Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii katika nchi yetu na hoja yangu ya kwanza kabisa itakuwa kwa heshima na taadhima kubwa kutoa pongezi na shukrani kwa uongozi wa Wizara hii nikianzia na Mheshimiwa Waziri mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Waziri anipelekee salamu zangu kwa Mheshimiwa Rais za kumshukuru sana. Sisi kama wana-Nyanda za Juu Kusini tuna kila sababu ya kumshukuru sana Rais. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kupanua wigo wa utalii kwenye nchi yetu kuja Kusini, kama Southern Circuit na hilo amelifanya kwa matendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikianzia katika Jimbo langu la Iringa, kwanza Mheshimiwa Rais kwa Awamu ya Sita, kupitia Wizara zake, ameweza kutujengea uwanja wa ndege mkubwa ambao umekamilika kwa asilimia 86 ambao unaleta watalii wengi, lakini pia, matendo mengine aliyotuonesha ni kuimarisha miundombinu ya barabara zinazoingia kwenye mbuga yetu kubwa ya Ruaha National Park. Barabara ya Iringa – Samora kama kilomita 103 ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami, Barabara ya Ruaha – MR – Itunundu – Pawaga na yenyewe tumetengewa kilomita 20, tuna uhakika 25 zitajengwa mwaka huu, lakini pia, Iringa By Pass, kwa ajili ya kuweka mji wetu kuwa wa kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu. Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi ulikuja wakati wa Maonesho ya Kusini pale, kile kituo ambacho tumekuwa tukilalamika. Tumeuliza humu maswali zaidi ya nane na hapa nachukua nafasi hii kumpongeza sana Naibu Waziri aliyekuwepo, dada yangu, Mheshimiwa Mary Masanja ambaye mimi huwa namuita kivutio cha utalii, yaani yeye mwenyewe ni kivutio cha utalii, kwa kazi kubwa aliyofanya tukiwa tukipambana, kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Leo Naibu Waziri, dada yangu, Mheshimiwa Mary kile kituo kimeanza kwa hiyo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi imesababisha sasa mimi kutoa hoja, kwa ajili ya kuwatetea tembo waliopo ndani ya nchi yetu. Kwa nini nawatetea tembo? Ninawatetea tembo na wanyamapori wengine, lakini ninawatetea tembo nikiwa nina sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, species ya tembo duniani, wanasema miaka ya milioni sitini iliyopita 37 mpaka 34 tembo, walikuwa wa aina karibu 175 mpaka tunapoongea leo tembo wamebakia species tatu tu. Specie mojawapo ipo Asia, specie nyingine iko Savannah na specie nyingine tuko nayo sisi Forest Africa ambao ni tembo tulionao huku Tanzania na East Africa in General, wakiwemo tembo kwenye mbuga zetu za Tanzania na tembo waliopo Mbuga ya Ruaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo wamekuwa wakipambana muda mwingi. Inasemekana, unajua Waheshimiwa Wabunge tukilia sana Mungu anaweza akasema sawa, nyie wote ni viumbe wangu, kama hawa wanawasumbua sana ngoja niwachukue wote kama alivyowachukua kwenye nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa hatueleweki kwa sababu, tembo, kama Wanyama, ni moja kati ya big five na ni moja kati ya wanyama wanaovutia watalii wengi kuja Africa baada ya kuwa zile species zimepotea huko kwao. Tembo ni mnyama kati ya wanyamapori wengine wanaotusaidia katika kupambana na umaskini wa nchi hii, kupambana na maradhi, kupambana na wale maadui watatu ambao tuna changamoto nao. Hawa wanapokuja kuwaona tembo wanalipa fedha za kigeni, tunaweza kununua dawa, tunaweza kujenga vituo vya afya, tunajenga shule na tunajenga miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo inanisababisha kuona kwamba, hawa wanyamapori sisi tunaweza tukaishi nao. Ndio maana hata Mungu alivyomuumba Adamu alimuweka kwenye bustani na wanyama. Tunachotakiwa sisi kutumia ni akili zetu, sisi ni binadamu, tumepewa utashi, wao hawajapewa utashi. Wakati mwingine unajiuliza, sisi kila wakati tunaenda Ruaha National Park tunakwenda kutalii, tunakutana na wanyamapori, tunakutana na simba na tembo, tunarudi tukiwa salama tume-enjoy, afya zetu za akili zimekaa sawa, lakini wao wakija kwetu tayari shughuli inakuwa ni nzito, sisi tunashindwa kutumia akili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachowaomba, kama Wizara, hebu fanyeni utafiti wa kina. Tembo wame-undergo evolution mbalimbali, inaonekana tembo wa zamani kwanza walikuwa wadogo tu, wana kilo kama tano tu, sasahivi