Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Mimi ninaanza mchango wangu katika eneo la kubana matumizi. Ni kwamba, kwa miradi yetu yote tuliyonayo katika nchi hii na bajeti yetu hii ya shilingi trilioni 49, kama hatuwezi kubana matumizi, yaani Serikali haiwezi kubana matumizi, bado ni hatari kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, sehemu ya kwanza ya kubana matumizi ilikuwa ni kuhakikisha magari yetu yote ya Serikali yanatumia gesi, yafungwe mitambo ya gesi. Hawa wenzetu, kupitia TEMESA, wafanye kazi hiyo au wataalamu wapelekwe India ambako sisi tulikwenda kujifunza jambo hilo tukaliona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakitoka na knowledge hiyo wakaja nayo Tanzania, kwa kupitia mikoa yetu sisi ya Tanzania, kote kule watakuwepo mafundi watakaofanya kazi hii kwa gharama nafuu, ili magari yetu ya Serikali yaanze kutumia mfumo huo wa gesi. Halafu na magari yetu sisi, ya watu binafsi, yaanze kutumia mfumo wa gesi, tutaokoa sana matumizi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakupa mfano mmoja tu; ni kwamba kama unajenga nyumba wewe mwenyewe tu binafsi, wewe ni mjenzi unajenga nyumba yako ya kuishi lakini unataka ule vizuri, unataka kula kuku, unataka kula nyama na unajenga nyumba, hiyo nyumba haiwezi kwisha. Kwa sababu, kuna wakati ni lazima upunguze gharama, upunguze matumizi, gharama ya familia kwa sababu, unafanya kazi ya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo hii sisi tuna miradi mikubwa, miradi ya reli, miradi ya meli, miradi ya barabara na bado tumekutana tena na Kimbunga Hidaya kikatuletea mvua kubwa, lakini bado tunatembelea magari ya gharama kubwa, kitu ambacho ni hatari kubwa sana kwa nchi. Katika eneo hilo mimi ninashauri, kwanza tunayo magari mabovu katika halmashauri, tunayo magari mabovu Serikalini; mimi ninamshauri Waziri wa Fedha kwa kumtumia Mfilisi wa Serikali, haya magari yote yanatakiwa kuuzwa kwa sababu, hizo ni pesa. Zipo mpaka meli ambazo zimechakaa, zipo feri zimechakaa, ukienda kila maeneo vyombo vya Serikali vimekaa ni lazima vile ambavyo vimepitwa na muda wake viondoke. Ninafikiri huo ndiyo utakaokuwa ni mpango wa kwanza wa kubana matumizi ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengine ambayo sisi tunataka kusaidia kuishauri Serikali ni namna ya kupata vyanzo vipya vya mapato. Chanzo cha mapato ambacho kinatumika na Serikali kwa sasa hivi cha kuongeza kodi bado ni hatari kubwa sana kwa maisha ya wananchi. Yako maeneo ambayo kodi ingeingia kwa ndani, inafichwa tu ndani ambako mwananchi anakutana nayo haoni kama amelipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo ambayo yamependekezwa, mimi ninaunga mkono kabisa. Yamependekezwa katika mafuta, hayo yote mimi sipingani na Wizara ya Fedha. Ni kwamba, ni lazima tukusanye, lazima tupate kodi tuendeshe nchi yetu. Tujiondoe katika mikopo mikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambacho ninataka kumshauri Mheshimiwa Waziri ni, je, kinachokusanywa kinaingia katika mfuko wa Serikali? Hiyo ndiyo alama ya kujiuliza. Ni kwamba wananchi wanalipa kodi, kule kwenye Halmashauri kule wananchi wanalipa ushuru, je, huo ushuru wote unaingia katika Mfuko wa Hazina au Mfuko wa Halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huko ndiko kunakotakiwa kuangaliwa kwa kiwango kikubwa. Ni kwamba tukiangalia wakusanyaji, hizo control number zinazotolewa, je, zinaingia moja kwa moja Serikalini? Kwa sababu, sasa hivi kila mnavyokua na teknolojia inavyopanda na watu ndiyo wanatengeneza mifumo. Wanakuwa katika majumba yao, ikitolewa control number haiingii katika control number ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo linalotakiwa kuchunguzwa sana. Watu wetu wa usalama, watu wetu wa fedha, basi walichunguze sana jambo hili kwa sababu, minong’ono na manung’uniko