Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, na mimi nashukuru kwa kupata nafasi lakini nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri anayofanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika ajenda yake ya kumtua mama mdoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ya sifa kubwa ambayo Mheshimiwa Aweso amejaliwa ni usikivu, niliposimama hapa mwaka jana kuchangia bajeti ya maji, nilizungumza umuhimu wa Wizara kuangalia namna gani ambavyo wataongeza bajeti ili waweze kukarabati miundombinu ya maji ambayo imechakaa. Nikatolea mfano wa Maeneo ya Mwenge Ichenjeze ambayo yanapatikana kwenye Mkoa wangu wa Songwe. Miundombinu ilikuwa ni mibovu lakini leo nimesimama hapa kumshukuru sana Mheshimiwa Aweso, ametuletea fedha bilioni moja 1.7 na sasa hivi mabomba yanatandazwa, ukienda kule Mloho na Vwawa, wananchi wanapata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Aweso, tulimshauri kuhusu mita zile za malipo ya kabla, jambo hili lilikuwa ni muhimu sana, wananchi walikuwa wanateseka kwa kubambikiziwa bili za maji. Leo sisi ni mashahidi, Mheshimiwa Aweso ameshaanza kulifanyia kazi na kwenye taarifa yake amesema kwamba ameanza kwenye mikoa mitano ukiwepo Mkoa Tanga, Arusha pamoja na mikoa mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kitu kimoja, katika mchakato huo nimevutiwa zaidi na namna ulivyotoa nafasi kwa wataalam wetu wa ndani. Umeondoa ile kasumba kwamba kila kitu lazima tuagize nje. Mita hizo umezinunua humu humu ndani, zinazotengenezwa na wataalam wetu wa ndani katika vyuo vyetu, nikupongeze sana kwa hilo. Niombe vilevile taasisi zingine ziweze kuiga mfano huo ambalo ni jambo jema, kwa sababu kwanza linasaidia kukuza ujuzi ndani ya nchi yetu na kulinda thamani ya fedha ambazo tunazo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee zaidi nampongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi Wanawake wa Mkoa wa Songwe tunasema kwamba ndiye balozi namba moja wa Ajenda ya Kumtua Ndoo Mwanamke Kichwani. Katika kipindi chake tumeshuhudia mapinduzi makubwa katika sekta ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii Mikoa yote ya Tanzania imepata mitambo ya kuchimba maji lakini sisi kwenye Mkoa wetu wa Songwe mtambo ule haujafika ukakaa tu, tunavyoongea sasa hivi tumeshachimba visima 65 ndani ya Mkoa wa Songwe, hili ni jambo jema, nimuombe Meneja wetu wa RUWASA, ameenda kwenye wilaya zote tatu, bado Wilaya moja ya Ileje, naamini kwamba atafika ili wananchi waweze kuondokana na kero ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu ameona kwamba haitoshi kwenye bajeti hii ametoa visima 900 kwenye majimbo yote 180. Hili ni jambo ambalo ni kubwa sana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu anatekeleza kwa vitendo ajenda yake ya kumtua ndoo mwanamke kichwani. Sisi Wanawake wa Mkoa wa Songwe tuko pamoja naye na tunamuunga mkono sana. Tunasema kwamba mwaka 2025 kura zote ni kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tuna changamoto kubwa kwenye nchi yetu, kwamba fedha za miradi zinapelekwa lakini ukiangalia tija ya hizo fedha haionekani. Ndani ya miaka michache ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeshuhudia mapinduzi makubwa ya usimamizi wa fedha za miradi na World Bank wamekuwa ni mashahidi, wameonyesha namna gani ambavyo Tanzania sasa hivi tuko vizuri kwenye kusimamia fedha za miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi namuomba Mheshimiwa Waziri kitu kiimoja, umesema kwenye taarifa yako kwamba, kwa fedha hizo sasa mikoa imeongezeka kutoka mikoa 17 mpaka mikoa 25 na Mkoa wa Songwe uko ndani. Mimi naomba, tumekuwa tukisema miaka yote kwamba, ndani ya Mkoa wa Songwe, tunaishukuru sana Wizara tumepata miradi mingi lakini bado tulikuwa hatujapata miradi ya kimkakati. Tunao mradi wa kutoa maji Tunduma kwenda kuyasambaza kwenye Miji ya Mbozi, Tunduma, Vawa pamoja na Mji wa Mlowo, ni miji ambayo ina changamoto kubwa sana ya maji; Mheshimiwa Waziri tunaomba utusaidie kwa sababu mkandarasi ameshapatikana tunaomba sasa fedha hizo zije, mradi huo uweze kutekelezwa na usainiwe ndani ya Mkoa wa Songwe kama ambavyo juzi mmekuja kusaini ule mradi wa mafumbo ndani ya Wilaya ya Mbozi, Mheshimiwa Waziri, tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala lingine ambalo ni muhimu sana, tunasema kwamba tunapozungumzia mafanikio yote ya Wizara ya Maji, hatuwezi kusahau kuwapongeza watu wa RUWASA, kwa kweli wanafanya kazi sana. Meneja wetu wa RUWASA Mkoa wa Songwe, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri, tunasema kwamba unapomkamua ng’ombe maziwa ukumbuke vilevile kumlisha. Mimi nikuombe, mwaka jana nilisimama nikaongea, Mkoa wa Songwe mpaka sasa hivi hatuna gari la maji, tuna gari moja tu, yaani hilo gari anatumia Meneja wa RUWASA, wanatumia ma-engineers wa wilaya, hilo gari linaenda site na hilo gari linakuja Dodoma, hivi sasa leo yuko Dodoma, maana yake kule Songwe hakuna gari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso ni msikivu lakini kwa hili naomba awe msikivu zaidi, utupatie magari ya kutosha ndani ya Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, hukusu suala la maslahi ya watumishi, watumishi hawa wa RUWASA tangia walivyohamishwa kule kwenye halmashauri kwa kweli maslahi yao bado hayajaboreshwa. Wengine wa taasisi nyingine maslahi yao yaliboreshwa lakini hawa bado mpaka sasa hivi maslahi yao ni duni. Mheshimiwa Waziri, changamoto ni nini? Kama suala la kuthibitisha, tunaomba wathibitishwe ili maslahi yao yaweze kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu ni suala la ofis, juzi nilienda kumtembelea Meneja wa RUWASA, kwa kweli nilisikitika sana, amejibanza tu kwenye kachumba kamoja tu pale kwenye ofisi ya wilaya, hakuna ofisi kabisa. Ukimuona hapa Dodoma amevaa suti lakini hana ofisi, kwa hiyo, mimi naomba ujenge ofisi ili watu hawa wanavyofanya kazi nzuri, wafanye kazi kwenye mazingira ambayo ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye Wilaya ya Momba pamoja na Songwe hawana ofisi. Naomba sana waweze kupatiwa ofisi, ahsante sana. (Makofi)