Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza najua hii wizara ina Waziri mgeni, anatengeneza mifumo Wizara, lakini anakwenda vizuri. Nampongeza sana Mheshimiwa Kairuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri ndugu yangu Kitandula naye ameingia ni mgeni na anamsaidia kufanya kazi vizuri, lakini vilevile tuna Katibu Dkt. Abbas ambaye ni mzoefu anafanya kazi vizuri na watendaji wote na Makamishina wote wa TANAPA, TAWA, TFS wanafanya kazi vizuri. Tatizo lilikuwa kwenye hela na sasa kwa sababu tunawarudishia hela tunajua watafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo mawili katika Wizara hii, kwanza wapo watu wa philosophy wanaosema kwamba, katika utawala bora ufanye kuliko kutokufanya. Mheshimiwa Rais alipoanza kutembea porini watu walimuona kama anazurura tu, walisema kazi gani hiyo atafanya? Hata hivyo, leo kila mahali pameongezeka, watalii wameongezeka, fedha imeongezeka. Ni miaka mingi sana hatujawahi kufika watalii milioni moja na kitu, sasa imekwishafika. Kwa hiyo, amefanya kazi kubwa ile ambayo watu walikuwa ni kazi ya kawaida, lakini imetoa matokeo makubwa sana, nimpongeze kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Rais wetu ni msikivu sana, tumezungumza mara nyingi sana kwamba, hawa watu wa TANAPA, TFS na TAWA wana maeneo makubwa sana ya utawala asilimia 32 point. Kuna hifadhi 21, lakini hifadhi zinazotoa hela ni tano tu au tatu, zote tunalinda. Tuna mapori 29 na mengine tengefu karibu 23 na tuna misitu karibu mia nne na kitu, yote haya yanahitaji fedha za kuyalinda haya mapori, vinginevyo yatabaki matupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulinda haya mapori hatuhitaji yote yaje na faida, kwa sababu kuna mambo mengine yako kwenye environment type. Unaweza kuzungumza kwa maana ya mazingira lazima kuwepo miti na mambo mengine ambayo yanatunza nchi yetu, siyo lazima yalete faida, kwa hiyo, yote yanalindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekubali kuwapa zile fedha ambazo zilikuwa zimerudi kwa makusanyo yao na sasa zinakwenda kukaa na wao, maana yake ni yake ni kwamba watakuwa na uwezo mkubwa wa kulinda tembo na kuzuia ujangili kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hilo jambo ambalo amelifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie fidia ambayo ni kifuta jasho na kifuta machozi, sasa sijui tatizo liko wapi, kila mara Wizarani wanatuambia fedha za kulipa kifuta machozi, lakini kila mara wanakwenda kufanya tathmini kwenye maeneo yetu ya vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo yangu ya Hunyari, Kihumbu, Mariwanda, Sarakwa, Tingirima, Kyandege, Mugeta na maeneo mengine yote wanafanya tathmini, lakini malipo hayatoki. Sasa Mheshimiwa Waziri, tusemeje sasa, kama malipo hayatoki tunasemaje na mnasema pesa zipo?

