Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji jioni, lakini kabla sijaanza mchango wangu ambao nitauelekeza katika maeneo makubwa matatu, kama ushauri kwa Serikali na kama maoni yangu nikiwa kama Mbunge muwakilishi kabisa wa wananchi wa Singida Magharibi, ukweli lazima tuuseme. Umuhimu wa kusema ukweli ni kuweza kulisaidia Taifa liweze kuwa na mtazamo ambao ni sahihi kutoka mtazamo ambao sio sahihi ambao unaweza ukajengwa katika mazingira tu ya kijamii, kiuchumi ama mazingira mengine ya kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezunguka Nchi ya Kenya kwa mwaka huu, nimekwenda Uganda na nimekwenda Rwanda. Nataka niseme kwa dhati ya moyo wangu kwamba, standard za kuulinda uchumi wa Tanzania zinazofanywa kwa makusudi na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wake wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kama hautembei unaweza usielewe haya ninayoyasema. Standard za kuulinda uchumi kwa Afrika Mashariki kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, wewe na Serikali yako na Rais wetu mnalitendea haki sana Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia jambo zima la inflation toka dunia imetoka katika misukosuko ya Covid-19, angalia inflation katika Nchi ya Rwanda, angalia inflation katika Nchi ya Uganda na Kenya kwa statistics. Tanzania tunafanya the best katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa Nchi za SADC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu na mimi niko proud na Waziri wa Fedha. Kwanza huenda kwa sababu tu nitasema, mtasema huyu anamsemea kwa sababu ni ndugu yake wa Singida. Mimi nazunguka duniani, mmenipa nafasi ya kuwa mwakilishi kwenye Bunge la Dunia, ninazunguka dunia yote. Viwango vya namna uchumi wa Tanzania unavyokwenda Mheshimiwa Waziri shikamoo, unajitahidi sana kaka yangu kuliweka Taifa katika misingi ambayo imewapunguzia economic shock Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia baadhi ya wachangiaji wamezungumza wamesema…
MBUNGE FULANI: Eti, rudia.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ananiambia nirudie. Nimesema kwamba, juhudi ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Wizara hii ya Fedha imesababisha kupunguza economic shock kubwa ambayo ingeweza kuleta frustration kwenye nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza wachangiaji, kaka yangu ametoka kuchangia hivi karibuni, hii Finance Bill mnayoileta mwaka huu, nawaambia mimi nitakuwa Mbunge wa kwanza kuiunga mkono kwa sababu kubwa zifuatazo, haiwezekani kama Taifa tukawa tumewapa monopoly watu wachache kuagiza sukari. Wamepewa monopoly na Serikali kuagiza sukari na wamepewa incentive, mimi ni muumini mzuri sana wa viwanda na sina maana kwamba, viwanda vyetu vya sukari vinafanya vibaya, lakini wanafanya vitu ambavyo vina-abuse soko na kumuumiza mlaji wa mwisho, ambaye ni mwananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya, nikupe mfano mdogo. Mwaka jana Wizara ya Kilimo ime-analyze gape la sukari kwenye nchi wakapata tani 60,000. Wakawaita wenye viwanda wakakaanao chini wakawaambia agizeni hii sukari. Nakwambia Mheshimiwa Waziri kama sio makusudi viwanda vyote vya sukari viligoma kuleta sukari nchini, why should be like this? Hivi kweli tuingie gharama ya kuwapa mzigo watanzania walaji wa mwisho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari ilifika mpaka shilingi 7,000. Mheshimiwa Waziri, mimi leo nataka kusema harakisha, ikiwezekana mngekuwa mnaweza kurekebisha Kanuni, Finance Bill ije haraka, tutaipitisha kwa msimamo mmoja, Wabunge wote tutaipitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa hatuwezi kuruhusu monopoly ya kuagiza sukari inafanywa na watu saba. Wakipewa vibali wanachukua wanakwenda kuviuza kwa watu kwa expense ya kuja kuwapa mzigo walipa kodi ambao ni raia wa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo jambo nikiwa kama Mbunge ninayetokana na Chama Cha Mapinduzi, Mbunge ambaye kazi yangu ni kuja Bungeni, kusimama na kuyasemea masilahi ya walipa kodi ambao wamekiamini Chama changu kilichopo madarakani kwa ajili ya kuwapigania katika welfare zao, hatuwezi kuruhusu jambo hili. Kwa hiyo nataka nimwambie Waziri wa Fedha pamoja na Watu wa Mipango, hiyo Finance Bill tutaipigia debe kwa sababu inagusa masilahi mazima ya walipa kodi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nalotaka kuishauri Serikali yangu; Hayo mengine sina lengo la kumwingilia Mheshimiwa Spika na Kamati yake, yako kwenye Kamati ya Maadili, Mheshimiwa Mpina amepelekwa kwenye Kamati ya Maadili, sitaki kuingilia. Hata hivyo, nachotaka kukuambia ni kwamba Serikali yoyote duniani itakapokosa kuwa na nguvu ya kuingilia soko inapoona raia wake wanafanyiwa makusudi na kuibiwa, Serikali hiyo inakosa legacy ya kuiongoza nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia na Serikali yake hawawezi kuona kuna wafanyabiashara wachache wanajipanga kuona bei sukari inafika shilingi 7,000 Rais akae ametulia aseme kwamba; “Eeh, tunalinda viwanda vya ndani.” Hata ingekuwa ni mimi nisingeruhusu hiyo hali. Jukumu la kwanza la Serikali yoyote iliyochaguliwa na wananchi ikaaminiwa jambo la kwanza ni kulinda welfare ya watu wake, hiyo ndiyo kazi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna hoja huku zimezungumzwa, mimi sina lengo la ku-interfere mambo ya Kamati. Unaposema kwamba Serikali imepata hasara ya shilingi bilioni 500, where do you get these economic calculations? Unazitoa wapi? Siku zote tunapoagiza shortage ya sukari na tunapoangalia sugar gap tunatoa exemption ya uagizaji wa sukari. Sasa hizo shilingi bilioni 500 zinatoka wapi? Hili kama siyo lengo la kutaka kuichonganisha Serikali na wananchi walioko nje waone kwamba Mama Samia ameshindwa kuisimamia Serikali anataka kuumiza wananchi. Haya mambo kwa Wabunge makini, tuliosoma kwa kodi za walipa kodi, tunaojua thamani ya Taifa letu we will never allow them to happen over our dead body kwenye Taifa letu, hatuwezi kukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukachekeana, tukaoneana haya kwenye mambo, when it comes kwenye mambo yanayohusiana na masilahi ya Taifa letu tutailinda Serikali yetu kwa wivu na gharama kubwa kwa masilahi ya Watanzania. Hili nalisema wazi mchana kweupe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nilishauri kwenye bajeti ya Mheshimiwa Nape. Mheshimiwa Mwigulu nataka nikuongeze wigo wa kukusanya kodi. Tulizungumza na kaka yangu Mheshimiwa Sanga; tulisafiri na wewe kaka yangu kwenda Marekani, tulichojionea kwenye mataifa makubwa ambayo Watanzania siku zote mnatoa mifano; “Eti kwa nini Marekani wana barabara nzuri, kila kitu angalia Ulaya.” Those guys wanalipa kodi. Lazima tujenge utamaduni wa watu kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenye Taifa letu mkiangalia kwenye statistics, zinaonesha wanaotubeba kwenye kulipa kodi ni watu wasiozidi 5,00,0000, Taifa lenye watu milioni 60 lakini nguvu kazi tuseme ni watu milioni 30, wangapi wanalipa kodi? Watu hawalipi kodi. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nakupa mfano mdogo na nataka nikuulize swali, ni madereva wangapi wanaoendesha tax mtaani mmewasajili kidigiti na mnjua hela wanzokusanya kwenye tax? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo kuna taxi zinapaki Airport, kila siku natoka airport nashuka inanileta nyumbani na ninalipa shilingi 20,000. Nani analipa kodi kwenye ma-tax haya yanayoendeshwa barabarani? Nani analipa kodi kwenye majumba? Mimi mwenyewe nina nyumba zangu nimepangisha watu wanakaa, hata mimi nazungumza hapa sijawekewa mfumo na Serikali kuhusiana na hela ninazozipata kwa kulingana na kodi za nyumba zangu, kodi za Serikali zinakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanadanganya, mtu ananunua kiwanja anauza, value imepanda anadanganya Serikali ameuza kiwanja shilingi milioni 200, ameiba zaidi ya shilingi milioni 160. Serikali haya mnashindwa kuya-monitor. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nataka nikusaidie mawazo, digitalize uchumi wa Tanzania, ondoeni cash economy. Ninawambia tax base ya nchi itaongezeka, Serikali mtakusanya mapato. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, mtajenga uchumi wa kisasa utakaoweza kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ninaloshauri Serikali yangu. Kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa unafanya kazi nzuri na kubwa katika Wizara yako. Wewe pamoja na timu ya watu wako tunakuona mpaka umekwenda kula chakula sijui kinaitwa mlonge, tukasema labda utamsahau Mama Alaska na utahamia kule lakini tunamshukuru Mungu ulirudi. Ninaomba nitoe ushauri kwa Wizara yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na changamoto ya ma-engineer kule kwenye mikoa. Sometimes unakuta mtu ambaye hana fani ya engineer anakwenda kusimamia barabara. Nakushauri kupitia bodi zako sijui ERB na akina nani, tengeneza pool ya vijana waliomaliza chuo kikuu ambao ni ma-engineer wawekeni kwenye list hakikisheni kila mkandarasi anayepata kazi kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawachukua vijana wasiopungua watano waliomaliza vyuo vikuu wapate skills. Wakimaliza mradi kwanza watapata kipato, pili mtakuwa mnatengeneza technology transfer kwa zile kampuni ngeni kwa vijana wa Kitanzania. Baada ya miaka mitano kampuni za wazawa wa Kitanzania zitakuwa na uwezo wa kuchukua tender kubwa. Mheshimiwa Bashunga ninalisema hili nikiwa na imani na wewe kama Waziri kijana unaweza ukalifanya kwa lengo la kusaidia nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho lakini siyo kwa umuhimu. Kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, umepewa Wizara kwa muda mfupi umefanya kazi kubwa na ya kizalendo. Kwa mara ya kwanza nimepata muda wa kusoma mpango wote, hongera sana. Hivi ndivyo watu wa Singida wanavyofanya, hivi ndivyo Singida inavyotoa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naweza kusema kwamba, kwa mpango huu na kwa miaka ijayo, alisema Mheshimiwa Askofu Gwajima watu wakafikiri anatania, jitahidini mipango tunayoipanga tui-reinforce kwa sheria ili kiongozi yeyote anayekuja kwenye Taifa letu apite kwenye njia ya mipango na maono ya Taifa kwa miaka 100 inayokuja. Tukiweza kufanya namna hii tutakuwa tumelijengea heshima Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na kwa haya niliyoyasema kwa uimara wa uchumi wa Taifa letu, Rais wetu anavyohangaika kutafuta fedha huku na huko, ninakiri na kusema hadharani mchana kweupe kwamba Rais Mheshimiwa Dkt. Samia ameonesha uzalendo mkubwa, ujasiri mkubwa na nguvu kubwa kama mwanamke. Mimi Mbunge wake nasema Mitano tena kwa Mama, mwenye wivu ajinyonge. Mimi Mbunge wa wananchi ndiyo nimekwishasema sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.