iko kule. Tunaona kwenye nchi za wenzetu, hawa watu wa namna hiyo wanaokaa na laptop wanaingilia mifumo ya fedha ya Serikali, kwenye nchi nyingine wapo, wanakamatwa wanapelekwa Mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna watu ambao wanasafiri, wanaweza wakasafiri hata kwenye ndege. Akaanza kuangalia kwenye laptop yake, yeye anakwenda kukaa kwenye kiti anaangalia ni sehemu gani kuna dola katika begi, inampa alarm. Sasa, kama imefikia hatua hiyo, basi na sisi ni lazima tuwe makini sana katika mifumo ya ukusanyaji wa fedha. Hapo tunaweza tukafaulu sana katika mapato yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, barabara zimeharibika. Miundombinu inatakiwa kurekebishwa kuanzia kwenye vijiji na kwenye miji yetu, lakini pamoja na miundombinu kuharibika mpaka barabara ambazo ni trunker na zenyewe zote zimeharibika. Ni kwamba, ni lazima tuhakikishe tunapata chanzo cha kutengeneza hizi barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kusaidiwa na mjomba, sisi Watanzania ni lazima tujifunge mkanda tutengeneze barabara zetu. Ndugu zangu Mheshimiwa Rais anaumiza kichwa sana, ni wapi atapata pesa, kwa ajili ya kutusaidia sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho ninapendekeza mimi ni kwamba, maeneo yote ambayo yanakuwa ni chanzo cha kupata pesa, basi kila mtu ni lazima afunge mkanda. Pesa zikusanywe kule na Mheshimiwa Waziri wa Fedha akutane na makundi yote maalumu. Makundi yote yanayofanya biashara, makundi ya machinga, makundi ya wajasiriamali na makundi ya wafanyabiashara wakubwa, basi tukae kujadiliana ni maeneo yapi ambayo sisi tunaweza tukapata chanzo cha kupata pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ninataka nilizungumzie hapa ni suala la mikopo. Ili tuweze kutengeneza uchumi wa nchi yetu tunamuomba sana Waziri wa Fedha ahakikishe riba zinapungua katika benki zetu, hakuna jinsi nyingine. Kwa hali ambayo tunataka tupate walipakodi wengi ni kwamba, ni lazima tupunguze masharti ya fedha Benki Kuu, ili wakopaji wawe wengi halafu tuweze kutengeneza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, nchi hii ule mfumo kwamba, kuna wafanyakazi na wakulima halafu kundi la wafanyabiashara likatolewa, basi huyo mkulima ataumia na huyo mfanyakazi ataumia. Kwa hiyo, hayo ni maeneo ambayo tuone ni namna gani wafanyabiashara wanaweza wakatafutiwa fursa, ili waweze kulipa kodi, waweze kufanya biashara na walipe kodi kwa ulaini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo ninataka kuzungumza hapa ni kuhusiana na faini. Faini iliyopendekezwa tunamuomba sana Waziri wa Fedha, ni kubwa mno, labda wafanyabiashara wanakwenda kufunga kabisa maduka yao. Kwa sababu, usipotoa risiti ukapigwa faini ya shilingi milioni 15, duka lina mtaji wa shilingi milioni 7 inamaanisha kwamba, tayari wewe unatakiwa uende tena, yaani unalikimbia duka tu. Ni kwamba, watu watakimbia maduka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliona Mwaka 1997 lilipokuja tu suala la VAT zaidi ya maduka 7,000 yalifungwa na watu wakahamia Malawi, wakahamia Zambia. Tukabakia sisi kukaa kwa sababu, tunaipenda nchi yetu. Sasa kwa hii faini itakayoanza Tarehe Moja, faini ya shilingi milioni 15, Mheshimiwa Waziri wa Fedha tunawaomba sana. Jamani Waheshimiwa Wabunge, kama kweli tutaipitisha hii faini ya shilingi milioni 15, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, lakini suala la hii faini ninaogopa sana kuunga mkono hoja kwenye hii faini kwa sababu, hata mimi nitakuwa ni miongoni mwa watu watakaojeruhiwa. Kwa sababu, risiti tunatoa, lakini unajikuta mtu mmoja una maduka sita sasa kwa hiyo, inamaanisha kwamba, watu wataishia gerezani. Mfanyakazi wako asipotoa risiti na wewe sasa hivi uko hapa Dodoma, Bungeni, tayari unaingia katika matatizo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)