Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana na mimi kupata nafasi ya kuchangia kwa siku ya leo kwenye hii Wizara ya Maji. Tunamshukuru sana Mungu kwa kuendelea kutupa afya na nafasi ya kuwatumikia wananchi ndani ya nyumba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiofichika kwamba, maji ni muhimu sana kwa wananchi wetu na Watanzania kwa ujumla. Bila maji tafsiri yake ni kwamba hakuna kinachoweza kufanyika. Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa kocha mzuri na ukocha mzuri unatokana na namna alivyoamua kupanga wachezaji wake toka mwanzo kwenye kila namba na namna wachezaji wake walivyoamua kucheza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Aweso kwa kuwa mchezaji mzuri sana kwenye Sekta ya Maji. Yeye mimi ninamchukua ni kama namba tisa bora kabisa kuwahi kutokea kwenye Sekta hii kwa sababu ya aina ya utendaji wake wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu zozote zile ndizo zinatufanya sisi kama Waheshimiwa Wabunge tuweze kufahamu kazi kubwa ambayo anaifanya Mheshimiwa Aweso na Sekta yake na Watumishi wenzake wote kwenye Wizara ya Maji. Utakubaliana na mimi kwamba katika moja ya jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Waziri ameweza kulifanya leo hii, ukitafuta kila Mheshimiwa Mbunge mwenye mradi wa maji humu ndani na yeye amekuwa ni kama sehemu ya engineers wanaotekeleza ule mradi. Hii yote ni kwa sababu ya ushirikishwaji mkubwa. Hii namna ameisambaza mpaka kwa Watendaji wake wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwapongeza sana watu wa Mamlaka ya Maji na Wizara nzima kwa ujumla na taasisi zake zote wakiwemo hata wale RUWASA, ambao wanashughulika na maji maeneo ya vijijini. Ukiangalia takwimu, kwa mfano; nilikuwa ninajaribu kumsikiliza Mheshimiwa Aweso pia nimesikiliza vizuri sana Hotuba ya Kamati. Upatikanaji wa maji umeongezeka. Kuongezeka kwa huduma ya upatikanaji wa maji vijijini na mijini kutoka asilimia 77 mpaka 79.6 vijijini na asilimia 88 mpaka 90 mjini. Hili ni jambo kubwa sana na hii inaenda sambamba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Jiji la Mwanza ukichukulia miradi mingi mikubwa ambayo imetekelezwa tumekuwa na chanzo cha maji kwa zaidi ya miaka 40, kikiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 90 peke yake. Leo ndani ya miaka miwili peke yake na miaka mitatu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imejenga chanzo kikubwa cha maji kilichokamilika kwa asilimia 100 kwa zaidi ya shilingi bilioni 69, kikiwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni 48 kwa siku. Haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wetu kwenye miji hii tunayo wawakilisha ilikuwa ni jambo la aibu sana mtu anaishi zaidi ya kilometa tano kutoka lilipo Ziwa Victoria, lakini hana uhakika wa maji safi na salama ya kunywa. Leo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini ya Mheshimiwa Aweso na timu yake nzima wamefanikisha ukamilishaji na ujenzi wa chanzo kikubwa cha maji na cha kipekee kinachokwenda kuwahudumia na kuwaondolea adha watu wa Mji wa Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chanzo hiki kitahudumia zaidi ya watu 450,000. Nimetazama kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri pamoja na miradi mingine anaeleza namna ambavyo itahudumia Watanzania zaidi ya 4,000,000 kwa miradi yote ambayo imekamilika. Tafsiri yake ni nini? Kwamba, tunapozungumza tatizo la maji kwenye nchi hii ni lazima tuwe na mikakati ambayo italeta tija na kufanikisha kwenye miradi yote ambayo tumeitekeleza. Jambo hili Wizara ya Maji, kwa miaka hii miwili wamefanya kazi kubwa sana, kwa sababu shida iliyokuwepo kwa Watanzania ni miradi inapoanzishwa na kushindwa kukamilika kwa wakati na hivyo kushindwa kufikisha huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza sana Wizara ya Maji, kwa sababu wao katika miradi ambayo wameifanya kwa ubora zaidi ukiachana na ule mradi ambao Waheshimiwa wameshautaja wa Arusha, lakini Mradi wa Butimba ni kielelezo kikubwa kwenye nchi hii kwamba, Serikali ikiamua inaweza na pale inapoamua inaweza kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza sasa hivi tunatarajia na nikuombe sana Mheshimiwa Aweso. Katika kazi kubwa