Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya. Hakika kila mwaka tunashuhudia bajeti ya Serikali ikipanda, hii ni kutokana na sekta nyingi zilizomo katika nchi kupatiwa pesa nyingi, kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango, Naibu Waziri Mheshimiwa Chande na wafanyakazi wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Mimi napenda sana leo nijielekeze katika kutoa pongezi kwa mafanikio yaliyopatikana katika Serikali hii kwa bajeti ya Mwaka 2023/2024 pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikianza kwa upande wa Kilimo. Tunaishukuru Serikali, kwenye bajeti iliyopita miradi mingi ya kilimo imefanyika na tumeona kabisa wameongeza ukubwa wa karibu hekta 543,306 zenye thamani ya shilingi trilioni moja na kuanza ujenzi wa mabwawa 14. Haya ni mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya Serikali imejitahidi kiasi cha kutosha na kwa kweli, tunajivunia, hakuna sehemu yoyote katika nchi hii ambayo imekosa mradi wa afya. Mimi mwenyewe binafsi pale kwangu Bagamoyo nimepatiwa pesa karibu shilingi milioni 900, kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe ya Bagamoyo ambayo ipo toka Mwaka 1957. Haya ni mafanikio makubwa sana ya Serikali yetu. Vile vile, nimepatiwa pesa karibu shilingi milioni 300, kwa ajili ya jengo jipya la EMD pamoja na vifaa tiba ambavyo vimeletwa. Kwa kweli, mambo ni mazuri katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu, halikadhalika, mafanikio ni makubwa sana. Mimi kwa kipindi kifupi nimekuwa Mbunge wa Bagamoyo, lakini kuna shule karibu nne mpya za sekondari. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali. Shule za msingi karibu tano mpya kwa hiyo, Serikali inajitahidi sana katika kutumia bajeti yake katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya mawasiliano. Naishukuru Serikali, sasahivi sehemu nyingi ambako kulikuwa hakuna mitandao, mitandao inafanya kazi. Hata wanavijiji wenzangu kutoka sehemu za Makurunge, Fukayosi na Kijiji cha Mkenge walikuwa na tatizo kubwa la miundombinu, sasahivi wanapata mtandao kama kawaida. Haya ni mafanikio makubwa sana ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi labda nirudi katika Bajeti ya Mwaka huu 2024/2025. Naipongeza Serikali kwa bajeti kubwa ambayo inakadiriwa kuwa karibu shilingi trilioni 49, lakini kuna mambo mengi mazuri. Kwa kweli, wananchi wameifurahia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nataka nizungumzie mkakati wa kuongeza kodi ya mapato ambao Serikali wameuonesha. Kuna Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mapato, Sura Namba 438, ambayo wenzangu wote wameizungumzia na sio vibaya tukairudia kwa kuona kwamba, hili jambo kwa kweli, bado halijakaa vizuri. Sura Namba 438, Kifungu 86(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi kimesema kwa kuweka ukomo wa faini ya juu ya kosa la kutokutoa risiti kwa kiasi cha currency 1,000 sawa na shilingi milioni 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwa Watanzania, mimi nafikiri Watanzania wengi watafunga maduka yao, biashara zao nyingi zitafungwa. Leo hii mwananchi anayetoka katika Kijiji cha Mkenge, ambaye hajui maana ya hii EFD risiti anaweza akaenda katika duka akakamatwa kwamba, kwa nini hakuchukua risiti na mwenye duka akakamatwa. Hii naona kwamba, Mheshimiwa Waziri, hebu jaribuni kuiangalia kwa kweli, bado tunahitaji ukusanyaji wa kodi ufanyike, lakini kwa faini kama hizi sidhani kama kutakuwa na afya katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nishauri kitu kimoja katika suala la ukusanyaji wa kodi. Kwa kweli, suala la ukusanyaji wa kodi ni suala la muhimu sana katika nchi. Ninaiomba sana Serikali, sasahivi kifike kipindi Mameneja wa TRA katika Mikoa yote wawe walimu wa masomo ya kodi katika shule za msingi na shule za sekondari, ili kizazi chetu kione umuhimu wa kulipa kodi. Sasa hivi watu wengi tuliopo hatuoni umuhimu wa kulipa kodi, vizazi vyetu tusivirithishe hii hali ya kutokulipa kodi. Itolewe elimu maalum kwa wanafunzi wa shule za msingi na shule za sekondari, waambiwe umuhimu wa kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi aambiwe kabisa hili darasa unalosoma ni kodi ya Serikali. Haya madawati unayokalia haya ni kodi ya Serikali. Kwa hiyo, itafutwe njia yoyote ya kutoa elimu kwa vizazi vyetu vya chini, ili huko badae tusijetukapata tabu ya kulalamika katika ukusanyaji wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa mapendekezo yake. Ninampongeza katika Sura Namba 148, Kipengele cha 18, kuliondolea na kulipa msamaha wa kodi Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania, ili liweze kufanya majukumu yake vizuri. Mheshimiwa Waziri, kwa hili nakupongeza sana. Kwa kweli, ilikuwa ni changamoto na janga kubwa, watu walikuwa wakihangaika kutoa vifaa vyao bila mafanikio. Ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo nataka kuligusia hapa. Katika Sheria ya Sukari, Namba Sita. Hapa wanazungumza kwamba, NFRA kununua sukari, kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununu sukari, kuratibu na kuhifadhi pengo la sukari kwenye hifadhi ya chakula ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme kitu kimoja. Kama sikosei mwaka jana au mwaka juzi kuliletwa hoja binafsi hapa Bungeni kwamba, NFRA imeshindwa kununua mahindi ya wananchi, ilikuwa haina pesa kabisa. Mheshimiwa Rais akaingilia kati, pesa zikatolewa, mahindi yakanunuliwa. Leo hii mnataka kuipa mzigo tena NFRA wa kuingia katika kununua na kuhifadhi sukari, hii pesa inatoka wapi? Ni wapi NFRA wanaipata wakati mahindi ya wakulima bado hayajapata soko? Kwa nini kwanza wasiingie katika mahindi halafu badae huko, kama mambo yao ya kipato yakiwa mazuri au bajeti yao ikiwa nzuri, ndio waingie katika kununua sukari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa mimi naona kidogo kama kuna changamoto ambayo itakuja kujitokeza mbele ya safari. NFRA wakipewa mamlaka ya kununua sukari inawezekana wakatokea watu wakaenda wakapata vibali kwa jina la NFRA na wakaenda kununua sukari ikaja kuwa disturbance kubwa kwa wazalishaji wetu wa sukari hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda kuchukua nafasi kuongea kwamba, hapa pana tatizo kidogo, hebu tuliangalie vizuri kwa sababu, haiwezekani wazungumze kwamba, wazalishaji wa sukari wanaficha sukari kwa hiyo, NFRA wanunue sukari, ili kuwadhibiti. Hii sio sahihi kwa sababu, mzalishaji wa sukari hafichi sukari, bali anayeficha sukari ni distributor anayeuza sukari. Hivi mpaka leo Serikali imeshindwa kuhakikisha kwamba, inawadhibiti hao wanaoficha sukari katika maghala mpaka wachukue maamuzi kwamba, NFRA ndio wanunue sukari? Mimi naona kweli, hii haijakaa sawa, kama wameshindwa kununua mahindi wataweza kununua sukari kweli? Hapa ni kuingiza Serikali katika mtihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine katika hicho kipengele cha pili, kutoza shilingi hamsini kwa kilo ya mabaki ya uzalishaji wa sukari (by product). Mimi hapa ninapenda nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, sukari ina by product nyingi, sukari ina molasses, sukari ina ethanol, sukari inatoa by product ya bagasse, sasa ni kipi hapa ambacho mnakwenda kukichaji shilingi hamsini katika hii by product? Tunataka kukijua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise mkisema mnachaji by product zote kwa shilingi hamsini kwa kilo, hii itasababisha matatizo kwa wafanyabiashara, itasababisha matatizo kwa wenye viwanda. Leo, kesho na keshokutwa wenye viwanda watashindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara vizuri kwa sababu tu kodi zimeongezeka. Hebu iangaliwe kwa sababu, kitu kama bagasse ambayo inazalishwa tani nyingi sana katika uzalishaji wa sukari haitumiki sana. Kitu kama molasses soko lake sio kubwa sana, labda hapa muangalie ni kitu gani katika hivi mtakwenda kuchaji shilingi hamsini kwa kilo, lakini sio kwenda kuchaji shilingi hamsini by product zote ambazo zinaweza kuzalishwa katika sukari. Mheshimiwa Waziri, hii haijakaa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napenda kuishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya. Mheshimiwa Waziri pale kwangu Bagamoyo pana bandari ambayo inakusanya pesa nyingi, inakusanya mapato mengi kwa Serikali, lakini Bandari ya Bagamoyo imesahaulika sana. Hakuna kinachoendelea kwa maana ya ujenzi, hakuna kinachoendelea kwa maana ya miundombinu, kila mwaka bajeti inapangwa, lakini bado hali haijakaa sawa. Hebu ikumbuke ile bandari ijengwe vizuri, ili iweze kuinua kipato kwa Serikali kwa sababu, inakusanya mapato mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda pale Meneja wa TRA anakaa katika kontena. Meneja wa TRA ambaye pengine anakusanya karibu shilingi bilioni mbili kwa mwezi anakaa katika kontena kwa kweli, hali hii haipendezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuweka mkakati au mpango wa kuja kujenga bandari ya uvuvi Bagamoyo. Hiyo nimeiona katika bajeti na katika mipango, lakini sasa nataka niseme kitu kimoja, Bagamoyo kuna chuo cha uvuvi pale Mbegani. Kile chuo kina hatihati ya kuondolewa kutokana na kuchukuliwa kwa bandari, lakini chuo kile kinatakiwa kiwepo Bagamoyo, ili kwenda sambamba na hiyo bandari ya uvuvi ambayo inatarajiwa kujengwa. Chuo kile bado kina eneo la karibu ekari 400 ambazo zipo pale, hazina kazi kwa hiyo, Serikali ifikirie itakapoamua kujenga Bandari ya Uvuvi Bagamoyo, basi na chuo kile kiendelee kuwa palepale, kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana wetu, ili waweze kuingia katika sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza tena Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara yote kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya. Pia, ninampongeza Mheshimiwa Rais anatupambania sana, majimbo yetu mengi yako vizuri, miradi mingi ya maendeleo ipo, hatuna shaka kabisa na tunamwombea kila la heri. Mheshimiwa Rais, bajeti ya Mwaka 2025 tutakuwa tumefanya mambo makubwa zaidi kuliko hapa tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)