Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa jioni hii ya leo ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii jioni hii ya leo kwa kuniwezesha kunipa afya ili na mimi niweze kusema machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya katika Jimbo letu la Bunda Mjini ambapo tumepata miradi mbalimbali kwa ajili ya wananchi wetu. Tumepata vituo vya afya, tumepata zahanati, tumepata barabara za mitaa na mradi mkubwa wa TACTIC ambao wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wanausubiri kwa hamu kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya mambo makubwa katika Taifa letu. Sisi kama Wabunge tumeendelea kushuhudia mipango mikubwa ambayo imeendelea kufanywa na Serikali yetu kama vile ambavyo ameendelea kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa na Taifa ambayo sisi kama Waheshimiwa Wabunge tunaishuhudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kushauri Wizara ya Fedha. Mimi pamoja na nafasi yangu ya Ubunge lakini mimi ni mfanyabiashara na biashara zangu nimefanya hapa hapa nchini pamoja na changamoto zote kubwa zilizopo. Napenda kumshauri pia Mheshimiwa Waziri kwamba nchi yetu ina vyanzo vingi sana vya mapato na hasa mamlaka kubwa ambayo imepewa nguvu za kusimamia ukusanyaji wa kodi katika Taifa hili ni Mamlaka ya Mapato Tanzania - TRA. Hawa kabla ya kufanya kazi hii naamini kuna mafunzo mbalimbali ambayo wanayapitia yanawafanya waweze kuelewa ni namna gani wanaweza kuwa-handle wafanyabiashara, lakini hizi mamlaka zingine za halmashauri zinakuwa ni tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaenda kwenye Halmashauri au mtu wa Halmashauri anakuja kwenye duka la mfanyabiashara ni mkusanya taka tu, amechukua tender ya ukusanyaji taka katika Halmashauri ile lakini huyo mkandarasi ambaye amechukua tender katika Halmashauri hiyo, anaweza kuwa na uwezo wa kwenda kufunga biashara ya mfanyabiashara kwa sababu tu ya kutokulipa hela ya taka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, saa zingine huyo mfanyabiashara anayefungiwa biashara yake kwa sababu ya kutokulipa fedha za taka katika biashara yake haoni ni sehemu gani ambayo anazalisha takataka, lakini tu kwa sababu sheria zinatutaka kulipa yule mtu analipa, lakini unakuta hao watu wanakwenda wanafunga biashara za wafanyabiashara. Kwa mfano, service levy, service levy saa zingine taasisi inataka kulipa service levy inaomba control number kwa Maafisa Biashara lakini kutoa ile control number inawachukua muda mrefu sana, saa zingine hata miezi mitatu saa zingine mpaka wafanyabiashara wanaamua kujitengenezea wao wenyewe control number zao ili walipe fedha zile za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nje na hapo yale madeni yanachukua muda mrefu na unapokuja kuletewa hesabu unakuta madeni yale yamekuwa makubwa. Mheshimiwa Waziri kwa sababu leo mpango huu tunaoujadili hapa ndiyo utakaofanya bajeti zingine zote za Wizara zote tulizozijadili na kuzipitisha ziweze kutekelezeka, zitatekelezeka baada ya kuwa tumepata makusanyo ambayo yanaridhisha au katika kiwango kile ambacho Serikali imejipangia kwa mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri usipotengeneza miundombinu mizuri kwa wafanyabiashara wako wa Taifa lako, utawafanya namna ya kukusanya kodi katika Taifa hili itakuwa ni kazi moja ngumu. Kuna mlolongo mwingi sana wa tozo na kodi mbalimbali, kwa mfano kuna service levy, kuna ushuru wa mabango, na huu ushuru wa mabango Mheshimiwa Waziri hapo nyuma umekuwa umepelekwa TRA na TRA walikuwa wanakusanya vizuri zaidi hata kuliko hivi ilivyo sasa, kwa sababu TRA walikuwa wanajua namna gani ya kuweza kukusanya kodi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na huo ushuru wa ada ya taka, zimamoto, OSHA, leseni, kodi ya zuio, kodi