Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi pia ya kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Tarehe 16 mwezi huu wa sita kwa maana ya juzi pale Jimbo la Igunga tulikaa mimi na Waheshimiwa Madiwani pamoja na viongozi wetu wa Kamati ya Siasa ya Wilaya na viongozi wetu wa chama wa kata zote 16 za Jimbo la Igunga. Tulikuwa tunafanya Tathmini ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kuangalia namna ambavyo tumetekeleza Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi 2020/2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapato ya halmashauri yetu ya Wilaya ya Igunga tukijitahidi sana kukusanya ni shilingi bilioni nne kwa mwaka lakini wakati tunafanya tathmini tulijikuta tumetekeleza miradi ya zaidi ya shilingi bilioni 70. Kwa mantiki hiyo nianze kwa kumshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake ya Awamu ya Sita kwa kutupatia fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye Jimbo letu la Igunga. Kwa shilingi bilioni nne ambayo tunaipata kama halmashauri ninaamini kwamba kama tungekuwa tukitumia fedha zetu peke yake ingetuchukua zaidi ya miaka kumi kufikia ambayo tumeyafikia ndani ya miaka minne. Tunasema, ahsante sana kwa Mheshimiwa Rais, ahsante kwa Serikali hii yetu na ahsante kwa Chama chetu Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze kaka zangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, hawa mimi ni majirani zangu lakini pia ni ndugu zangu. Niwashukuru kwa kazi nzuri na kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, fanyeni kazi sisi ndugu zenu tunawaombea na Mungu atawabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo matatu ningependa kuyachangia mchana huu ambayo naamini yanaweza yakasaidia kututoa hapa tulipo. Jambo la kwanza ningependa kuchangia ni suala la Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka yetu ya Mapato inafanya vizuri lakini kuna mambo ambayo yanahitaji kuboreshwa ili tuweze kuhakikisha tunakwenda vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuimarisha undugu na Utanzania kati ya Mamlaka yetu ya Mapato ya Tanzania na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni mahusiano kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Utakubaliana nami Mheshimiwa Waziri ana kazi kidogo ya kufanya kuwaasa maafisa wake waongeze mahusiano vizuri kati ya wafanyabiashara lakini pia na Mamlaka yao ya Mapato Tanzania (TRA). Wana-deal na watu ambao ni watu wa kawaida sana, sasa wao ni wataalamu na wamesomea hii kazi lakini sasa inabidi waende na approach ambayo itawasaidia kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabiashara wetu waweze kutoa ushirikiano kubwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na naamini litasaidia kuongeza hata wigo wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi trilioni tunazokusanya kwa sasa ukiwa na mahusiano mazuri kati ya wafanyabiashara na Mamlaka yetu ya Mapato Tanzania naamini tutaongeza wigo mkubwa wa ukusanyaji wa kodi nchini. Pia nimefanya kautafiti kidogo kumekuwa na changamoto; Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Maafisa wako wa TRA, wamekuwa hawana mahusiano mazuri sana na Viongozi wa Serikali kwa maana ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Kuna mazingira unakuta hata wanabishana au kama kuna vikao basi unakuta hata maafisa wako hawatokei kwenye vikao. Tunaomba muwajenge, muwaeleze tunajenga nchi moja tushirikiane katika kuhakikisha tunasonga mbele vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ningependa kulichangia mchana huu ni maendeleo vijijini kwa maana ya rural development and rural transformation. Kama Taifa kwa sasa tumefanikiwa sana kwenye maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye suala la shule za msingi ambapo tumeweza kufikia lile lengo la universal primary education. Kama Taifa tumejenga shule za msingi kwenye kila kijiji mpaka sasa, niamini ni vijiji vichache sana nchini havina shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa ni suala la umeme vijijini (rural electrification). Katika kutekeleza Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi, tuliahidi kila kijiji kitapata umeme. Tumefanikiwa pia nchini kwa sasa tumekamilisha suala la usambazaji wa umeme vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa zahanati, tumejenga zahanati nyingi sana nchini kwa maana inasaidia wananchi kupata huduma za afya. Pia na huduma za kifedha kuna suala la jambo la financial inclusion hapa na lenyewe tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa sababu ya miamala ya simu (kutumia mitando ya simu). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna maeneo mawili ambayo nimefanyia utafiti ni changamoto ambayo itatusaidia sana kwenda kupiga hatua nyingine katika kuhakikisha tunafanya maendeleo vijijini. Kwa kuwa ukijaribu kuangalia 70% mpaka 80% ya Taifa letu ni vijiji na siyo miji. Sasa kuna eneo la kwanza, eneo la barabara vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya Wabunge wamechangia hapa. Katika kukuza uchumi wa nchi mshipa namba moja ni suala la miundombinu kwa maana ya barabara na ukiangalia landscape ya nchi yetu maeneo mengi yana mito midogo midogo ambayo ni mito ya misimu. Sasa tuongeze fedha upande wa TARURA, mimi niwashauri Serikali kwa sasa mnatupatia takribani shilingi bilioni mbili kwenye kila jimbo, mkifikisha angalau shilingi bilioni tano kwenye kila jimbo tutafanya maendeleo makubwa sana katika Taifa hili na tutafungua uchumi kwa kiwango kikubwa sana. Hii ndiyo itakuwa eneo moja la kusaidia sana katika mabadiliko na maendeleo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunasema miundombinu kwa maana ya barabara ndiyo mishipa ya uchumi. Barabara zitajengwa vijijini lakini pia na yale madaraja madogo madogo ambayo kwenye mito yetu mingi, kwa sababu ukiangalia maeneo yetu mengi yanakuwa na mabonde mabonde tukishaweka haya madaraja madogo madogo na makalavati itatusaidia sana kuwa na barabara zinazopitika kwa mwaka mzima hata misimu ya mvua na itasaidia sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ningependa kulielezea Serikali ambalo kwa sasa inabidi tupambane katika kuhakikisha tunalifanikisha ni maji vijijini. Ukifanya utafiti katika vitu vya muhimu ukiacha pumzi jambo linalofuata ni maji. Tunaomba mwongeze nguvu, mwongeze fedha katika eneo la maji ifike hatua vijijini maji yasiwe anasa yaani kila mwananchi awe na maji nyumbani kama ulivyo umeme. Kama hana nyumbani basi yanakuwa karibu ili tuwaepushe wananchi kutokana na adha ya kutoka na matrela ya ng’ombe maji kilometa tano, kumi kwenda kwa ajili ya kupata maji. Serikali tunaomba mliangalie hili na kwenye kupitia mipango (Tume ya Mipango) mliangalie sana suala la upatikanaji wa maji ambalo ninaamini ni moja ya huduma ya msingi sana kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo ningependa kulichangia mchana huu ni Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025/2050. Nikupongeze kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila mnakwenda vizuri na Tume yako ya Mipango na wataalamu wote ambao mnashirikiana nao, lakini nikushauri katika Dira hii tunayoiandaa sasa hivi kwanza i-reflect mahitaji ya vijana. Taifa letu kwa sasa asilimia takribani 60 mpaka 70 ni vijana ambao ni chini ya miaka 45 (miaka 40 mpaka 30 kushuka chini) twende tukatengeze Dira itakayo-reflect mahitaji ya hili Taifa la sasa. Twende na mtazamo (thinking) ya kisasa ambayo ndivyo mnavyoliona Taifa la utandawazi. Tuangalie mila na desturi zetu, tuangalie mshikamano na umoja wa nchi yetu ambazo ni tunu zetu lakini tuangalie mahitaji ya Taifa tunalokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine la msingi tutengeneze Dira ambayo itatengeneza mazingira ya kuondokana na urasimu nchini. Kwa sababu katika mipango yako na uwekezaji jambo litakalokukwamisha katika nchi hii ni urasimu. Tumekuwa tukitoa mifano ya mataifa ya jirani kwamba kama mwekezaji anahitaji vibali ndani ya siku mbili, ndani ya siku saba amepata vibali. Kwetu sisi bado tunapigana mark time, mwekezaji anakuja miezi miwili, miezi mitatu bado anasumbuliwa na kuhangaishwa. Sasa unaangalia je? Ni nini? Tunamkwamisha nani? Tunalikwamisha Taifa letu. Mwangalie katika Dira ya Maendeleo mnayoitengeneza suala la urasimu mliwekee kabisa mwongozo tuje tuepuke vikwazo vingi katika uwekezaji, kwa sababu suala la uchumi wa nchi uwekezaji ndiyo indicator namba moja ambayo itatusaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tunatakiwa tuongeze wigo wa walipa kodi, tax base yetu bado ndogo sana. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Mipango mfanye jitihada, umizeni vichwa, think tanks wako waumize vichwa tuongeze tax base. Ni aibu kwa Taifa kutokuwa na walipa kodi zaidi ya milioni tano kwenye Taifa la watu milioni 60 angalau tuanze kusoma kwenye digits na milioni kumi na tano, milioni kumi saba za walipa kodi. Tutakuza sana uchumi na tutakusanya matrilioni ya fedha mengi sana kupitia Mamlaka yetu ya Mapato na taasisi zinazokusanya maduhuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ningependa kuongelea suala la sekta za uzalishaji. Kwenye sekta za uzalishaji Mheshimiwa Profesa liangalieni hili na tuwe na vipaumbele tuamue kama Taifa tunaamua kuwekeza kwenye nini? Nini kitakuwa kipaumbele kama Taifa kwenye sekta ya uzalishaji? Au tunaamua kwenda na sekta zote tunaamua kwenda na kilimo, ufugaji, madini, viwanda. Kama tunaamua kuweka priorities tuangalie yaani Taifa letu lifikie hatua tunajivunia kwamba tuna kitu tunakifanya kama Taifa kimoja ambacho kinatutambulisha duniani lakini pia kinakuza Pato na Uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia katika suala la Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mheshimiwa Waziri naomba mliangalie sana tuje na sera ambazo zitaweza kutusaidia kwenye suala la uboreshaji wa makazi ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna wananchi ambao wanaishi maisha duni sana huko vijijini, lakini katika dira hii ambayo tunaenda kutengeneza ya kwenda 2050 tuitengeneze na tutakuja na sera ambazo zitasaidia sana kuboresha makazi. Tuhakikishe wananchi wanaishi katika makazi bora na ndiyo namna ambavyo tunatoka kwenye dunia hii sasa, tunatoka kuwa nchi yenye kipato cha chini kwenda kipato cha kati, maana yake hata makazi ya wananchi wetu yawe bora zaidi pia wawe na ustawi ulioimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)