Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia kwenye hotuba hii muhimu sana ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai wa kuweza kuwepo leo humu ndani ya Bunge ili kuweza kufanya kazi hii muhimu. La pili, nianzie pale pale alipoishia Mheshimiwa Waitara kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli ambaye haioni sijui tumtafutie jina gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi wa Jimbo la Bukene tunaona kabisa kwamba katika watu ambao wamependelewa ni wananchi wa Jimbo la Bukene. Kabla ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia kuingia madarakani, Jimbo langu la Bukene lilikuwa linapata fedha za maendeleo kwa mwaka takribani shilingi bilioni 28. Baada ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia kuingia madarakani fedha za maendeleo kwenye Jimbo langu la Bukene zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 28 sasa hivi napata shilingi bilioni 78 kwa mwaka. Kwa hiyo huo ni ushahidi wa wazi wa dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yabkuondoa kero mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kule kwangu kuna miradi ambayo usingetegemea kuona inafika katika Jimbo la Bukene. Kuna Mradi mkubwa sana wa Kupeleka Maji ya Ziwa Victoria lakini karibu vijiji vyote vina umeme, barabara na kila sekta kama vile elimu na afya. Kwa hiyo sisi tulishatoa tamko kwamba 2025 Jimbo la Bukene chakumlipa pekee Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba anapata kura nyingi sana za kishindo na za kumwaga kutoka Jimbo la Bukene. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sana timu ya TAMISEMI kwa dhati ya moyo wangu, kuanzia Mheshimiwa Waziri, Mchengerwa; Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Dugange na Mheshimiwa Katimba; Katibu Mkuu Ndugu Ndunguru; Manaibu Makatibu Wakuu wote wa TAMISEMI Ndugu Msonde, Mtwale, Mativila na Willson Charles, kwa usikivu wao na jinsi ambavyo wana-respond unapokwenda ofisini kwao kwa ajili ya matatizo mbalimbali. Niseme tu kweli timu ya TAMISEMI imekamilika na inafanya kazi ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo kadhaa ya kuzungumzia kwenye Wizara hii, nianze na suala la maboma. Maboma ya shule za msingi, maboma ya sekondari, maboma ya zahanati ambayo wananchi walitumia nguvu zao wakayakamilisha na sasa yanasubiri kumaliziwa. Shida iliyopo ni kwamba mwitikio wa wananchi ulikuwa ni mkubwa sana na maboma ambayo yapo tayari yanasubiri kukamilishwa ni mengi sana. Katika Jimbo langu la Bukene pekee nina maboma 61 kwenye vijiji 43 ambayo yanasubiri kukamilishwa. Tulifanya tathmini sisi Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, kwenye jimbo langu pekee hayo maboma 61 yaliyopo kwenye vijiji 43 ili yakamilike yanahitaji shilingi 2,800,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi ni nyingi mno huwezi kuzipata kutoka bajeti ya ndani ya halmashauri. Sisi Halmashauri yetu ya Nzega hiyo shilingi bilioni 2.8 ndiyo karibu mapato ya mwaka mzima. Sasa hatuwezi kutumia mapato ya mwaka mzima kukamilisha maboma kwa sababu tuna vipaumbele vingi na mambo mengine mengi ya kutekeleza. Kwa hiyo ushauri wangu hapa ni lazima TAMISEMI iwe na intervention ya makusudi kabisa ya kutafuta fedha Serikali Kuu kwa ajili ya kukamilisha haya maboma ili tufufue ari ya wananchi. Wananchi ambao walichanga na kujenga haya maboma, sasa hivi ukiwaendea kwa ajili ya mchango mwingine wanakuuliza mbona tuliyochanga hayajakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo TAMISEMI wasaidie hili kupata fedha maalum. Kwangu tu ni shilingi bilioni 2.8 sasa ukiangalia majimbo yote kwa kweli utaona kwamba fedha za mapato ya ndani haziwezi zikamaliza haya maboma ambayo ni muhimu tuyamalize ili