Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia pia, katika hoja hii na namshukuru Mungu kwa uzima na afya zetu. Mimi nitakuwa na mambo kadhaa, lakini kwanza naanza na pongezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia, kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo yanafanyika katika Jimbo la Mafinga Mjini. Kwanza sisi, kama watu ambao tunajishukughulisha na kilimo, tunapongeza sana suala la mbolea. Tulishauri hapa Bungeni, kweli Serikali ikaleta ruzuku ya mbolea na baadae kulikuwa na changamoto za hapa na pale, tumeendelea kushauri na maboresho yameendelea kufanyika. Kwa hiyo hili ni jambo linalostahili pongezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, naishukuru na kuipongeza Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kijamii. Tuna kituo cha afya pale Ifingo, tunashukuru sana kimekamilika na tumepata gari la kubebea wagonjwa (ambulance), tunachosubiri kutoka kwa wenzetu wa TAMISEMI ni gari, kwa ajili ya ufuatiliaji kwa wenzetu wa Idara ya Afya. kituo hiki pamoja na kusaidia watu wa Kinyanambo, lakini pia, kinasaidia watu kutoka hadi Ihalimba, watu wa Kata ya Rungemba na watu wa kutoka Jimbo jirani la Kalenga wanakuja pale kupata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika elimu, tumesogeza elimu kwa kujenga Shule ya Sekondari pale Ndolezi na sasa tunaendelea kwa kushirikiana na wananchi kujenga shule nyingine ya msingi, ili kupunguza umbali wa wale watoto wanaotoka kule Ndolezi kwenda Mafinga au kwenda Mwongozo au kwenda Mkombwe Shule ya Msingi. Kwa hiyo, tunapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nawapongeza wananchi wote wa Jimbo la Mafinga Mjini kwa sababu, haya yote tunayofanya tunashirikiana kutoka Kata zote na Vijiji na Mitaa yote kwa sababu na wenyewe pamoja na jitihada na nguvu ya Serikali na nguvu ya halmashauri, lakini yapo maeneo kama wale wa Ndolezi na wale wa Kikombo walitoa nguvu zao kwa kushirikiana na jitihada za Serikali kufanikisha miradi ikamilike. Wale wa Kituo cha Afya cha Lufingo, wale wa Bumilayinga wote tunafanya kazi kwa kushirikiana, lakini pia, yote yanafanikiwa kwa sababu, tunashirikiana na uongozi wa Serikali kwa maana ya Mkuu wa Mkoa, Ndugu yangu Peter Serukamba na uongozi wake wa Mkoa, lakini na Mkuu wetu wa Wilaya Dkt. Linda pamoja na Madiwani, wote tunashirikiana na wataalamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanafanikiwa chini ya usimamizi wa Chama chetu Cha Mapinduzi chini ya Comrade Yassin Daudi, MNEC wetu Ndugu Asas na Katibu wetu wa Mkoa Ndugu Goma, lakini kwa pale Wilayani tuna Mwenyekiti wetu jembe Ndugu George Magelasa Kavenuke na Katibu wetu Ndugu Clement Bakuli pamoja na viongozi wa ngazi zote za chama. Hawa wote ninawapongeza kwa sababu, tunashirikiana kuleta maendeleo pamoja na wadau wa maendeleo muhimu sana wenzetu wa Water for Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wametuchimbia visima virefu vya maji kwenye shule zote za sekondari, kwenye zahanati zote, kwenye hospitali yetu ya Mafinga na kwenye vituo vyetu vyote vya afya vya Ifingo, Ihongole pamoja na kule Bumilayinga. Kwa hiyo, ninawapongeza sana na wadau wengine tunaoshirikiana nao kwa maana ya TARURA, TANESCO, RUWASA, MAUWASA, TFS na Shamba la Saohill pamoja na JKT Mafinga katika kufanikisha maendeleo ya wananchi wa Mafinga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi, sasa ninakuja katika mchango wangu. Jana kuna mtu alichangia hapa na alisema Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Mheshimiwa Prof. Mkumbo ni Singida Boys na mimi nasema nawa-consider wao kama wachezaji wa Yanga Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua kwamba, ule ushirikiano wao umeleta heshima kwa klabu ya Yanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama ingekuwa ni Simba ningesema hawa ni Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute. Kwa hiyo, ule ushirikiano umeiwezesha Simba kwenda robo fainali Klabu Bingwa, lakini ushirikiano ule ndani ya Yanga, wa Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, umeiwezesha Yanga kwenda kuchukua ubingwa na kwenda robo fainali. Sasa ninawaomba ushirikiano huu ambao nimetoa mfano, sasa na ninyi mshirikiane kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango kuhakikisha kwamba, uchumi wa nchi na maisha ya Wananchi wa Tanzania yanakuwa ni maisha ambayo yameboreshwa na yanakuwa na affordability. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili hayo yafanikiwe, tunapozungumzia bajeti, maana yake ni mapato na matumizi. Sasa yapo mapato unaweza kuyapata kwa kutoka jasho, lazima ufanye uzalishaji, lakini yapo mapato yanaweza kupatikana katika nchi yetu bila kutoka jasho. Ninawaomba Mheshimiwa Waziri, nendeni mkarejee mchango wa Mheshimiwa Kakoso wa mwaka jana wakati wa bajeti kuhusu namna gani Taifa linaweza likanufaika kutokana na hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi watu wa Gazeti la Mwananchi waliandaa kongamano la kuzungumzia mambo ya mabadiliko ya tabianchi na kwa namna gani hii changamoto inaweza kugeuzwa kuwa fursa. Inaonekana nchi yetu kwa kutumia misitu tuliyonayo, tunaweza tukapata takribani shilingi trilioni mbili na nusu zikachangia katika Pato la Taifa. Hebu wekezeni nguvu katika jambo hili na kuna dhana inajengeka kwamba, hiyo hewa ya ukaa watapata fedha watu ambao wametunza misitu asilia, lakini mimi naomba muende mbele, hata misitu ya kupandwa, hata chai, hata parachichi, hata mikorosho, unaweza kupata fedha katika suala zima la hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili. Ili tuweze kupata fedha maana yake ni lazima tuzalishe. Sasa nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Kilimo, kumekuwa na kilio kikubwa katika suala zima la kilimo cha chai. Kule Mufindi wawekezaji waliochukua hawafanyi chochote, wafanyakazi kwa miezi minne hawajalipwa mishahara, ukienda Rungwe kilio hichohicho, ukienda Lupembe kule kwa mwenzangu Mheshimiwa Swalle kilio hicho hicho, ukienda Korogwe, ukienda Lushoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu jamani tuone tunaokoa vipi sekta ya uzalishaji ya chai, ili kuona kupitia chai tunaendeleaje kupata fedha za kigeni kama alivyosema Mheshimiwa Mrisho Gambo. Mwisho wa siku tunahitaji dola, tutapataje dola kama hatujaboresha mazingira ya kuzalisha, tukauza hiyo chai tukapata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninawaomba hebu tujaribu kuliangalia katika muktadha mzima wa kuongeza mapato ya nchi yetu, lakini, ili haya mambo yaweze kwenda vizuri ni lazima miundombinu wezeshi iwepo. Sisi watu wa Mufindi maisha yetu ni kilimo hicho cha chai, mazao ya misuti na kilimo katika ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufanya majumuisho, utueleze hatma ya Barabara ya Mafinga kwenda Mgololo, tumesaini mkataba mwaka jana, Mwezi wa Sita, Tarehe 16, mpaka sasa mkandarasi hajaingia kazini. Ninawaomba, ile barabara ni uchumi sio tu wa Mafinga, Mufindi na Iringa, bali ni uchumi wa Taifa hili kwa sababu, kule kunatoka mazao ya misitu; nguzo, mirunda na mbao zinatoka kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unakuta pale malori, ma-semi trailers yame-park wiki nzima, hayawezi ku-move. Wakati wa mvua umesimamisha uchumi kwa sababu, yale magari yaki-move, nilishawahi kusema hapa, yatajaza mafuta, utapata fuel levy, Serikali itapata mapato. Kwa hiyo, hata gharama za uzalishaji zinakuwa kubwa, nawaomba sana, Mheshimiwa Waziri tuliangalie hili, lakini katika suala hilohilo ambalo ninalizungumzia tena la uzalishaji, Mheshimiwa Waziri tuliteta na wewe pale nje, sisi watu wa Mufindi ndiyo watu wa kwanza kuanzisha Benki ya Wananchi, ilikuwa inaitwa Mufindi Community Bank (MUCOBA).