ambayo umeifanya, watu wa Mwanza wanayo matarajio na imani kubwa kwenye mradi ambao tutakwenda kusaini muda siyo mrefu wa usambazaji wa njia na bomba za maji, ujenzi wa matenki zaidi ya matano yatakayobeba zaidi ya lita milioni 31 kwenye Kata ya Kishili kule Fumagila, Nyamazobe kwenye Kata ya Mkolani na kule Buhongwa. Hii itakwenda mpaka kule Usagara kwenye Wilaya ya Misungwi. Pia, itakwenda mpaka Kisesa kwa Mheshimiwa Kiswaga. Tafsiri yake watu wa Mwanza, Nyamagana na pembezoni kule Ilemela tatizo la maji linakwenda kuwa historia. Hii peke yake inatosha kusema hongereni sana Wizara ya Maji kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliposema suala la ushirikishwaji na wewe ni shahidi tulikuona kwa mara ya kwanza kwenye uzinduzi wa ule mradi wa maji kule Kiwira tukasema kweli shughuli imepata mwenyewe. Mheshimiwa Aweso, amesema hapa utulie usiwe na presha kwa sababu majukumu uliyonayo ni makubwa na atahakikisha anakwenda Kiwira kila mara kama alivyofanya Butimba kuhakikisha ule mradi unakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa zaidi tunafahamu watu wetu wengi wanaamini kwa kuona na miradi mingi ambayo tunaitekeleza muda fulani hivi imekuwa haikamiliki kwa wakati. Kutokukamilika kwake kwa wakati tumeona hapa Kamati imesema vizuri sana. Tunapokuwa hatuna fedha za kutosha hatuwezi kukamilisha miradi hii kwa wakati. Miradi hii ili ikamilike kwa wakati ni lazima tuwe na fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Waziri wa Maji na timu yake, ni vyema sana tukafikiri kama Kamati walivyopendekeza turejeshe ile shilingi bilioni 137, ili Wizara iweze kufanya kazi vizuri. Wakandarasi wetu ambao hawalipwi kwa wakati siyo kwa sababu Wizara ya Fedha inazo hela imezikalia; hawalipwi kwa wakati kwa sababu Wizara haina fedha. Kwa hiyo, tuhakikishe fedha zinakwenda Wizarani na Wakandarasi walipwe ili miradi ikamilike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitazama vizuri Mheshimiwa Aweso, alipokuwa anasema Benki ya Dunia imetupa tena nafasi kwa mara ya pili mfululizo kwa kutuongezea idadi ya Halmashauri kutoka 80, mpaka 137 na Mikoa kutoka kumi na ngapi mpaka ishirini na ngapi. Haya ni matokeo makubwa ya uadilifu na uaminifu kwenye utendaji wa kazi za miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tunasikia hapa miezi michache iliyopita Mheshimiwa Aweso na Wizara wanaongelea miradi kichefuchefu. Miradi hii ndiyo iliyokuwa inawafanya wananchi wachukie. Wananchi wanakichukia chama, wananchi wanawachukia hadi Wawakilishi wao. Ni kwa sababu fedha za kutekeleza haya hazipo.

Mheshimiwa Spika, miradi ya maji Kamati imesema ni miradi mikubwa inayohitaji fedha za kutosha. Haiwezekani kama tukitegemea hizi shilingi bilioni 600, hatuwezi kutatua changamoto za maji tulizo nazo. Kwa hiyo, Wizara na Serikali isisite kukopa kwa ajili ya miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninarudia tusisite wala tusiogope kukopa kwa ajili ya miradi ya maji kwa sababu mwananchi aliyepo kule Fumagila, mwananchi aliyepo Kanenwa na mwananchi aliyepo kule Bulale ndani hawezi kujua chochote kwamba hatujakopa au tumekopa au hatuna hela; atakachojua yeye Serikali wamekuwa wazembe hawawezi kufanya kazi. Kwa hiyo, ni lazima tukubali kwamba Serikali ni lazima iingie kwenye mikopo ilete fedha itekeleze miradi mikubwa ya maji halafu mambo mengine haya yanaweza yakaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tuna Mheshimiwa Aweso hapa ni Mkemia. Jana Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru, alieleza vizuri sana kuhusu ubora na namna ambavyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimetoa matunda bora ukiwemo wewe. Hivi kama Mwalimu asingeamua kukopa kujenga Chuo cha Dar es Salaam, tungekuwa nacho Chuo cha Dar es Salaam, leo?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukope kwa tija na hivi ndivyo Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyofanya. Mradi wa Butimba wamekopa, umejengwa na umekamilika. Wananchi tunaanza ku-enjoy maji haya na miradi mingine tusiogope kwa sababu kwa kufanya hivyo ndivyo tutakavyotatua kero za wananchi. Nikuhakikishie nikimalizia mambo yote haya kwa wananchi ni maji, maji, maji. Ahsante sana. (Makofi)