Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu, Wizara ya Maji inayoongozwa na ndugu yangu kaka yangu Mheshimiwa Aweso.
Mheshimiwa Spika, tumesikia hapa kwenye salamu za kutambulisha wageni wametambulisha uwepo wa wananchi wa Pangani pamoja na viongozi wetu wa Chama. Mawazo yangu ni kwamba kijana huyu Mheshimiwa Aweso, Waziri wetu wa Maji watu wa Pangani watambue ya kwamba tuna kazi naye sisi kama nchi hapa. Kwa hiyo, waendelee kumpa nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe shukurani za pekee sana kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi kule Handeni tumekuwa na mradi mkubwa mara ya mwisho mwaka 1974. Hiyo ndiyo kusema kwamba miaka 50 imepita, Handeni hatukuwahi kuwa na mradi mkubwa wa maji. Amekuja Mheshimiwa Rais, mama shupavu, mama muungwana na mama anaye elewa shida za wanawake. Ametuletea Handeni fedha za miradi kiasi ambacho tunashindwa hata tuanzie wapi na tumalizie wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumepata shilingi 1,248,000,000 Mradi wa Kweinkambala ambao unapeleka maji kwenye mitaa yote mitano ya Kata ya Kweinkambala. Tumepata shilingi milioni 261 Kata ya Kwamagome, tumepata shilingi milioni 320 Kata ya Malezi, tumepata mradi wa Mabanda Mankinda shilingi milioni 761. Kana kwamba haitoshi tumepata shilingi bilioni 2.5 ujenzi wa Bwawa la Kweinkambala. Hivi ninavyozungumza, awamu ya tatu ya utoaji wa fedha shilingi milioni 900 zipo kwenye akaunti tunasubiri mvua zimalizike kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi funga kazi ambao Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametupa wana Handeni, mradi mkombozi kwa shida hii ya maji ambayo tumekuwa nayo kwa miaka karibia 50 ni Mradi wa HTM (mradi wa Miji 28 shilingi bilioni 171).
Mheshimiwa Spika, mradi huu ni mradi wa Kitaifa. Tunajenga dakio la maji pale Mswaha, tutayasukuma maji kwa pump mpaka pale Tabora ambapo tutajenga treatment plant. Tutayatoa maji pale kwa gravity mpaka Kwamatuku, yakitoka Kwamatuku yatasukumwa kwenda Sindeni, yakitoka Sindeni yatasukumwa mpaka Mlima Mhandeni, mlima ambao panajengwa tenki kubwa la milioni mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi wana Handeni Mheshimiwa Waziri, ninaomba uelewe hili na ulichukue; tumekubaliana kwa pamoja kwenye mkutano wa hadhara tenki lile juu ya Mlima Mhandeni litaitwa Tenki la Ukombozi. Kwa hiyo, kwenye kumbukumbu zenu, kwenye takwimu zenu na maandishi yenu ya Wizara wakabadilishe badala ya kuliita Tenki la Vibaoni liitwe Tenki la Ukombozi. Ina maana kubwa sana hiyo. Mheshimiwa Rais, anakwenda kuwakomboa wananchi wa Handeni kutoka dhiki hiyo ya maji ambayo tumeipata kwa miaka mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maji yatatiririka kutoka Mlima Mhandeni mpaka Kwedizando kule Kwediyamba, maji yatatiririka kutoka Mlima Mhandeni mpaka Bangu kule Kideleko, maji yatatiririka mpaka Kulukole kule Malezi kutoka Mlima Mhandeni. Kazi ya Mheshimiwa Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hiyo. Maji yatatiririka mpaka Lusanga, maji yatakwenda mpaka Kulukole, maji yatakwenda Komoza na maji yatakwenda kila kona ya Jimbo la Handeni Mjini kutoka Mlima Mhandeni. Ndiyo maana tunasema tenki lile liitwe Tenki la Ukombozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo mambo machache ambayo lazima tuyafanye kuboresha mradi wetu na kuufanya uende kwa haraka. Mradi huu wa HTM umekuwa designed kukamilika miaka miwili na miezi nane. Tumeshafanya kikao cha kwanza na Mkandarasi, tumekubalina kwamba, atafupisha muda na mradi ule ukamilike walau mwezi Machi, mwakani. Ombi langu kwako Mheshimiwa Waziri, tutakapomaliza Bunge hili, kwa sababu wewe ni kijana wetu wa nyumbani twende tukakae na Mkandarasi tuhakikishe kwamba, mradi huu unakamilika mapema, kwa sababu fedha zipo na ni kazi tu ya kugawanya zile kandarasi ili washambulie wajenge kwa mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukakamilishe distribution design kwenye Kata zote 12 na ikaanze mapema kwa sasa, kwa sababu fedha zipo tusingoje muda. Distribution design ifanyike ili tujue wapi mabomba yanapita yale ya usambazaji. Vilevile, kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza siku zote tukafanye soft part engineering design ya ule mradi wetu. Ni muhimu sana Mto Ruvu - Korogwe ambao ndiyo tunachukulia maji tukaulinde. Tukalinde mazingira, tukalinde vyanzo kwa kufanya hii kazi ambayo nimeisema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kwamba pale Handeni tunao mradi wa Kitaifa wa Msomera, mradi ambao tumewapokea wenzetu kutoka Ngorongoro na tunaishi nao kule Handeni. Kwa kuongezeka kwa Mradi wa Msomera na kwa sababu Handeni tayari ina halmashauri mbili, watendaji wetu wanazidiwa. Tuhaitaji tuongezewe watendaji na vitendeakazi kama magari ili waweze kufanya kazi kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile HTM ile ya zamani twendeni tukaikarabati. Tusiiache ikawa mfu ili tuwe na alternative sources na alternative distributions. Twendeni tukaikarabati HTM ya zamani baada ya kuwa tumeshakamilisha mradi huu mpya tunaoendelea kuujenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi Mkoa wa Tanga tumekubaliana kwamba mwaka 2025 kura zote za Mkoa wa Tanga zinakwenda kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na sababu tunazo. Nitawatajia miradi michache iliyopo ndani ya Mkoa wetu wa Tanga. Mradi wa Maji wa Mkinga Holoholo shilingi bilioni 35, Mradi wa Maji Dibuluma Songe Kilindi shilingi bilioni 22, uboreshaji wa mradi kwenye Jiji la Tanga kwa dada yangu Mheshimiwa Ummy shilingi milioni 516, uboreshaji wa maji huko Mheshimiwa Waziri anakotokea shilingi bilioni moja, uboreshaji wa maji kwenye Mji wa Muheza ambako Mheshimiwa Mwana FA ndugu yangu Naibu Waziri anapotokea shilingi milioni 700. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya ninayoyataja ndiyo yanafanya mwaka 2025 watu wasihangaike. Kura za wana-Tanga zitakwenda kwa Mheshimwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)