tufufue ari ya wananchi katika kuchangia maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la afya. Katika Bunge hili mwaka wa fedha huu ambao tumebakiza miezi miwili na nusu kuumaliza, TAMISEMI kupitia Naibu Waziri alipokuwa anajibu swali langu iliahidi kutupatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kipya katika Kata ya Igusule, kwa sababu kata hii sasa ina mradi mkubwa wa kielelezo ule wa Coating Yard ya bomba la mafuta ambao Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko juzi tulikwenda naye kuzindua pale na kata hii sasa ina muingiliano wa watu wengi. Serikali ilikubali tujenge kituo cha afya pale na bajeti hii ambayo bado miezi miwili, Serikali ikaahidi kutupa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kazi hiyo. Sasa leo hii tumebakiza miezi miwili na nusu hizo milioni 500 bado hazijafika Nzega.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Igusule walitoa eneo ambalo linatosha, likakaguliwa nadhani na mkurugenzi akawa ameshajulisha TAMISEMI, lakini mpaka leo, hiyo shilingi milioni 500 haijapatikana. Kwa hiyo nichukue fursa hii kuiomba TAMISEMI katika miezi miwili na nusu iliyobaki, hiyo shilingi milioni 500 tuliyoahidiwa kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Igusule, basi iweze kupatikana ili Serikali iweze kutimiza ahadi yake na wananchi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali, pale Kituo cha Afya cha Itobo wametupatia shilingi milioni 180 na mchakato wa kununua X-ray machine umeshaanza na almost unakamilika ili tuweze kupata huduma muhimu ya X-ray pale. Nafahamu tulikuwa na shida pia ya mashine ya kufulia ile tuliyopewa miaka ya nyuma ilishindwa kufanya kazi kabisa, lakini kuna mashine mpya ambayo tayari ipo pale na muda wowote ule inaanza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni TARURA, imefanya kazi kubwa kwa barabara za vijijini. Hivi karibuni tumeshuhudia mvua na Jimbo langu pia pamoja na kwamba mvua ni baraka na inatuhakikishia tutavuna mpunga mwingi, baadhi ya barabara zimekatika na maji ya mvua. Barabara zetu ni za vumbi za changarawe, kwa hiyo, kunapokuwa na mvua kubwa zinakatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba zile fedha za dharura ili TARURA ziweze kupelekwa kwenye maeneo yetu na ziweze kufanya kazi ya kutengeneza barabara ambazo zimekatwa na kuharibiwa na mvua kubwa. Nina Barabara ya Mambali – Chambo, Barabara ya Mogwa – Luhumbwe na Barabara ya Kasela- Mwamala zimekatika na nyingine nyingi tu ambazo sasa hazipitiki kutoka na mvua kubwa. Kwa hiyo, niombe zile fedha za dharura kwa ajili ya kushughulikia barabara hizi kuzirudisha kwenye hali yake ya kawaida ziweze kupatikana ili barabara ziweze kutengenezwa na wananchi waweze kuzitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nashukuru sana kwa ushirikiano ambao tunapewa na Serikali ya Mkoa sisi kama Waheshimiwa Wabunge na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais ambaye amemteua Mkuu wa Mkoa mpya. Nichukue fursa hii kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumkaribisha sana Tabora, ndugu yetu Chacha Matiko, ambaye ni mchapakazi na mfanyakazi mzuri. Kwa muda mfupi tu ameshakaa na Waheshimiwa Wabunge, tumeelezana vipaumbele (priorities) za Mkoa wa Tabora, kwa kweli tunayo matumaini makubwa sana kwamba ataendeleza kazi nzuri sana iliyofanywa na Dkt. Batilda Buriani ambaye amehamishiwa Mkoa wa Tanga. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, muda wako umekwisha, kengele ya pili hiyo.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, namkaribisha sana Ndugu yangu Matiko katika Mkoa wa Tabora, Waheshimiwa Wabunge wote tutampa ushirikiano mkubwa. Nashukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)