Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya dharura kuhusu kuongezwa kwa umri wa waombaji wa ajira za Serikali

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hoja ya dharura kuhusu kuongezwa kwa umri wa waombaji wa ajira za Serikali

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mbunge makini wa kundi la vijana, mdogo wangu Mheshimiwa Ng’wasi Kamani. Kwanza, naiunga mkono hoja hii kwa sababu mbili au tatu. Kwanza, kwa mujibu wa Sheria ya Ajira (Permanent Employment) inataka kuanzia miaka isiyozidi 45 na siyo 25. Kwa hiyo, tukiangalia kwa mujibu wa sheria yetu tunajichanganya.

Mheshimiwa Spika, pili, kwa mujibu wa taratibu za ajira za kijeshi tumeona maeneo mengi walikuwa wanatafuta vijana ambao wana uzoefu wa ziada kwenye maeneo fulani fulani, wengine wawe wamepitia kwenye majeshi ya mgambo na kadhalika. Sasa kwa mwanafunzi ambaye amehitimu katika mfumo wa moja kwa moja, siyo rahisi kupata hivyo vigezo ambavyo mara nyingi wanapotoa ajira za kijeshi huwa wanavitaka, lakini mwisho wa siku ni ukweli usiopingika kwamba tuna vijana wengi sana wako mtaani wanatafuta ajira.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali, wanapokuwa wanatangaza tena ajira chache namna hii ni vizuri wakapunguza vigezo ambavyo havina ulazima kwa sababu wanakuwa na michakato ya ndani ya kuweza kuwapima na kutafuta wale ambao wanawahitaji. Wakitoa matangazo yenye ubaguzi wanaichonganisha Serikali na wananchi wake na wanatuchonganisha sisi ambao tunawawakilisha na wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja kwamba kigezo cha miaka 25 kipelekwe angalau miaka 30 au 35 ili tuwape nafasi vijana wengi zaidi kuingia kwenye soko hilo la kupigania ajira ambazo zimetangazwa. Ahsante.