Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kwa mikakati yake mikubwa ya kukuza utalii nchini. Sisi tunaokaa huko maeneo ambayo watalii wanakuja, tumeona matokeo makubwa sana na kipekee sana Serengeti tunazo shukurani kubwa kwa sababu ujio wa watalii wengi umebadilisha hali ya uchumi wa maeneo yetu, kwa hiyo, tunamshukuru sana sana Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana nimshukuru Waziri wa Wizara hii, Dada yetu Angellah Kairuki pamoja na Naibu wake Waziri wanaendelea kufanya kazi na nzuri. Mara nyingi kiongozi mzuri utamwona wakati wa changamoto. Tunakumbuka wakati ule kulipokuwa na hali ya mvua ikinyesha kwa wingi sana maeneo mengi ya Hifadhi ya Serengeti yalikuwa hayapitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naona waliweka jitihada kubwa sana na ndani ya muda mfupi barabara zilianza kupitika. Kwa hiyo, tunawashuru na kuwapongeza pamoja na menejimenti nzima ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake ikiwepo TANAPA, wanafanyakazi nzuri, tunawashukuru. Tunawaomba waendelee kuongeza kasi kubwa na uboreshaji uwe ni jambo lao na malengo yao ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja na kununua mabomu ambayo yametengenezwa hivi karibuni kwa ajili ya kupambana na tembo. Jambo hili ni jema, lakini mimi nashauri kwamba imefikia wakati sasa jambo hili tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili kila wakati tembo wanapongia vijijini wanalaumiwa wao, lakini ni kwa nini? Tembo hao wakishaingia vijijini hawaangaliwi kwa maana ya kurudishwa, hawasimamiwi na watu wa TANAPA, wanaoshuhulika nao ni maafisa wanyamapori wa wilaya ambao wako chini ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila taasisi kwa maana ya Wizara, inapoanzishwa inakuwa na core functions zake. Sasa ukiangalia madhumuni ya Wizara, kazi yake mahususi Wizara ya Maliasili ni kuendeleza utalii na kuhifadhi wanyama wetu, lakini TAMISEMI wao kazi yao kubwa ni kutoa huduma kwa wananchi, kama vile barabara, elimu, maji na kadhalika. Sasa wao si rahisi sana waka-allocate resources katika kupambana na wanyama hao warudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kule Serengeti kila wakati wanyama wanapoingia kwenye vijiji ukimpigia DGO mafuta hana, imeenda imerudi, huku wanyama wanashambulia mashamba na kadhalika. Sasa kazi hii, ninakumbuka katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri pale Morogoro tukipokea mabomu baridi alisema halmashauri zinunue mabomu haya. Sasa nikiangalia zilitajwa pesa nyingi sana ambazo zinanunua mabomu. Kama wanashindwa kutoa mafuta lita 30 wanawezaje kununua mabomu? Kwa hiyo, jambo hili si rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe Wizara irudi, ichukue kazi hii ya kudhibiti wanyamapori iwe ni kazi yake. Watu wa TAMISEMI waachwe washughulike na mambo mengine haya ya kuhudumia watu, vinginevyo basi huyu District Game Officer (DGO) basi arudi kwa watu wa Wizara ya Maliasili na wawezeshwe fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanyama hawa wanapoingia katika maeneo ya wananchi waweze kudhibitiwa haraka na nguvu kubwa iwekwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Serengeti tumepata madhara makubwa sana kwa hawa tembo pamoja na wanyama waharibifu. Tuombe sana Wizara sasa ichukue hatua za kudhibiti. Sawa kuna wakati mwingine tunauliza juu ya kifuta jasho, kifuta machozi na kadhalika, lakini hivi havisadii. Sisi tunahitaji wananchi wetu wabaki salama, tunahitaji mazao yetu yabaki salama, tuvune na kuendelea na shughuli zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo la pili ambalo ningependa kuishauri Wizara hii, tunahitaji kuona utalii unakua nchini na watalii wanaongezeka. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi katika utalii, lakini ukirudi na ukiangalia miundombinu katika kufikia hifadhi zetu bado ni changamoto kubwa na wakati mwingine gharama inakuwa kubwa. Leo gharama ya kuifikia Hifadhi ya Serengeti ni kubwa sana. Utoke KIA uende Arusha utoke Arusha mpaka Ngorongoro, Ngorongoro mpaka Serengeti ulipe geti ya Ngorongoro, uende Serengeti gharama inakuwa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe ule Uwanja wa Serengeti ujengwe. Uwanja huu umekuwa ni wa miaka mingi ambapo tumekuwa tunazungumza utajengwa, utajengwa. Wakati mwingine wanapatikana mpaka wafadhili, wanapatikana watu wa kuwekeza kutoka private sector, lakini bado tunachelewa kufanya maamuzi. Niombe sana Wizara ya Maliasili na Utalii ichukue hii ajenda hii na ishughulike nayo kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba bado barabara zinazoingia Serengeti ni changamoto, kwa maana ya barabara ya lami, kutokea kule Tarime pamoja na ile ya Sanzate – Nata, tunaomba Wizara iangalie barabara hizi ni za kimkakati kwa ajili ya kukuza utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni kuhusu WMA, hizi Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori ambazo zinamilikiwa na vijiji leo wameanza kukata tamaa na wengine wanatamani sasa zingerudi maeneo yao yale wafanya shughuli zingine kwa sababu pesa zao zimekataliwa huko Hazina. Tunaomba sana Wizara msaidie, tuko pale Serengeti na Ikona WMA, tunaomba pesa zao zije, zimesaidia kiasi kikubwa sana maisha ya wananchi kukuza utalii, I mean conservation iliweza kuwa improved sana kwa sababu ya fedha ile pamoja na kujenga miundombinu mbalimbali katika afya na elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe pia liko jambo lingine tunaiomba sana TANAPA iangalie vizuri, pamoja na Wizara hii kwa ujumla. Tunapotoa vibali vya ujenzi wa camps pamoja na lodges ndani ya hizi hifadhi zetu, naona kama ubora wa ujenzi wake si mzuri. Ninashauri Wizara iangalie sasa uwezokano wa kusomesha watu maalumu ambao watasimamia viwango vya ubora wa ujenzi wa hizi camps. Mtalii anakuja anaoneshwa picha imetengezwa kwa namna fulani anaona kwamba it is beautiful ni sehemu nzuri, lakini akifika malazi yale yanakuwa siyo mazuri mno. Sasa sisi tunampa tu mtu eneo jenga camp, jenga lodge, lakini ni la viwango gani vya ubora wake? Bado hatujawa na watu wa kusimamia viwango vya ujenzi wa hizi camps pamoja na lodges. Kwa hiyo matokeo yake mtalii anakuja analala sehemu ambayo ni sub-standard kwa hiyo tunaomba sana Wizara iende kuwekeza katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana maeneo ambayo yanapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti vijiji vile hasa upande wa Western Serengeti ambapo hakuna buffer zone tunaomba tujengewe malambo ya kutosha kwa ajili ya mifugo yetu. Tunaishukuru sana Wizara, mpaka sasa hivi yako ambayo yanajengwa lakini tunaomba yaongezeke kwa wingi zaidi ili ng’ombe wale wasiweze kupata shida ambayo wanapata sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna malambo na hata wakati Wizara ikiwasilisha, kwa maana ya Kamati, imesema lazima hivi vijiji pamoja na jamii zinazozunguka hifadhi tuweze kuziangalia, kwa maana ya kuzisaidia. Wame-sacrifice land na kwamba wanapata shida nyingi kwa kuishi pamoja na wanyama, kwa maana ya kupakana. Tuhakikishe kwamba watu hao wanajengewa malambo pamoja na huduma zingine za kijamii ili nao waweze kufaidika moja kwa moja na hifadhi hizi ambazo wanaishi pembeni nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niombe sana sasa Wizara hii kwa kushirikiana na TANAPA, waangalie namna bora ya kuongeza ajira kwa watu ambao wanapakana na hifadhi zetu hasa kwa upande ule wa Serengeti, wananchi wetu pamoja na kuwa na elimu nzuri bado ajira nyingi hazijapatikana kwa vijana wetu hata zile ambazo ni seasonal.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Hitimisha.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)