michache tu ya mipingo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunasema nini ikiwa baadhi ya taratibu na sheria zinavunjwa na zikivunjwa watu watalalamika lakini unalalamika kwa mazingira yale, kama leo Tendeguru wangeiachia eanyama wakafika pale kama asili ya corridor yao, wale tembo wasingehama kwenda vijijini, maana yake tembo anatoka Niasa – Mozambique anavuka Namtumbo – Mbalang’andu anakuja mpaka Kiyegeyi, yule mnyama anakuja mpaka Liwale, akifika pale anakuta tayari ng’ombe na binadamu wamekuja wanakaa pale. Tembo atafika hapo? Tembo anabadilisha njia, akibadilisha njia anakwenda kwa binadamu. Bado tuko na sheria, sheria haijasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwenda na Naibu Waziri wakati huo akasema wafugaji watatolewa, mpaka leo wako pale pale. Hivyo, msitegemee kumaliza migogoro kama hamuwezi kufuata sheria na taratibu. Nchi isiyokuwa na sheria na taratibu haiwezekani kumaliza migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hatuna shida ya ardhi, tembea kutoka Dodoma na ninaomba mchukue vichwa vyenu mviangalia. Dodoma msitu, Singida msitu, Tabora mpaka Igunda yote msitu, hao mnakwenda mpaka Shinyanga mpaka mnaingia Mwanza msitu. Bado watu hawajaweza kukaa kwenye maeneo yale, lakini wanakimbilia kwenye maeneo ambayo ni tengefu kwa vile ardhi ile haijatumika, ina mbolea ya kutosha na maji, lakini kama tungekuwa tumetengeneza maendeleo makubwa katika halmashauri zetu ya kuhakikisha maeneo ya wafugaji wetu yamesimamiwa, wasingehama. Leo wafugaji waliopewa ardhi kusini wote maeneo waliyopewa wamekimbia wamekwenda maeneo mengine, sasa hii migogoro mingine ni ya sisi wenyewe kutokusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwana mazingira, tukimaliza misitu yote Tanzania tunategemea nini? Tunategemea mvua? Je, kipindi cha ukame tutafanya nini na nchi yetu ambayo tunategemea iwe na maendeleo? Haiwezekani, sisi Wabunge tuwe vinara wa kusimamia mazingira, Tusiwe vinara wa kuchochea migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Balozi wa Utalii, tulipewa nafasi ya fulani ya kuzunguka na Wabunge, waliporudi hapa wote walinyamaza vichwa vyao. Walipofika ndani ya Selous pamejaa ng’ombe, ndani ya Serengeti National Park kuna simba, tembo na nyati, ndani kuna ng’ombe. Hivi jamani kwa nini mnavunja sheria? Kwa nini mnavunja taratibu kuifanya Wizara ionekane ngumu wakati tunategemea hii wizara ituletee mapato ya kutosha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapata mapato ya 17.2% ni fedha za kigeni, leo tunakwenda kwenye mabenki hakuna fedha za kigeni. Tunategemea hela za kigeni kutoka katika Wizara hii, hii Wizara ni ya kuisimamia, tuungane Wabunge, naomba kila mara mje mtufanyie semina ya kutuelewesha na baadhi ya Wabunge waende katika maeneo yao na kanda wakajionee haya mazingira ili watuletee majibu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Niasa Selous corridor, ile corridor nafikiri hata Wizara wenyewe walifanya makosa. Maeneo anayopita tembo katika corridor njia ni nyembamba, basi wamepewa vitalu wanawinda kipindi tembo anapita, unategemea nini? Fujo tu. Sasa matokeo yake, mazingira magumu ambayo yanatengenezwa inayaathiri nchi katika mazingira yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia maeneo matatu, TANAPA, Ngorongoro hawa watu ndio wanatuingizia pesa za kutosha. Katika mabadiliko ya tabianchi mwaka huu wameathirika vibaya sana kwenye haya maeneo na watalii wanahitaji kupita katika sehemu ambayo ni salama, security yao iwe imelindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali, niko chini ya miguu yenu, pelekeni hela Ngorongoro na TANAPA ili barabara zile zijengwe mara moja ili inapofikia kipindi cha msimu wa watalii kuja Tanzania wasikutane na mahandaki, makorongo na mabalaa ya barabarani. Maana yake wanahitaji kupita katika barabara ambayo iko salama na tunaamini nchi yetu iko salama. Mama ameiweka nchi iko peace kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lulida.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, niwashukuru sana Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)