Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Ninapenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mungu kwa afya na uzima wetu. Pia ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ile Royal Tour na nitasema kwa nini pongezi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu pamoja na pongezi nitazungumzia suala la misitu na umuhimu wa kuzingatia local content katika misitu. Nitazungumzia pia suala la bomu baridi hilo la kufukuza tembo, nitazungumzia utalii wa matukio na mwisho kama nafasi itatosha nitazungumzia sekta ya wanyamapori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa ile Royal Tour na kwa bajeti hii pamoja na maandalizi yake napenda kupongeza Waziri Mheshimiwa Kairuki, kaka yangu Bwana Dunstan Kitandula, huyu ni mtu rahimu na mpole sana, lakini pia Katibu Mkuu Dkt. Abbas na Naibu Katibu Mkuu Kamishna Wakulyamba pamoja na watumishi, wafanyakazi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza kwanza kwenye sekta ya misitu. Kwa bahati nzuri na wewe unatoka kwenye misitu na unafahamu kwa namna gani sekta ya misitu ina mchango mkubwa katika uchumi wa watu wa Iringa na Mkoa wa Njombe mpaka maeneo ya Madaba. Sisi Mafinga tumejaliwa kuwa na msitu mkubwa ambao unakwenda katika Wilaya ya Mufindi mpaka maeneo ya Kilombero huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa na jambo moja kwa Mheshimiwa Waziri, timu yake na wenzetu wa TFS, tunapozungumzia local content wakati mwingine nadhani kwamba ile local content ni mambo tu ya Kimataifa na mambo ya kwetu hapa Kitaifa. Kumbe local content maana yake ni kwmaba hata wale wenyeji walioko kwenye yale maeneo kama ni ya utalii au ni ya misitu wawe beneficiary wa uwepo wa ile neema ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia watu wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwangu hapa nasema nini, nimwombe Mheshimiwa Waziri na watu wa TFS wanapotoa ajira za muda mfupi, zile temporary, hakikisheni pia wanazingatia wenyeji wanaozunguka msitu wa Sao Hili. Wananchi wanaotoka kwenye vijiji vile nao wawe sehemu wa kupata vile vibarua. Wakati fulani tulikuwa tunatoa vibarua ikiwa inaeleweka kabisa kwamba msimu huu kijiji hiki kitapata vibarua labda watoto kumi au vijana kumi au akina mama kumi. Kwa hiyo, ninawaomba kuwepo na clear information ili wananchi wa Mufindi na Mafinga waweze kunufaika kama ambavyo wanasema siku zote kwamba ukiwa karibu na uaridi lazima unukie uaridi. Kwa hiyo, sisi watu wa Mafinga na Mufindi kunukia kwetu uaridi la kwanza na sisi kuwa sehemu ya washiriki katika ajira za muda mfupi zinazotokea kwenye mashamba ya Sao Hill. Ninaomba hili tulizingatie sana kwa muktadha ule niliosema wa local content.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili tuliwaomba Mheshimiwa Waziri na hii mimi tumewaomba Mkoa wa Iringa kwa nia njema. Tumewaomba kwamba jamani pale kwenye shamba la Sao Hill tutengeeni sehemu tujenge soko kubwa la mazao ya misitu la kimataifa, this is good for both of us. Nimewaambia, nimeongea na Mheshimiwa Waziri personal, nimeongea na Katibu Mkuu na pia nimeongea na Profesa Dos Santos. Sasa nikasema je, kweli jambo hili nina haja au sisi watu wa Mufindi tuna haja ya kumwandikia Waziri Mkuu kumuomba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kitu ambacho tumewaomba Mheshimiwa Waziri ni kwa manufaa yetu sisi sote, Wana-Mafinga, Wana-Mufindi, Wana-Iringa, Wana-Njombe, lakini pia wao ili tuikuze sekta. Tutakapokuwa na soko kubwa la mazao ya misitu tutakuwa pia tumeikuza hii sekta yetu. Tulisema, Profesa anajua, tumezungumza sana kuhusu percentage recovery kwenye mti, kwamba ule mti unakuta kwa jinsi ilivyo sasa hivi labda ni 40% tu ule mti ndio unatumika, 60% ni waste.