tuna tembo wana kilo 4,000 wame-undergo evolution ya kukua size, kuongezeka zile trunk zao, wameongezeka skull ya kichwa, wameongezeka rims zao mpaka yamekuwa majitu yale ya kilo 6,000/7,000 kwa tembo tulionao sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isijekuwa tembo hawa nao wanabadili tabia baada ya sisi kwenda kuwatembelea sana manukato yetu yanawavuta na wao kuja huku kwetu. Mnachotakiwa ninyi ni mkasome, tembo wasijekuwa wana-undergo evolution wanatamani, kwani India jamani, tembo wao si wanapakia maharusi? Hamuoni kule India wanapakia maharusi? Inawezekana na wa kwetu wameshatokea species nyingine inayotaka kuishi karibu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoa ushauri kama huu wataalam wanatujibu tu, tukianza kuwaruhusu waje huku kwa watu watabadili tabia, watakuwa na tabia za watu, wanabadilika ndio. Kwa sababu, hata wale wa India walikuwa kwanza wa pori, lakini baadae wamekuja kuwa huku, kama wapo huku tujifunze, muwafundishe wananchi wanaokaa karibu na hao tembo, maeneo yanayosumbua zaidi, ili wawe marafiki na wale Wanyamapori kwa sababu, wanatusaidia kutuletea fedha za kigeni na ni katika species ambazo Mungu amezilinda amezilinda Africa na anatuamini kwamba, tutaendelea kuwalinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, sisi tulikuwa tunaongea siku moja nikawaambia hivi kama tembo wanakuja huku wanafuata matikiti, wanafuata mpunga, sisi ni binadamu na wale ni herbivores. Herbivores wanakula vegetation, wameamua kula mpunga, wanakula matikiti, ni vegetation. Kwa nini msiwapandie kwenye buffer zone hayo matikiti nao wakiwa wanatoka, kabla hawajaingia kwenye matikiti ya wananchi wakutane na matikiti yao kwenye buffer zone kule? Mnasema ooh, watabadili tabia, kule ndani kuna mibuyu gani saa hizi wanayopata maji ya kutosha? Wanakutana na climate change, wanakutana na kupungukiwa kwa makazi kutokana na wanadamu kuwasogelea. Tembo wanakutana na changamoto ya kuibiwa viungo vyao zikiwemo pembe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu kama hivi wale nao Mungu ametupa tu, kama tunaona tabu sana sawa, watu watafunga na kuomba tembo watapotea and then tutapata wapi hela za kigeni? Hata kama tuliambiwa tuwatawale, Mungu alimwambia Adamu awatunze maana yake ni kwamba, mwishoni tutaulizwa, uliwatunza vipi? Sasa inaonekana kama akili zetu sisi zinazidiwa na akili za tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tembo wanatuzidi akili sisi binadamu? Tumeshindwa ku-control kuishi na Wanyama? Mbona leo tuko na simba hapa? Kule kwenye maonesho hatuko na simba? Iringa, simba wamekuja wametutembelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba ninyi fanyeni utafiti. Tumekutana na kundi la simba walivyokuja pale, sijui wale wazee wamefanyaje kwa sababu, mhifadhi wa kwanza kuwa Ruaha National Park alikuwa ni Chief Mkwawa, ulikuwa hauruhusiwi kwenda kuwinda kwenye ile mbuga bila kibali cha Chief na alikuwa anakuelekeza wanyama wa kuwinda, hauwindi tu kila mnyama. Leo wamekuja simba, wazee wanaenda, muulize Mkuu wa Mkoa wa Iringa dada yangu Halima Dendegu yuko pale, wakamwambia usiwe na wasiwasi hawa tunajua jinsi ya kuishi nao hapa. Walichofanya wale ni kuwazuia wale simba wasile watu na wasile mbwa, lakini waliwaruhusu kula vitu vinginevingine, ng’ombe, mbuzi na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, simba wamekula ng’ombe, wamekula mbuzi, hawajala mtu hata huyu. Wana akili timamu, lakini ninyi kama binadamu mmekaa tu, utafiti wa kwenda kusoma utakuta watu wanasema tunaenda Dubai kwenda kusoma jinsi ya kuishi na tembo, sasa Dubai wana tembo? Unaenda Ulaya kujifunza jinsi ya kuishi na nyani, wanapata wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hao ndio ujanja-ujanja, wasomi wetu watusaidie, wafanye uchunguzi watuambie Watanzania kuishi na tembo unaishi naye hivi, sisi tuta-enjoy. Wakija wakakaa sehemu nyingine, mmeshajua wanapita, mnasema wanafuata kule walikofanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo wana akili sana. Sisi wengine tangu tuondoke kwa bibi zetu hatujawahi rudi, lakini wao kwa babu zao na bibi zao wanarudi. Wanaenda kutembea ndio wanakutana na majengo, sasa tujifunze kama wanapita zone hii tunawalindaje?
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja. Tembo walindwe kwa gharama yoyote.