Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji. Naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, pamoja na timu nzima ya Wizara yake kwa namna ambavyo wametuheshimisha katika majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepunguza changamoto kwa kiasi kikubwa sana, leo sisi Wana-Lindi tuna maji mengi ya kutosha kwa hiyo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Jumaa Aweso. Mheshimiwa Rais anakutegemea sana kwa sababu, umekuwa msaidizi mwema wa kutusogeza mbele kuhakikisha kwamba, Watanzania tunaendelea kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa ukweli kabisa kwamba, katika miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania changamoto kubwa ya maji imepungua katika maeneo yetu kwa zaidi ya 60%. Pale Lindi Manispaa wakati naanza kuwa Mbunge tulikuwa na changamoto kubwa ya maji. Ilikuwa ni kazi kubwa kuomba kura na tukaaminiwa na wananchi, lakini leo maji yako mengi ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haki ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, kuendelea kumtia moyo na kuhakikisha kwamba 2025/2030 kazi iendelee. Katika eneo la Manispaa ya Lindi tuna miradi ambayo tulitakiwa tuitekeleze katika kipindi cha Mwaka huu wa 2023/2024. Sasa tumebakiwa na robo moja ya kutekeleza miradi hii kufikia mwaka mpya wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Jumaa Aweso, tuna Mradi wa Upanuzi wa Maji wa Hangaza Sekondari ambao tumeshajenga tanki. Mradi ule ulikuwa wa gharama ya shilingi 1,100,000,000 fedha ambazo zimetoka ni shilingi 400,000,000 na fedha ambazo zimebaki ni shilingi 731,000,000. Mheshimiwa Jumaa Aweso nakuomba sana uhakikishe kwamba, tunapata fedha hizi, ili kufanya mtandao wa maji uweze kuwafikia wananchi na waendelee kupata huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuna Mradi wa Maji Mkundi. Nikisema Mkundi, imesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, inawezekana majina ya maeneo yanafanana, lakini Mkundi ambayo ninaizungumzia Mheshimiwa Jumaa Aweso ni upande wa pili wa bahari ambako na wewe umeshawahi kufika. Tulitengewa fedha kiasi cha shilingi 934,000,000 pale wananchi hawajawahi kuona maji ya bomba, katika Mwaka huu wa Fedha kati ya kiasi hiki cha shilingi 934,000,000 tulizotengewa hatujaletewa hata shilingi moja. Tunakuomba utupatie fedha, ili twende kutekeleza mradi huu wa maji kwa sababu, matanki yapo, bado kwenda kuendelea kusambaza mtandao wa maji, ili kuhakikisha kwamba maji yanawafikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Jumaa Aweso tulikueleza changamoto kubwa ambayo tunayo Lindi Mjini. Maji tunayo ya kutosha, matenki tumejenga kwa gharama kubwa, lakini changamoto tuliyonayo ni juu ya kuyasambaza na kuwasogezea wananchi miundombinu, ili waweze kuvuta maji majumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika eneo hili tuna changamoto kubwa. Mheshimiwa Aweso ulituahidi shilingi 500,000,000 mbele ya Mheshimiwa Rais. Tunaomba utekeleze kabla hujamaliza mwaka huu wa fedha ili kuhakikisha kwamba, wananchi wa Lindi wanasogezewa maji. Shilingi 500,000,000 tunataka kuielekeza katika kata ya Ng’apa, Tandangongoro, ambako kuna mradi mkubwa wa maji ambayo ndio tunatumia Wananchi wa Manispaa ya Lindi na mengine tunawapelekea majirani zetu wa Mchinga, lakini wananchi wa Ng’apa wenyewe wanakosa maji kwa sababu, hakuna miundombinu ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuomba sana Mheshimiwa Jumaa Aweso ahakikishe kwamba, anatuongezea shilingi 500,000,000 ili kwenda kusogeza miundombinu ya maji. Tuna wananchi karibu 12,498 pale wanahitaji huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunayo miradi mipya tunashukuru kwamba, tuna Mradi wa Kujenga Tenki Kiduni kwa fedha za Covid-19, shilingi 600,000,000 na mradi umekamilika. Sasa tunataka kuongeza miundombinu ya maji kuhakikisha kwamba, Wananchi wa Ruaha, Mnazi Mmoja, wanapata maji safi na salama. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri utupatie fedha, hizi shilingi 1,229,000,000, ili tuweze kukamilisha wananchi wetu wapate huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna Mradi wa Upanuzi wa Maji kule Kitunda, upande wa pili wa bahari. Tanki tumejenga, lakini bado tunahitiaji kusambaza miundombinu ya maji, ili kuwafikia wananchi wa Kitunda, Mnali na Sinde. Mradi huu una gharama ya shilingi 1,500,000,000, tuna wananchi wengi wanaishi kule hawajawahi kuona maji safi na salama. Wamezoea kuokoteza maji huko mashimoni, mabondeni kwa hiyo, tunamuomba sana Mheshimiwa Jumaa Aweso ahakikishe kwamba, tunapatiwa hizi fedha, ili mambo yetu Lindi Mjini yawe supa. Tuhakikishe kwamba, mwaka huu uchaguzi tunaumaliza salama, mwaka kesho tunaendelea vizuri, tuendelee kurudi tena hapa mjengoni, tuendelee kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha?
MWENYEKITI: Muda umeisha, ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa kutuunganisha Wabunge wote pamoja na Wizara yake. Ushahidi tosha tumeuona kwamba, hata mwenyewe ameweza kuiunganisha familia yake. Tumeona wadada wazuri warembo walikuwa hapa wote wawili hawana mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)