Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitaomba na mimi nichangie kwenye maeneo matatu ambayo ni kwenye upande wa service levy, upande wa madeni ya wazabuni mbalimbali nchini Tanzania na kwenye upande wa dollarization. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye service levy, wafanyabiashara wa sekta ya utalii wamekuwa na changamoto ya usumbufu wa muda mrefu sana kutoka kwenye Halmashauri zetu. Kwanza ni namna ambavyo wanadaiwa zile kodi ni utaratibu ambao haukubaliki. Kuna mfanyabiashara yuko Arusha Mjini anatakiwa alipe service levy Halmashauri ya Arusha, anadaiwa Halmashauri za Monduli, Karatu, Ngorongoro na maeneo mengine ambayo anafanya biashara za utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado pia hata sheria yenyewe inataka mtu alipe service levy kutokana na turnover lakini nature ya biashara ya utalii haifanani na biashara nyingine na nitatoa mfano. Kwa mfano, mimi ni tour operator, nikimuuzia mgeni nje bidhaa ya utalii Tanzania nauza package. Namuuzia accommodation lakini sina hoteli, naweza kumuuzia transportation, pengine sina magari, na bidhaa nyingine kama park fees ambazo ziko Ngorongoro na Serengeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye mtalii akishafika Tanzania, mimi wajibu sasa nachukua kile alichonilipa kwenye account yangu, kama alilipa park fees, mimi nailipa Ngorongoro na Serengeti. Kama alilipa accommodation, labda namlipa Serena au hoteli nyingine. Kama alikuwa anataka kwenda Zanzibar, nimemuwekea kwenye package yangu, mimi nalipia pia na malipo yake ya kule Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho wa siku tukija kulipa service levy, nikilipa Ngorongoro watalipa service levy, nikilipa Serengeti, watalipa service levy, nikimlipa mtu wa accommodation, atalipa service levy na mimi pia ambaye nimetumika kama conduit pipe ya kupokea zile fedha natakiwa pia nilipe service levy kutokana na turn-over. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu hapa Waziri wa Fedha atusaidie kuwasiliana na wenzetu wa TAMISEMI ili kuhakikisha kwamba mtu anapolipa service levy basi…

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuongezee kidogo, mchanganyo uliopo kwenye hiyo sheria ya service levy unawakumba pia wawekezaji wengine wenye hali kama hiyo ya utalii ambao wanawekeza kwenye huduma za jamii kama shule, nao wanatakiwa kulipa kwenye package ya ada ambapo kuna chakula ndani yake, kuna malazi na kila kitu. Sasa, unakuta wanakuja kuchajiwa hela kubwa kuliko kile kitu wanachochaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimuongezee taarifa hiyo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gambo.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake ni nzuri lakini naomba isichukue muda wangu wa kuchangia.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gambo, taarifa ni sehemu ya Kanuni.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali lakini ndiyo maana nikasema isichukue muda wangu wa kuchangia.

NAIBU SPIKA: Endelea bwana.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Wizara ya Fedha na TAMISEMI wakae, waweke utaratibu mzuri zaidi wa kuweza kusimamia chanzo hiki, kwa sababu Halmashauri hizi zinapewa makadirio ya kukusanya fedha, kwa hiyo wanatumia pia hii ni kama fursa ya kwenda kukusanya kila mahali na mwisho wa siku wanai-disturb sekta ya utalii ambayo ni sekta nyeti sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ni kuhusu madeni. Unajua hii nchi wageni wana thamani zaidi kuliko Watanzania. Leo angalia mikataba yote ya wakandarasi wa nje, mkandarasi wa nje akipewa mkataba lazima kunakuwa kuna clause pale inasema kwamba Serikali ikichelewa kumlipa italipa pia na riba. Wengine wanakwenda mpaka kusema kabisa pengine watalipa riba asilimia 3 juu ya riba ambayo inawekwa na wenzetu wa Benki Kuu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa huyu mfanyabiashara wa Tanzania ambaye anayefanya kazi kwenye taasisi zetu, kwenye Halmashauri, yeye mbona hawekewi riba? Mwisho wa siku huyu mtu unakuta amekwenda kukopa fedha benki, benki wamemuwekea riba, kadri Serikali inavyochelewa kumlipa anapata hasara na mwisho wa siku unakuta vitu vyao vinapigwa mnada na wanapata hasara kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba kwanza, Waziri wa Fedha kwenye bajeti yake hii atauambie mpaka sasa hivi kuna madeni kiasi gani ya wazabuni wa ndani katika nchi yetu ya Tanzania? Pia, atuambie je, bajeti hii tunayoipitisha Halmashauri zetu na taasisi za Serikali zimeyatambua madeni hayo na wametenga fedha za kwenda kuwalipa? Maana bila ya kufanya hivyo, uwezekano wa kuwalipa utakuwa mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi tunaomba pia tuweke utaratibu hapa kwamba Mtanzania au mtu yeyote anayefanya kazi za ndani tuweke pia na riba ili Serikali ikichelewa kulipa iweke ni madeni ya kipaumbele kama ambavyo wanafanya kwa wenzetu wanaotoka nchi za nje. