Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kunipa fursa ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ambayo ni hotuba ya Maliasili na Utalii kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025. Nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wote kumpongeza Mheshimiwa Waziri, ndugu yetu Mheshimiwa Angellah Kairuki, Mheshimiwa Naibu Waziri Ndugu Dunstan Kitandula (Mbunge), Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya maliasili kwa kuandaa hotuba yenye mwelekeo wa kuleta tija katika sekta ya utalii nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee naomba pia niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake binafsi kwa kutangaza utalii Duniani kupitia Film yake ya Royal Tour lakini pia film hii ya hivi karibuni kwa jina la The Amazing Tanzania and really Tanzania is amazing kwa sababu ya baraka ambazo tumepewa na Mwenyezi Mungu kwa vivutio vyote hivi ambavyo tunavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu utaegemea katika maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 hadi 2025 Ibara ya 7(a) kwamba, pamoja na mambo mengine ni kubuni na kutekeleza mikakati ya kuongeza na kukuza wigo wa bidhaa na mazao ya utalii ili kufikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa tatu amezungumzia kuongezeka kwa watalii wa nje kutoka watalii 922,962 mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 kwa mwaka 2023. Pia, watalii wa ndani kutoka 788,993 kwa mwaka 2021 hadi watalii wa ndani milioni 1.9 mwaka 2023. Naipongeza sana Wizara kwa mikakati ambayo inaifanya kwa nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba utalii unaendelea kuingiza Pato la Taifa na kweli tumeona katika taarifa ya Wizara hakika hatua ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba nizungumzie kwanza kuhusiana na utalii wa ndani, kutokana na sensa tuko Watanzania zaidi ya milioni 60 au kama milioni 62 hivi lakini idadi ambao wameshafika labda katika maeneo mbalimbali ni kama milioni 1.8. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tunahitaji msukumo mkubwa sana kwa Wananchi wa Tanzania wa ndani ili kusudi waweze kuona vivutio na huu urithi ambao mwenyezi Mungu ametupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo ni kwamba watalii milioni tano ndiyo wanahitajika pengine itakapofika 2025 waweze kuwa wamefika. Bado napata mashaka, leo hii tuko 2024 mwakani Mungu akitujaalia tutafika 2025. Kwa hiyo, mimi naomba niendelee kuishauri Wizara ni vizuri kuendelea kutoa elimu na matangazo zaidi. Tunatambua kabisa kwamba Wizara imekuwa ikifanya mbinu mbalimbali kwa kutumia balozi, makundi mbalimbali na kadhalika, lakini naamini kabisa msukumo zaidi ukifika kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutaweza kufikisha zaidi ya watalii milioni tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurusa wa 100 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri amebainisha juhudi za Serikali kupitia Bodi ya Utalii kwamba wameanzisha ushirikiano mkubwa sana Duniani na kampuni Expedia Group ya Marekani. Inasemekana kwamba kampuni hii imefanikiwa sana katika masuala ya utalii, mimi nawapongeza sana lakini nilikuwa nina ushauri kwamba kuwe na mkakati wa muda mrefu wa kuongeza hotels na camps za utalii hasa kwenye hifadhi ambazo zinatembelewa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa naomba nishauri kwamba gharama za kuwekeza kwenye malazi ziwe rafiki ili wawekezaji wa ndani waweze kuvutiwa na waweze kuwekeza. Sambamba na hilo wenzangu wengi wamezungumzia kuhusu suala la miundombinu hasa barabara. Tumejua kabisa kwamba kipindi cha El-Nino kumetokea shida sana. Kwa hiyo, naomba nishauri kwamba kwenye hili suala la miundombinu liweze kuangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo natamani nilizungumzie ni kwamba naipongeza sana Wizara kwa kuendelea kupambana na hawa wanyama waharibifu ambao ni tembo. Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumzia kuhusu hili jambo lakini sisi pia katika mkoa wa Dodoma Wilaya ya Chamwino tuna kata kadhaa ambazo kwa kuzitaja ni Kata ya Manda, Chiboli, Chinugulu na Nghambaku, kata hizi nazo pia kuna shida sana ya hawa wanyamapori tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa tarehe 13 Mei Wizara ilikuwa imezindua suala zima la vilipuzi na kukabidhi haya mabomu 4,000 kwa Wizara. Basi naomba nishauri, kwa sababu katika hotuba hii ameandika kwamba halmashauri 20 za mwanzo ndizo zitakazofaidika na vilipuzi hivi. Mimi natamani kwamba katika yale maeneo ambayo pia bado kuna taarifa kwamba tembo bado wapo basi pia waendelee kuona ni jinsi gani na wao pia wanapata vilipuzi hivi ili kusudi waweze kukabiliana na hawa tembo, kwa kweli tembo wamekuwa ni shida sana, wamekuwa wanaharibu mazao na watu wanapoteza maisha yao. Kwa hiyo, na sisi tunaomba katika Wilaya ya Chamwino hili jambo liweze kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba sisi tunahifadhi zaidi ya 20. Naamini kwamba tukijipanga vizuri kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutaweza kufikia zaidi ya watalii milioni 10 kwa sababu nikitoa mfano, tuna Nchi za Afrika ambazo wenzetu nao wamefikia hatua kubwa. Mfano Egypt wameweza kufikia hatua ya kupata watalii milioni 14.9 kwa mwaka, Morocco milioni 14.5, Tunisia milioni 9 na South Africa milioni 7. Kwa sisi vivutio tulivyonavyo naamini kabisa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na najua kabisa kwa mipango ya Wizara na hii kazi ambayo Rais wetu amekuwa akiifanya mwisho wa siku tutaweza kupata watalii wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niunge mkono ushauri wa Kamati. Baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)