Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo na mimi nichangie kidogo juu ya hoja ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumpongeza kiongozi namba moja wa utalii Tanzania Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia nampongeza dada yangu Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki, Mheshimiwa Naibu Waziri, kaka yangu Kitandula pia na Katibu Mkuu wa Wizara hii kaka yangu Dkt. Abbas, hongereni sana kwa kazi kubwa mnayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayofanyika Wizarani hapa ni kubwa sana. Nilikuwa napotia Data za BOT nikaona kwamba mwaka 2021 sekta hii ya utalii iliingiza dola billioni 1.3, 2022 iliingiza dola bilioni 2.3 lakini mwaka jana mpaka Disemba iliingiza zaidi ya dola bilioni 3.3, hii siyo kazi ya kubeza ni kazi kubwa sana. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa sababu tunahitaji fedha hizi kwa ajili ya kwenda kuleta maendeleo kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa namna ambavyo tunafanya kazi, tunaendelea kushirikiana na Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu tunaamini kwamba mtafanya makubwa zaidi kwa sababu huku Bungeni kumejaa mawazo mengi sana ya kuweza kusaidia Wizara hii. Hata hii namba 20 ambayo tunayo maana yake ripoti ya mwaka jana inasema tuko namba 20 kwa wanaofanya vizuri; naamini tunaweza tukafanya vizuri zaidi na kupata watalii wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la Kitalu cha Uwindaji cha Makere, Uvinza Open Area; hiki kitalu mara ya kwanza kilikuwa chini ya Halmashauri ya Kasulu DC, miaka ya nyuma kidogo. Baadaye Serikali ikakichukua kikawa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Maana yake sasa hivi hatusaini mikataba na wao tena kama wawekezaji ila Wizara ndiyo inayosaini mikataba kupitia TAWA na mwekezaji huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninavyoongea hapa kuna vilio vya hali ya juu sana; kuna kilio kikubwa sana kwenye Jimbo la Kasulu Vijijini. Vijiji ambavyo vinazunguka na ambavyo vinapakana na mipaka ya kitalu hiki wanapitia machungu makubwa ambayo sijawahi kuyashuhudia tangu niwe Mbunge. Machungu gani? Kwanza, kuna changamoto ya mipaka kutofahamika vizuri; hakuna clarity ya mipaka. Yaani mpaka wa vijiji na kitalu cha uwindaji haifahamiki vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo imesababisha wananchi kulima maeneo ambayo mwekezaji anadai kwamba ni eneo la kitalu. Jambo la kwanza hatujui kwamba wapo kwenye kitalu au hawapo kwenye kitalu, that is number one; lakini mbaya zaidi ni kwamba mwekezaji anafanya operation ambazo kimsingi zinatumia nguvu kubwa. Ukienda pale utatoa machozi; anachoma mazao na mali za wananchi bila kuwa na huruma yoyote. We know that amewekeza pesa, tunajua. Tunajua wamewekeza pesa pale lakini kama hakuna clarity mipaka hiyo nguvu ya kwenda kuchoma mazao na mali za wananchi anaipata wapi? Mheshimiwa Waziri, hili jambo huwezi kulikimbia dada yangu, linakuhusu kwa sababu Wizara yako ndiyo imesaini mkataba na yule mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko umuhimu na ulazima wa Wizara kuweka utaratibu wa kuweka clarity ya mipaka ili wananchi waweze kujua kwamba huu ndiyo mwisho wa mpaka wa mwekezaji; wasije kwenda kulima kule na hatimaye wakaenda kupambana na mwekezaji wakaingia kwenye hasara ambayo wanaendelea kuipata mpaka sasa hivi; lakini kwa sababu hakuna clarity ya mipaka Mheshimiwa Waziri nakuomba sana utakapokuja kuhitimisha hapa, kwa sababu huyu najua ndiye aliyewekeza na najua dhana ya kuheshimu wawekezaji ambao wamekuja kuwekeza kwenye nchi yetu kwenye sekta ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika dhana nzima ya ujirani mwema Wizara yako iweze ku-contact naye; iweze kuzungumza naye angalau awaruhusu wananchi ambao wamelima na wakapalilia mazao yao yakaiva, sasa hivi wanavuna wanaenda kuwachomea mazao. Wawaruhusu mazao yao wayatoe halafu baada ya hapo wekeni mipaka inayoeleweka ili wananchi tuweze kuwapa elimu ya kutosha kwamba msivuke mipaka ya kitalu kwenda kulima kwenye kitalu. Otherwise hakuna anayejua mipaka hasa iko namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kuhusu TFS na kama hili halitapata majibu ya kutosha kwa kweli nitashika shilingi. Nilizungumza kuhusu TFS, TFS kwa kweli mimi ninawapongeza sana chini ya Kamishna Silayo. Kama miaka mitatu iliyopita tulikubaliana na tukaweka utaratibu kwamba kwenye Hifadhi ya Msitu ya Pori la Kagera Nkanda yaani Makere Kusini, kulikuwa kuna changamoto kwa maana kwamba msitu kwanza umepoteza uhifadhi na wananchi wakienda kulima kule TFS wanawatandika viboko ikawa ni changamoto kwelikweli; tukakubaliana tuligeuza kuwa ni shamba la miti. Kazi imeanza, ekari 1,500 zimeshapandwa na kwa sababu shughuli za kibinadamu haziathiri kilimo cha miti waliwaruhusu wananchi kwa utaratibu maalumu waende kulima na mwaka jana tuligawiwa ekari 21,000, hongera sana TFS kwa hilo nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna changamoto kidogo, kuna baadhi ya vishoka kule vijijini ambao wanakuwa katikati pale, nimetumiwa taarifa kutoka kwa wananchi. Yale mashamba tulikubaliana kwamba wananchi wagawiwe bure lakini kuna vishoka ambao wanajipenyeza kwa ajili ya kuwakodishia wananchi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri au Mheshimiwa Silayo kwa sababu hili jambo tumekuwa tukilifanya wote uingilie kati katika jambo hili ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya kitalu ambacho mmekifanya na wananchi kama ambavyo tuliwatangazia maana yake baada ya kukubaliana nilienda kwa wananchi kuwatangazia mashamba ni bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unavyoenda kule unawaambiwa watoe shilingi elfu 20 tukupe ekari moja, siyo utaratibu tuliokubaliana na kwa sababu msimu wa kilimo umekaribia kuanza naomba sana chonde chonde tufunge safari twende tukawaambie wananchi vishoka tuwakatae mashamba ya TFS Makere Kusini tunayagawa bure kwa sababu haiathiri shughuli ya kilimo cha miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda ni mchache nilitaka kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)