Mheshimiwa Kitandula nimekuja kwako mara nyingi tu mnazungumza kesho watalipa, kesho watalipa na hawalipi. Sasa mtuambie kwenye bajeti hizo fedha za kuwalipa hawa watu waathirika wa tembo zipo au hazipo? Maana yake sasa kila siku tunakwenda kuwaambiaje wananchi? Tutawambia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe hilo na sasa mjue kwamba tembo siyo kwamba wanakwenda kwenye vijiji vilivyopakana na hifadhi, sasa hivi tembo wanatembea nchi nzima, kwenye maeneo yangu wako karibu vijiji vyote 30, wanakwenda Nyang’aranga, Manchimweru, Mahanga, Mikomariro, Salama, Nyangere, Nyabuzume, kila mahali wanakwenda na watu wanadai fedha hazipo. Mheshimiwa Waziri nikuombe, bahati nzuri wewe ni mtu wa mifumo, tusaidie kutengeneza mfumo ambapo mkulima mazao yake yakiharibika anakuwa na karatasi ambayo itaweza kufika kwako mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya makaratasi ya fomu za kuleta malipo. Iende sijui wapi, aitwe Afisa Kilimo naye apewe hela, iende wilayani watoe hela, wananchi wanatoa wapi, wanakata tamaa. Kwa hiyo, niombe tutengeneze hiyo mifumo ikae vizuri ili tuweze kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya kuzuia tembo, sasa mimi sijui tumeleta mabomu, hivi sasa najiuliza, juzi tulikuwa tunasema tuongeze hela za kununua mabomu. Hivi yanatumika na nani? Kwa hiyo, tuombe sasa haya mabomu kuna wale watu wanaitwa VGS tumieni, kila kijiji kwa mfano pale kwangu wako 15 kila kijiji, watumieni na muwape mafunzo na vifaa walinde tembo. Maana yake vinginevyo ninyi wenyewe hamuwezi hiyo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo anaweza kuja kwa siku mara tatu, hamuwezi kwenye hayo mambo, lakini kwenye kifuta machozi kulipa yale malipo ya fidia mnakuja saa 10.00 mnaondoka saa mbili, halafu mnaondoka na hela mnarudi nazo Wizarani, Hapana. Mna KDU pale kwenye maeneo yenu, zile fedha zinapokuja kama mtu hayupo, wananchi siyo wa kuwapigiwa kengele kama wanafunzi. Mtoe matangazo, mkilipa fedha yake kwa siku hiyo anaumwa, mgonjwa mpeleke pale KDU aifuate, kama ana uhalali wa kuipata, aipate karibu kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, malipo ya Nyatwari. Hapa wamezungumza Wabunge wengi, amezungumza dada yangu pale Esther nikamwangalia, sasa najiuliza hivi kweli, amezungumza Waziri wa Ardhi hapa, Mheshimiwa Jerry kwamba, Serikali na mtu yeyote anayetwaa eneo la wananchi kama hana fedha za kulipa asiende kutwaa eneo hilo. Sasa mmeahidi miezi tisa, imepita, sasa inaenda mwaka Nyatwari Tamau na Serengeti hawajalipwa na wananchi wameathirika sana, sasa tunafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ninachosema ni twendeni mkaiambie Serikali, washaurini kwenye upande wanaohusika kwamba, malipo ya Nyatwari Tamau na Serengeti yamegoma. Waambieni wananchi waishi, kwani shida iko wapi? Sasa haya mateso ni ya nini sasa? Yaani mnawapa watu mateso mpaka wanakata tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi huwa najiuliza hivi sasa tunafanyaje kwa mfano? Hivi hawa wananchi tunaendaje kuwaambia wapige kura? Wanapiga kura kwa namna gani? Wana mateso, hawalimi, hawajengi, hawafanyi chochote, wanafanyaje? Waambieni bwana malipo hayapo, fedha haipo, tutakuja kuwapa sijui 2040, waambieni wajenge waendelee kuishi, kama wanavyoishi kwa sababu, sasa malipo yameongezeka ina maana hatutakuwa na hiyo hali ya malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara na Serengeti. Sisi tuna matatizo, Mkoa wa Mara na Serengeti asilimia 80 ya Hifadhi ya Serengeti ambayo ndiyo hifadhi bora Tanzania na Africa ambayo ndiyo inatoa hela nyingi Tanzania iko Mkoa wa Mara.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere, hitimisha. Muda umeisha.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninakuomba Mheshimiwa Waziri ujue tuliomba kujengewa VETA ambayo itaitwa VETA ya Serengeti, ambayo hata wananchi wa huku wanaokuwa wanakufa kule ndani wanapopata matatizo haya wao wanajua kuna kitu tunakiona. Miaka karibu 60 sasa ile hifadhi iko kwetu na haina maana sana kwa Serengeti, hata ajira ya Watu wa Mara haipo kwenye mambo ya TANAPA, TAWA na TFS.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe sasa watu wa Mara wafikiriwe kwa sababu, asilimia 80 ya hifadhi ya Serengeti iko mara. Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)