Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Amandus Julius Chinguile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uhai na hatimaye kupata nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nitoe pole kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi, kwa mafuriko yaliyotukuta hususani kwenye Jimbo langu la Nachingwea. Madhara yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ni makubwa kwenye Jimbo langu la Nachingwea na niendelee kuwapa pole kwenye maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nitoe pole kwa wananchi waliovamiwa na wanyama wakali (ndovu) na hasa kwenye Kata ya Mkoka, Kipara Mnero, Namapwia, Nditi, Ngunichile, Mbondo, Kilimarondo pamoja na Matekwe. Tunajua kwamba Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini na tunaamini kwamba tutapata suluhu ya kudumu kwenye kadhia hii ambayo wananchi wa Jimbo langu la Nachingwea tunapitia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kujielekeza kwanza kwenye maboma. Kazi kubwa imefanyika sana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais, wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiyo maana tunaendelea kumpongeza na kuendelea kusema kwamba, ameendelea kuupiga mwingi. Wakati wenzangu wanasema na kusifia kwamba, Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi, hata sisi kule Nachingwea ameupiga mwingi. Pia kule tumeshakubaliana mwakani hana sababu hata ya kuja kwenye kampeni sisi tayari tumeshajipanga kura zote kwa Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika kwenye Hospitali yetu ya Wilaya ya Nachingwea utadhani ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa sasa. Majengo mapya yameendelea kujengwa, kizuri zaidi tumepata ICU mpya ya kisasa ya Kimataifa, ipo Nachingwea, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Siyo hivyo tu Mheshimiwa Rais wakati anaingia madarakani tulikuwa na kituo cha afya kimoja, sasa hivi tunavyo vituo vya afya vitano. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hiyo kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anaendelea kuifanya, naiomba sana Wizara kwenye eneo hili la maboma tuweke mpango mkakati wa kuhakikisha tunakwenda kukamilisha maboma ambayo wananchi wamejitokeza na kuyajenga. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Nachingwea kuna maboma 93 na vituo vya afya ni vitatu, kuna Kituo cha Afya cha Kassim Majaliwa, kipo kwenye Kata ya Chiola, pia kuna Kituo cha Afya Namapwia na Kituo cha Afya Maili Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ikitukamilishia hivi vituo, maana yake mpaka mwisho wa mwaka tutakuwa tunazungumzia habari ya vituo vya afya zaidi ya 10. Maana yake ongezeko la vituo tisa zaidi kwenye utawala wa Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwenye maboma ya shule za msingi, kwenye Jimbo langu la Nachingwea 70%, ya majengo ya shule za msingi ni chakavu sana. Ukienda kwenye Kata ya Kilimarondo hiyo shule huwezi kijificha wakati mvua inanyesha, utafikiri kama huko juu hilo bati limetobolewa na misumari, kila sehemu inavuja. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara kwenye maeneo kama haya watusaidie kupata shule mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili siyo eneo la kukarabati jengo moja, ni kutuletea shule kwa sababu hii shule ni ya zamani, hii shule imejengwa enzi za wakoloni. Kwa hiyo, watusaidie kupata shule mpya kwenye maeneo haya ambayo kwa kweli hali yake ni ngumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hiyo tu kwenye eneo la Ninjihi, Kata ya Kilimarondo nayo shule ya msingi huko hali ni ngumu. Hali ni ngumu kwenye maeneo hayo, kwa sababu kazi kubwa imefanyika kwenye eneo la shule za sekondari, niiombe sana Wizara sasa pamoja na maeneo mengine shule za msingi kwenye halmashauri yangu kwenye Jimbo la Nachingwea ni ngumu. Kwa hiyo, tunaomba usaidizi zaidi ili kwenye