Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa kipekee namshukuru Mungu kwa sisi sote tuliopo hapa na wanaotusikiliza kuzungumzia mambo mazuri haya ya nchi yetu. Namshukuru Mungu kutupa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza nchi hii kwa amani na utulivu katika kipindi hiki Tanzania. Ni chaguo la Mungu na tuendelee kumtii na kusikiliza na kumpa support. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Rais kututeulia Waziri wetu wa Utalii binti yetu huyu ambaye sasa ndiye Waziri wa Utalii, Mheshimiwa Angellah Kairuki. Niseme kwamba ana uwezo na anapenda kujisomea ndiyo maana hii kazi siyo ngeni kwake na amepata Naibu Waziri Mheshimiwa Dunstan Kitandula ambaye pia ni mtu anayependa kujisomea sana, kwa hiyo, hakuna ugeni kwenye Wizara. Wameweza na wamechukua na Katibu Mkuu Abbas waendelee kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi ni mashahidi tumeoina wenyeviti wa taasisi zilizo ndani yao; tumeona ma-General wastaafu wawili wa nchi hii ni watu wakubwa sana. Tumemwona General Mabeyo na tumemuona General... limenitoka lakini yule mkubwa zaidi wa siku nyingi. (Makofi)
MWENYEKITI: General Waitara.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: General Waitara, tumemwona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wale watu ukiwapa Chombo chako nataka tujue sote kwamba kiko salama. Kuna mambo yaliyojitokeza hapa mengi, labda hela zinaliwa na labda hela zinatapanywa. Nataka niseme hivi tumeomba miundombinu iende kwenye maeneo ya mbuga za wanyama. Sasa tunapoenda kupeleka miundombinu hiyo nani apite huko? Hawa wanyama wanataka hiyo miundombinu? Tunataka watalii wengi na ndiyo maana Mungu akampa maono Mheshimiwa Rais akaja na Royal Tour. Watalii wameanza kuingia nchini, hawa watalii wanapenda amani na utulivu na safari salama. Hakuna mtalii atatoka nchini kwake aje kuvunjika kiuno hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuwezesha jambo hilo liende inabidi hii Wizara ipewe hela za kutosha. Rasmi kabisa naomba niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuwaunge mkono na tuwapatie hela iliyoombwa na Mheshimiwa Waziri shilingi bilioni 348,125,419,000 wakafanye kazi na wasilale. Kwanza, ni vijana wadogo hawa. Tuone matokeo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tuendeshe hili gari tukiangalia kwenye wind screen, mambo ya kuangalia side mirror huko nyuma ikawaje na ilikuwaje, ilishakuwa; sisi tusonge mbele. Waheshimiwa Wabunge nawaomba sana tuweze kuwapa support. Nakubaliana kabisa na hotuba aliyosoma Mwenyekiti wa Kamati hii, nakubali. Tutaendelea kuyafanyia kazi na yatarekebishika lakini kwa leo tunapoenda kuhitimisha tuwape hii hela wala haifiki hata nusu trilioni; ni hela kidogo tu wameomba na wazalishe. Mimi naamini hii Wizara ya Utalii Tanzania ingewekwa vizuri, wakapewa nafasi hao wanaofanya kwenye hizo taasisi nyingine za utalii wakapewa exposure wakaenda nje na wakaenda huko katika trade fair kama ilivyokuwa zamani, TTBS wakajitangaza, tungepata hawa watalii kabla hata mwaka huu kuisha lakini hatutaki kutoa hela, tunataka tu tuwafinye. Tutawaminya halafu tutapata nini? Ukitaka hela lazima uweke hela, halafu ndiyo utapata faida zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo kwa vile muda ni mchache naomba niende moja kwa moja kwa wanawake kufikiriwa katika hii sekta ya utalii. Wanawake wa Tanzania bado hatujapewa fursa na pale tulipopewa hata kama ni madereva hatujaweza kufikiriwa na kupewa support. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana research zimefanyika na wengi, wanawake siyo kama wanaume kuna nyakati ambapo watajifungua wapeni likizo zao inavyobidi. Pia, siyo hayo tu kuna kuonewa kule yaani kutofanyiwa kama inavyotakiwa. Naomba uwalinde wanawake waliopo katika sekta hii ya utalii ambao ni kama 54%; wapatiwe haki zao walindwe na pia wapatiwe nafasi ambazo ni za mishahara ambayo inakidhi matumizi yao na matumizi ya familia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii Sekta ya Utalii hata ukiangalia walivyokuwa wanatambulishwa waliopo juu hatukuona hapa wanawake wengi tumeona wanawake kama wawili ama watatu tu, nao sijui wamepatikana kwa bahati. Sasa kwenye level zote kwenye taasisi zako, Mheshimiwa Waziri, wewe ni gender ya (ke) sisemi kwamba ukawape ambao hawana uwezo, kwani walipoanza shule, wakaenda sekondari mpaka vyuo vikuu wakahitimu iweje walioweza ni wanaume tu? Ina maana miaka hiyo wanawake walikuwa hawawezi? Naomba uwafikirie sana hawa wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba sana Mheshimiwa Waziri uangalie ni jinsi gani sasa wanaoishi tambarare ya Mlima Kilimanjaro ambao pia ni kivutio na ni maajabu ya dunia, ile theluji inaondoka kwa sababu ya tabianchi lakini tunaweza kurekebisha uoto wa asili kwa kurejesha tena kuotesha miti na mengineyo. Watu hawa wanaanzia toka kule Siha wanakuja Hai, Moshi Vijijini ambako na Vunjo ipo lakini mpaka Rombo, kumekuwa kukame. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utatoa mradi ambao tumeona huyu Prof. Dos Santos Silayo, anagawa miche kwa ukarimu kabisa, nimuombe tena aendelee kugawa katika shule zote, aendelee kugawa hata kwenye kaya za watu, waoteshe tu, ukishaotesha mti ukaumwagia maji au ukatafuta chochote, yaani kadri ya uoto utakavyoendelea lazima ule mlima utarejea katika hali yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri ikimpendeza, atoe pilot project ya wanawake hawa kuweza kuwa na vitu vya asili. Tumeona asali inatengenezwa na inaweza kuwekwa katika kufuga nyuki. Hata kuku pia wale wazungu wakija wasile tena yale mayai waliyozoea yale makapi makapi yale, wale mayai ambayo ni organic kama wanavyokula mboga organic hapa wanafurahi. Ndizi organic, ndizi haiwekwi hata siku moja fertilizer yoyote ambayo ni ya nje, hivyo ndiyo vivutio vyenyewe. Wanatoka kule walishavizoea, tuwape vitu vyetu vya jadi, waweze kufurahia hata kukaa kwao hapa. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia 100, nawatakia kila la heri, ahsante. (Makofi)