Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote, hongereni sana. Wanasema “Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.” Mimi nakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu umefanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukianzia mkoani kwetu sisi, kwa kweli tumepata maji na kuna miradi ambayo inaendelea, ambayo wanakijiji walikuwa hawajawahi kuwa na maji lakini sasa hivi wanaanza kupata maji safi na salama, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna vijiji ambavyo vilikuwa havijapata maji lakini miradi imekamilika na vingine ambavyo sasa hivi inaenda kukamilika. Kwa mifano, kuna vijiji vya Itagutwa, Nyamlenge, Wangama, Idodi, Ufyambe, Izazi, Makatapola, Magulilwa, Nabula, Kilambo, Mlanda na vingine vingi. Kwa kweli kazi kuwa imefanyika, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri katika Wizara yake kuna ile Program ya P4R, wameshika nafasi ya kwanza kwa nchi 50, si kitu kirahisi, ni kitu ambacho ni sifa kwa nchi yetu na kinatuletea sifa kubwa sana. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo wametuletea pesa ambayo itasaidia kupeleka maji katika vijiji vile ambavyo havikutajwa katika taarifa yako. Kwa hiyo, ni mategemeo yangu sasa vile vijiji ambavyo tunavitaka vipate maji, vitapata maji tena. Sisi tuna vijiji vingi kwetu, ningevitaja lakini kuna vijiji vingi ambavyo vipo vinatakiwa kupata maji, nitakuletea kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kwa kuzungumzia madeni. Kumekuwa na changamoto kubwa saba ya taasisi za umma na mashirika mbalimbali kutokulipa maji katika mamlaka zetu. Hii inasababisha mamlaka kushindwa ufanya kazi yake ipasavyo, tunaona hivyo wakati Serikali ikiwa na sisi kama Bunge tukiwatengea OC humu ndani lakini hawpeleki hizo fedha kwa Mamlaka ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninaomba na ninatoa ushauri, ninaomba Wizara muende mfuatilie fedha hizo, lakini mna mradi wa zile prepaid meters. Ninaomba muende mkafunge hizo prepaid meters kwenye hizo taasisi na hayo mashirika ambayo hayawalipi pesa. Mkianza nao hizo pesa zitapatikana na tutaweza kuangalia Mamlaka yetu ya Maji itapata fedha. Kwa hiyo, mimi huo ni ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, prepaid meters zianze kwenye taasisi hasa zile zenye madeni makubwa. Tunasoma taarifa za CAG, Taarifa za Kamati ya PIC, LAAC na PAC zote zinazungumza madeni makubwa ya Taasisi za Serikali. Sasa kama tunawatengea pesa hapa na hawawalipi mamlaka, mkafunge prepaid meters tuone watafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la upotevu wa maji, kumekuwa na upotevu mkubwa wa maji katika maeneo mengi tunayoishi. Maji yamekuwa yakipotea na tumekuwa tukitoa taarifa, wakati mwingine hakuna majibu ya haraka. Kwa hiyo, unakuta kwamba tunaona Serikali inapoteza Serikali inapoteza maji mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mmesema mna system ya ku-detect upotevu wa maji, lakini hata kama mna system ya ku-detect upotevu wa maji, wakati mwingine tumekuwa tukiona maji yanatiririka bila kudhibitiwa, sasa hapo inakuwaje, mnaona halafu ham-respond tu kwenda kufanya hivyo?

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo huwa napita, karibu na Nzuguni kuna eneo ambalo karibu mwezi mzima maji yametengeneza kama bwawa hapa Dodoma. Kuna maeneo ya Ilazo maji yanamwagika lakini hatuoni ile response ya wafanyakazi kwenda kufanya hivyo. Kwa hiyo, ushauri wangu mimi kila wakati muwe mnapanga program ya kwenda kuangalia jinsi mabomba mabomba yanavyoendelea hata kama mmeweka leo, TARURA inaweza ikaja ikatengeneza barabara wakafukua wakaharibu muundombinu. Kwa hiyo, mtengeneze hiyo regular monitoring and evaluation ya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, kuna suala la uboreshaji wa huduma za maji wenzangu wamezungumza, tumekuwa na changamoto ya maji vijijini. Pamoja na zile asilimia mlizoweka kwamba mmefikia asilimia 79.6 lakini bado kuna changamoto ya maji vijijini kwa asilimia kubwa. Tunaona kwamba tulitoa ile shilingi 50 kwenda 100 lakini ile 50, asilimia 88 inatakiwa igawanywe kwa ile 50. Igawanywe kwa mabonde, maji vijijini na maji mjini lakini hakuna kiwango kinachosema, mijini wapewe maji asilimia hii, vijijini wapewe maji asilimia hii na mabonde wapewe asilimia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nina ushauri, katika ile 50 kwenda 100, asilimia 60 wapewe RUWASA. Ambao ndiyo wanaoweza kutoa maji kwa wananchi vijijini. Hizi 20 wapewe mabonde na 20nyingine wapewe mijini kwa sababu mmeshafikisha asilimia 90 ambayo karibu mnamaliza. Hii itasaidia Watanzania wengi hasa wa vijijini waweze kupata maji. Mkiwapangia, Mheshimiwa Lucy alivyosema hapa kama wanavyofanya wenzetu huko TANROADS, unakuta kwamba asilimia 70 wanapewa TANROADS na asilimia 30 wanapewa TARURA; na huko muwawekee kiwango ili waweze kujua ni kiwango gani ambacho wanatakiwa kukipata wao kama wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sababu kule RUWASA wazawa ndiyo ma-engineer wetu, wakandarasi wetu, sasa hawa wakandarasi hamuwalipi pesa, wana raise certificate kuanzia miezi sita mpaka miaka miwili hawapati pesa hata kidogo kwa sababu wao hawadai interest, lakini makampuni mengine ya nje wanadai interest mnawalipa. Sasa mnawaonea hawa wazawa. muwape pesa na ndiyo maana tunaangalia katika bajeti asilimia ya pesa za maendeleo hazi…(Makofi)

(Hapa Kengele Ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kunti, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, katika fedha za maendeleo, hamjapewa hizo pesa. Tunaomba Serikali itoe fedha ili muweze kupeleka vijijini, ahsante sana. (Makofi)