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwa na eneo la namna hiyo maana yake ni kwamba katika mti tunaweza tukafanya ile recovery percentage ikawa hata 90%, kwamba huyu hapa atafanya mambo ambayo huyu hapa kama ana mambo ya sawdust atafanya. Kwa hiyo niwaombe, pamoja na kuwa Mheshimiwa Waziri alisema watalamu wamemweleza tofauti, mimi nawaombe, ninawaombeni kwa niaba ya wananchi wa Mafinga na Mufindi hebu mkalitafakari upya jambo hili, ni kwa manufaa ya sisi na sekta ya misitu, hili nimewasilisha kama ombi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu katika misitu, tuliwaomba na mwaka jana nilisema pia kwamba makusanyo yale ya cess, zamani ilikuwa kwamba yule mtu anayepata kibali cha kuvuna analipa malipo yote kwa mkupuo mmoja, halafu baadaye mnatenganisha ile ambayo ni cess wanatupatia sisi halmashauri. Wakaja na utaratibu kwamba tujikusanyie wenyewe. Ile pale kama nilivyosema, kama tuko karibu na uaridi na tunukie uaridi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba utaratibu ule tuufikirie upya. Mtu anapokwenda kulipia na sisi kama Serikali tumesema tunataka twende na utaratibu wa one point katika masuala ya malipo. Sasa kwa nini mtu asilipe, halafu baadaye mtugawie ile ambayo ni sehemu yetu ya cess. Watu wa TFS wanasema sijui kuna gharama za bank charges na kadhalika. Sisi tuko tayari ku-share hizo costs, lakini ilivyo sasa sisi kama tunategemea cess maana yake makusanyo sasa yanaendelea kushuka. Nawaomba wakae na local government, kwa maana ya TAMISEMI, tuone na tuje na huo mfumo ambao utatuwezesha sisi kukusanya cess pasipo kutumia mabavu wala nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo ninataka niliseme na nipongeze ni suala la bomu baridi kwa ajili ya kufukuza hao tembo na hapa ni lazima kama Serikali na kama Wabunge tuzipongeze Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa ushirikiano na kitaasisi ambao umewezesha kuja na hili bomu baridi ambalo litasaidia sana maeneo ambayo wenzetu wanapata matatizo ya tembo kuingia kwenye makazi ya wananchi.
Kwa hiyo, napongeza vyombo, na nawapongeza nimeona wamekwishatoa order, wamenunua, na watu wengine tuunge mkono jitihada, vyombo vinapokuja na ugunduzi fulani fulani basi sisi kama Taifa, wale watu wa Mzinga wana mazao mbalimbali tuwaunge mkono, tununue mazao yale kwa ajili ya manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kuhusu Royal Tour kwamba utalii wetu uendane na kitu kinaitwa utalii wa matukio. Mtu akija kupanda Mlima Kilimanjaro, akija Serengeti, akija Ruaha mwakani aweze kupata hamu ya kuja ten ana ili aweze kupata hamu ya kuja tena maana yake ni kwamba tuwe na matukio ambayo yanasindikiza hivi vituo vyetu. Kwa mfano kuna maeneo wenzetu kama Brazil wana kitu kinaitwa Rio Festival. Hizi festival hata hapa Tanzania wenzetu Sauti za Busara Zanzibar watu wanakuja kwa ajili ya utalii, lakini pia anakuja kwa ajili ya lile tukio. Kwa hiyo, tupanue wigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninaamini ndugu yangu Mafuru ni brain, atakuja kupitia TTB tukawa na utalii wa matukio. Leo hii tulikuwa na wageni hapa wa waratibu wa The Great Ruaha Marathon. Wamebuni kitu kizuri kwamba unakimbia Marathon ndani ya Mbuga za Ruaha. Kwa hiyo, tubuni, tuwe na matukio mbalimbali ambayo yataongoza vile vivutio vya utalii. Kuna kitu kinaitwa Nyama Choma Festival, yule mtu kama alikuja mwaka jana apate hamu tena ya kuja mwakani kwa ajili ya lile jambo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele imelia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huo utalii wa matukio kuna huu utalii wa michezo. Nilitoa mfano ile Simba ilivyoshiriki African League, yale ndiyo matukio ambayo pia yanaleta utalii. Tunavyokuja kufanya AFCON tunaleta utalii. Kwa hiyo, tupanue wigo pamoja na hii traditional utalii lakini tuongozane na utalii wa matukio…
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nawapongeza tena Mzinga kwa kuja na bomu la baridi kwa ajili ya tembo na Wizara kwa kushirikiana na Mzinga kwenye jambo hilo muhimu Mungu atubariki sote. (Makofi)