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika hili tutaangallia hata uwezekano, kabla ya kukubali bajeti yako ipite Bajeti Kuu ya Serikali, tutaomba tupate ufafanuzi wa kutosha kwenye kipengele hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni kwenye mambo ya dollarization. Unajua hii nchi yetu hii, tukiona watu wameongea jambo, tunaamka tunatoa matamko bila kuangalia na ukubwa wa changamoto ya matamko yetu na sekta zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano kwenye changamoto ya upatikanaji wa dola, hapa nitakupa mfano halisi, leo wenzetu wa Benki Kuu wanasema wana-control price. Ukiwauliza leo watakwambia kwamba dola ukitaka kubadilisha ni shilingi 2,680 lakini namuuliza huyu mtu wa Benki Kuu, je, nikienda leo benki nikitaka nibadilishe shilingi nipate dola kwa rate hiyo mnayonipa itapatikana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, benki nyingi ukienda leo wanakwambia kwa siku unaweza ukapata dola 500, sasa dola 500 unafanyia nini? Mimi juzi hapa, nakupa mfano hai, nilikuwa na shida ya dola 300,000, nilitumia mwezi mmoja kuweza kupata dola 300,000 ili niweze kununua kitu ambacho nilitaka kununua nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unajiuliza, leo mnasema mna-control price. Mkisha-control, mtu akienda kule nje akikosa, je uwezo wa benki zetu wa kutoa upo? Na kama haupo, Serikali inakuwa ni sababu ya black market katika nchi hii. Leo mnasema dola ni shilingi 2,680 hazipatikani, mtu akikwambia nje inapatikana dola kwa shilingi 3,000 itabidi ununue kwa sababu kule nje huwezi kuuziwa kitu kwa kutumia fedha yetu ya Kitanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi nadhani kwa sababu, wenzetu wa IMF kwenye ripoti yao ya hivi karibuni wameweza kukosoa utaratibu wa Benki Kuu au wa Tanzania kwa ku-control exchange rate ya dola yetu kwa sababu, haiko realistic kule kwenye market na ni kitu ambacho kinaleta changamoto kubwa sana. Kwa hiyo ni vizuri mkaangalia umuhimu wa free market, mkaangalia uwezekano wa kuruhusu watu wapate dola kwa utaratibu wa ushindani wa soko kama walivyofanya wenzetu wa Kenya.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili. Ushauri wangu ni nini kwenye jambo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye Ukurasa wa 35, ametuambia kwamba, hadi Machi 2024, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani bilioni 5.3. Kiasi ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa na kununua kutoka nje kwa miezi 4.4 ambacho kiko juu ya lengo la nchi la muda usiopungua miezi minne.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama lengo la nchi ni muda usiopungua miezi minne, kwa nini hii 0.4 ambayo imepungua kwa sababu, pale ni lower demand and supply, kwa nini msiichuke mkaiingiza kwenye benki zetu? Ili Watanzania wakitaka kununua bidhaa nje, wakienda kwenye benki, wakute dola zinapatikana kwa sababu, wenzetu wa Kenya wamefaya hivyo na sasa hivi changamoto hii kwa kiwango kikubwa imeondoka kwenye nchi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu ni, mnapoenda kwenye Sekta ya Utalii, ni sekta ambayo ni very sensitive. Leo ukisema kila kitu kifanywe kwa shilingi, sawa nakubali ni hatua sahihi kabisa, lakini mimi ninayefanya biashara ya utalii napokea dola kutoka nchi za nje. Kama Ngorongoro, Taasisi ya Serikali, wanataka nilipe park fees kwa dola, hiyo njia itasaidia sana kupunguza black market. Mimi nitapokea dola kutoka nje, nitalipa park fees kwa dola kwenye Taasisi ya Serikali, Serikali itabakiwa na zile dola.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkiruhusu kulipa kwa shilingi, nitapokea kwa dola, nikienda kuangalia Benki Kuu shilingi 2,680 huku nje shilingi 3,000 mtakuwa mnachochea black market. Maana yake ni nitachukua zile dola zangu, nitakwenda kununua nje ya mfumo, halafu mwisho wa siku nitakwenda kulipa kwa shilingi na zile dola zenyewe hamtaziona kwa sababu, zitakuwa mikononi mwa watu, lakini zikienda kwenye Taasisi ya Serikali inakuwa ni rahisi zaidi kuziona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani hili suala la dollarization, Serikali inatakiwa itulie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ishirikishe sekta zote, isichukue maamuzi ya haraka na maamuzi ya jumla. Nashukuru sana.