Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya mimi kuchangia pia Bajeti Kuu ya Wizara ya Fedha na Mipango. Nami naanza kwa kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie, atusaidie kutuepusha na majanga katika nchi yetu ili mipango yetu mizuri iliyosomwa na mawaziri wetu na mipango yetu mizuri tuliyonayo iweze kutimia maana yake majanga nayo huwa yanavuruga sana bajeti za Serikali na bajeti za nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimesimama hapa na mimi naanza kuchangia kwa kushukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na mawaziri wetu wote ikiwemo Mheshimiwa Waziri wa Fedha chini ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa sababu yale yote makubwa na mazuri tunayosema tumeyafanya na tunawaambia wananchi wetu leo kwa vyovyote zile fedha lazima zitakuwa zimepita Wizara ya Fedha zikaja kwenye halmashauri zetu na zikaja kwenye mikoa yetu ndiyo maana tukapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa tathmini yangu kwa kule kwetu Kilombero tuna asilimia zaidi ya 80 ya kutekeleza mambo makubwa ambayo Chama cha Mapinduzi iliahidi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesimamia kutupatia fedha hizo. Kwa uchache kidogo nataka ku-mention mambo makubwa tuliahidi, tuliomba tupeni dhamana wananchi tunavyoenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wananchi wanavyotaka kuhukumu Chama cha Mapinduzi na kuhukumu Serikali yetu katika uchaguzi lazima wazingatie mambo yale ambayo tumeyaahidi na tumeyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza na Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo hapa ana barabara. Mimi nilikuwa sijui kama Wizara ya Fedha nayo ina barabara zake lakini barabara yangu ya lami ya Ifakara - Kidatu ipo chini ya Wizara ya Fedha, chini ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu wake pale wanasimamia kama contracting authority wa barabara ile kilometa 67 sasa hivi imebakia kama kilometa moja kukamilika. Nasisitiza Mheshimiwa Waziri nimekuomba mara kadhaa ukakague barabara hii na Daraja kubwa la Ruaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni uchumi mkubwa sana wa Kilombero na Mkoa wa Morogoro. Tunavyotaka kujenga uchumi kufungua Mkoa wa Morogoro kutokea Lindi kupitia Mahenge, kwenda Songea kupitia Malinyi na kwenda Njombe kupitia Mlimba barabara hii ilikuwa ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata Hospitali ya Wilaya katika miaka hii mitatu, minne ambayo tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tumepata miradi ya maji shilingi bilioni 45. Zile fedha anazofanya kule kwenye miradi ya miji 28 lazima zimepita Wizara ya Fedha. Kushirikiana na madiwani na viongozi wa vijiji tumejenga zahanati 12, sekondari za O level 12 na advance sekondari tano. Sasa hivi tuna mkandarasi wa lami ya Ifakara - Mlimba na yupo site na tunaomba barabara ya Ifakara kwenda Malinyi ianze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema Daraja la Ruaha karibu ya shilingi bilioni 10 linajengwa na linakamilika. Tumepata shilingi bilioni 500 kujenga kiwanda kipya cha sukari ambacho wakulima walikuwa wanalalamika miwa yao inabaki. Tunatarajia kupata substation na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Doto Biteko, alikuwa pale juzi. Ameenda kuzindua mradi wa substation shilingi bilioni 23 tumepata kupitia Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumepata Mahakama mpya ya Wilaya, tumepata Stendi mpya ya Wilaya, tumepata Soko jipya la Wilaya na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, alikuwa pale juzi amethibitisha hayo ninayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amenipa shilingi milioni 802 tumeshaanza na OCD na Mheshimiwa DC Dunstan Kiyobya, Kamati ya Usalama Wilaya ya Kilombero inasimamia ujenzi wa kituo kipya cha polisi cha wilaya, nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga vituo viwili vya afya na tumejenga soko la samaki. Sasa hivi tumepewa fedha kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO tunaboresha tuta la Ifakara kuondoa yale mafuriko ambayo mlikuwa mnatucheka nayo. Mheshimiwa Waziri, nakuomba tu kwamba fedha zile za tuta hazitoshi mtuongezee ili tuweze kujaza maji mengi katika Bwawa la Mwalimu Nyerere muweze kuzalisha umeme wa kutosha na tumepata lami za mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo hayo mazuri kuna changamoto nataka nizielezee kwa ufupi kabla sijaingia ndani ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri. Kila Mbunge hapa amesema na mimi nataka kusisitiza. Sisi tumepata mafuriko inawezekana tukawa namba moja nchi hii kwa ubovu wa barabara za mitaa. Tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri, katika vipaumbele vya kwanza vya kupeleka fedha pelekea fedha TARURA waboreshe barabara za mitaa. Hali ya Jimbo la Kilombero Halmashauri ya mji wa Ifakara ni mbovu sana na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, alikuwa pale ameona, sisi mji wa Ifakara karibu wote ulipata maji. Kwa hiyo barabara zote zina mashimo na makalavati yameharibika tunaomba sana utusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mafuriko hayo wakulima wameathirika kiasi kikubwa sana (wakulima wa mua na wakulima wa mpunga). Tunaomba Serikali muangalie namna ya kupeleka mbegu na mbolea katika msimu ujao wa kilimo na namna gani ya kuwapa pole wakulima hawa. Sasa hivi mkulima anavuna gunia la mpunga shilingi 70,000; bei bado ndogo. Kama Serikali inanunua mazao mengine na hii NFRA inunue pia mpunga ili ikuze bei kidogo wale walanguzi waweze kupandisha bei kumpa mkulima bei ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto ya kusambaza umeme katika vitongoji. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati amenipa vitongoji 15 lakini kazi ni bado. Tunaomba kufufuliwa kwa kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nimekuomba mara kadhaa, pale kuna nyumba kibao zipo Serikali imechukua kwa muwekezaji imerudisha Serikalini. Kiwanda cha Mechanical & Machine Tools na vifaa vyake vyote vinaharibika tu pale havifanyiwi usafi. Tembeleeni pale; Mheshimiwa Waziri wa Fedha unavyotembelea barabara ya Ifakara Kidatu tembelea na kile kiwanda. Fufueni kile kiwanda kama mlivyofufua Kilimanjaro Machine Tools ili wananchi wetu wapate ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho katika changamoto ni bei ya sukari. Sisi pamoja na ukulima wetu wa miwa, sukari ikiadimika kama mwaka jana hatukuvuna mua kwa sababu ya mafuriko (mua umelowa hauvuniki) sukari imekuwa haba, kiwanda kimezalisha chini ya uwezo. Tumekaa kila sehemu tunapita Kilombero inazalisha sukari inawezekana namba moja kwenye nchi hii, hakuna mkakati wowote au mpango wowote kwa wananchi wa pale Kilombero kuuziwa sukari kwa bei rahisi. Tunanunua sukari shilingi 6,000 au 5,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana tunamlaumu Mheshimiwa Waziri Bashe leo kwa hatua alizochukua. Mimi nipo kwenye mkutano wa hadhara wa biashara na DC na Kamati ya Usalama, wananchi wanalalamikia sukari bei 6,000 kwa nini na sisi tunalima miwa? Ndiyo Mheshimiwa Waziri Bashe, anapiga simu live kwamba Kamati ya Usalama ya Kilombero iende ikafungue kiwanda ndiyo tunapata sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nasisitiza sana ni kwamba kama dhahabu yetu nyeupe ya sukari ni muhimu sana Serikali ikawa na mipango wakati inaadimika tukaipata kwa bei rahisi. Ukiniuliza mimi leo kipaumbele changu cha kwanza tuzalishe sukari ndani ya nchi yetu na ndiyo maana Serikali imekubali katika 25 percent ya Kiwanda cha Illovo kukubaliana na muwekezaji kuwekeza shilingi bilioni 500 ili kiwanda kijengwe upya. Kiwanda kile kitatumia miwa ya wananchi ya kutosha na kitawezesha nchi yetu kujitegemea katika sukari; hicho ni kipaumbele changu cha kwanza lakini la pili; inapotokea changamoto kama msimu uliopita basi tupate sukari kwa bei rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri, nataka kusisitiza hapa na kusema nimeona umezungumzia mambo ya uwekezaji na miradi mikubwa kama ya reli. Sisi Kilombero na Morogoro tuna mpango wetu wa reli ya Kidatu kuunganisha na Kilosa na wataalamu wametuambia reli hii mkiiunganisha itatusaidia kuweka kontena Bandari ya Dar es Salaam ikaenda mpaka Johannesburg South Africa; hichi ni kiungio muhimu sana cha uchumi. Nimeona kwenye kamati na nimeona kwenye bajeti kwamba mtatoa fedha hizo, Mheshimiwa Waziri tunakuomba reli ya Kilosa - Kidatu ipatiwe fedha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwsiha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asenga, kengele ya pili hiyo.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)