Mheshimiwa Naibu Spika, benki nyingine za wananchi mnazoziona nchi hii, walikuja kujifunza MUCOBA, lakini benki hii kutokana na mtikisiko wa kiuchumi wakati fulani tuliyumba kiasi kwamba, ninamshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, na Mzee Yassin Daudi alikuwa Mwenyekiti wa Chama wa Wilaya. Tulikaa wakatusaidia, wenzetu wa Benki ya Zanzibar wakaja na wakaongeza mtaji, lakini all over a sudden mwaka jana, Mwaka 2022, TRA wamekuja kuchukua katika akaunti ambayo iliwekewa fedha za wananchi za mikopo ya asilimia 10 shilingi 681,000,000. Sasa mimi nashindwa kuelewa Mheshimiwa Waziri, benki ambayo inachechemea inawezaje ikadaiwa fedha kiasi cha shilingi 681,000,000?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mawasilisho kadhaa, nitayaleta mezani kwako unisaidie, barua imeandikwa kwa Kamishna kuomba jambo hili lifanyiwe kazi. Matokeo yake sasa Benki ya Wananchi wa Zanzibar imeona kwamba, hapa hakuna biashara na imeondoka, lakini Benki hii ya Wananchi wa Mufindi ilikuwa ni msaada kuondokana na ile mikopo tuliyosema hapa siku moja ni mikopo ya kausha damu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, hebu iangalie hii benki ambayo ni mkombozi kwa wananchi wa kawaida wa Mufindi, wanachukua mikopo katika gharama nafuu na pasipokutakiwa kuweka dhamana kubwa. Mimi naamini unaliweza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la miradi. Nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sisi tuna mradi, katika Mradi wa Miji 28 Mafinga tupo, lakini mpaka sasa hivi mkandarasi hajalipwa certificate nne, kaondoa watu wake site. Sasa tulijinadi tukasema kwamba, lazima kufikia Mwaka 2025 mradi utakamilika, sasa imebaki miezi saba, mkandarasi hayupo site. Nakuomba, wewe kama Waziri wa Fedha, Fedha zipatikane.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho na Mheshimiwa Rais kwenye hili ninampongeza sana, ameshiriki mikutano yote ya mazingira duniani akiendelea na hii slogan yake ya clean energy, sasa clean energy haipo tu kwenye kupikia. Mheshimiwa Waziri hebu kwanza tufanye incentives kwa watu wanaowekeza kwenye masuala mazima ya gesi, watu wanaowekeza kubadilisha magari yatoke mifumo ya mafuta kuwa ya gesi, sisi hapohapo tumekuja kuweka tena tozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaomba katika kipindi cha miaka mitano hebu kwanza tusahau, twende na slogan ya Mheshimiwa Rais ya clean energy. Sasa huku Rais anasema clean energy, sisi tunaweka tozo juu yake, hatuta-achieve hilo jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho. Mheshimiwa Waziri umesema kwamba, mafuta yakipanda, ile ikiwa imeshuka ile bei utakuwa unai-maintain, ili fedha iende kwenye barabara...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Chumi.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba kuhitimisha, naunga mkono hoja. Naomba haya niliyoyasema, hasa hili la MUCOBA na Barabara ya Mafinga – Mgololo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitilie mkazo.