ya mapato ile ambayo saa zingine mfanyabiashara anakuja kupigiwa hesabu baada ya kukamilisha mwaka hesabu ya mwisho anatozwa ile ya asilimia 30 ya faidi aliyoipata kwa mwaka. Hizi kodi zote Mheshimiwa Waziri karibia zipo zaidi ya 10 hapa ninavyoziona, hizi kodi ingewezekana zingetafutwa zile kodi ambazo zinaweza kubebana Pamoja, zikawekwa pamoja halafu zikakusanywa kwa sehemu moja kuliko kuwa na mlolongo mwingi wa kodi nyingi ambazo zinakuwa kero kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara ndiyo zao letu tunalolitegemea kama Serikali ili wafanyebiashara tuweze kukusanya kodi kutoka kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuna hili jambo la faini la shilingi milioni 15,000,000 kwa mfanyabiashara yule atakayeuza halafu akashindwa kutoa risiti, aidha mnunuzi yle aliyenunua bidhaa kutoka dukani halafu akashindwa kuomba risiti akikutwa hapo mlangoni apigwe faini milioni 15. Lakini ukiangalia mazingira ya wafanyabiashara wetu katika Taifa letu ni mazingira magumu, halafu na mitaji yenyewe hawana na mitaji yenyewe waliyonayo hiyo kidogo wameikopa benki. Sasa leo ukikuta mtu ameenda dukani saa zingine akakuta mtandao haupo hata namna ya kutoa risiti haiwezekani, halafu akaondoka bila risiti akakutwa hapo mlangoni, akapigwa faini ya shilingi milioni 15, huku kibanda chake cha biashara kina mtaji wa shilingi milioni mbili, hili jambo naamini kwamba Waziri pamoja na Serikali ni vizuri mkaliangalia kwa sababu hili likipelekwa kwa wananchi na wafanyabiashara wetu walio wengi wao watashindwa, kwa sababu utakuwa unampiga faini ya shilingi milioni 15 inayozidi uwezo biashara yake anayoisimamia jambo ambalo kwa hali ya kawaida tu halitawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeiomba Wizara ya Fedha jambo hili ilirudie vizuri kulitizama nje ya hapo wafanyabiashara walio wengi watapigwa faini halafu tutakuja hapa Serikali itakuwa inataja madeni mengi na makubwa ambayo inawadai watu na wale watu uwezo wa kuyalipa yale madeni hawana. Mimi nikafikiri ni vizuri tukawadai watu madeni ambayo wanao uwezo pia wa kuyalipa, tunadai matrilioni ya matrilioni ya shilingi kwa wafanyabiashara ambazo ni kodi ambazo wamekusanya saa nyingine halafu wameshindwa kuzipeleka Serikalini lakini uwezo saa zingine mtu tunamdai labda miaka mitano au tunafanya naye kesi miaka mitano, inaisha miaka mitano uwezo wa kulipa zile fedha hana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni la wananchi wangu wa Kata ya Nyatwali ambao wamefanyiwa tathmini kwenye maeneo yao toka mwaka jana na mpaka leo wanasubiri fidia ya kulipwa fedha zao, ili waondoke kwenye yale maeneo. Mheshimiwa Waziri unaelewa wale wananchi walikuwa hawana mpango wa kuhama kutoka kwenye lile eneo, isipokuwa Serikali imelitaka kwa manufaa makubwa zaidi na wananchi wale wamekubali na sasa wanachosubiri ni malipo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hii leo tunavyozungumza hapa wananchi wa Kata ya Nyatwali wanataka kusikia kauli yako juu ya malipo yao, ni lini watalipwa fedha hizi kwa sababu, sasa hivi pale wanapoishi, wanaishi katika adha kubwa. Wamepata mafuriko pale kipindi cha masika, nyumba zimeanguka, zimeezuliwa na upepo, lakini namna ya kuzirudisha zile nyumba haiwezekani kwa sababu, tayari walishafanyiwa tathmini wakamaliza kwa hiyo, wapo njia panda, wapo katikati hawajui waende mbele, hawajui warudi nyuma. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nakuomba utakapokuwa unakuja kuhitimisha bajeti yako hapa kwenye Wizara hii ya Fedha uwaambie wananchi wa Kata ya Nyatwali kwamba, zile fedha zao wanalipwa lini kwa sababu, muda wote akili zao zote zinategemea kupata kauli yako, ili wao waweze kujua wanaanzia wapi wanamalizia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)