eneo hilo na sisi tuweze kufaidika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuzungumzia habari ya TARURA na kwenye eneo hili kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TARURA Engineer Victor Seff, anafanya kazi kubwa na nzuri sana. Pia, Mkurugenzi wa Barabara Engineer Komba wanafanya kazi kubwa na nzuri kwenye kila kona ya Tanzania kuhakikisha kwamba, barabara zetu za TARURA zinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, kwa hiyo, tumeendelea kukagua barabara za TARURA karibu kila kona ya Tanzania. Kazi inayofanyika huko ni kubwa na nzuri. Kwenye eneo hili sasa ombi langu kwa Serikali tuwaongeze fedha TARURA ili waweze kufanya kazi kubwa na nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti hii ambayo tunakwenda nayo sasa kiwango cha upelekaji wa fedha kwenye eneo hili la TARURA siyo kzuri sana. Niiombe sasa Serikali ipeleke hela zile ambazo tulipitisha hapa ndani ya Bunge ili wenzetu wa TARURA waendelee kufanya kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashuri ya Wilaya ya Nachingwea ni kati ya majimbo kongwe Tanzania na tuliachwa sana nyuma kimaendeleo, kwa sababu ya namna ambavyo historia ya nchi yetu ipo na hiyo sina sababu ya kusema, Serikali inajua. Sasa ni wakati wa kuendelea kuiangalia kwa macho yote mawili, Jimbo la Nachingwea ili na sisi tuweze kukimbia kama wenzetu kwenye maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna uchakavu kwenye soko, soko lililopo kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Nachingwea ni la kizamani sana na namna ambavyo lilikuwa limekidhi wakati huo. Sasa hivi watu wameendelea kuwa wengi sana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea. Tayari timu ya Mkurugenzi ilishatoa maandiko kupeleka TAMISEMI, kwa hiyo niombe sana wenzetu wa TAMISEMI kati ya miradi mkakati ambayo watufikirie wenzao wa Nachingwea, ni soko hili la kisasa ambalo kimsingi litaenda kutusaidia hata kuwa chanzo cha mapato katika Halmashauri yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye upungufu wa watumishi. Tunajua kwamba Serikali imeendelea kuajiri na kutoa vibali kwa ajili ya kuajiri, tuendelee kuhakikisha majengo haya mazuri ambayo tumeendelea kuyajenga kwenye sekta ya elimu na sekta ya afya, tuendelee kutoa watumishi wa kutosha ili waende wakafanye kazi sasa kwenye majengo haya ambayo Mheshimiwa Rais ameendelea kuyajenga kila uchwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye eneo langu Maafisa Maendeleo Wasaidizi, mahitaji ni 36, waliopo ni wawili. Hatuwezi kwenda kwa namna hiyo, upungufu ni 34, haiwezekani! Tunaiomba sana Serikali ione namna ya kuendelea kutuwezesha kwa kutupatia hawa watumishi ili waweze kutusaidia kimaendeleo kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watendaji wa Kata, mahitaji ni 36, waliopo ni 30, maana yake kuna Kata sita hazina Watendaji wa Kata. Nani anaratibu huko maendeleo? Sasa hicho ni kizungumkuti kingine, watusaidie ili hawa wataalamu waendelee kutusaidia kujiletea maendeleo kule kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watendaji wa Vijiji, mahitaji ni 127, waliopo ni 106, upungufu ni 21. Kwenye maeneo haya maana yake wanaofanya kazi, aidha ni Kaimu Mtendaji au Wenyeviti wetu wa Vijiji, wanafanya kazi ambazo zenyewe zinahitaji utaalamu. Kwa hiyo, kwa namna hii maeneo ya vijiji hayawezi kwenda vizuri sana kama maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye CSR. Kwenye hili niendelee kuipongeza Serikali, Naibu Waziri hapa akiwa anampa taarifa Mheshimiwa Mbunge mmoja alisema, wamechukua hatua hasa kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza ni kupitia sheria zetu kama zina mianya ya hawa wanaopaswa kutoa CSR kujipangia wenyewe namna ya kutekeleza hii miradi. Tuone namna ya kupitia ili waende sambamba na mipango yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sisi kama darasa tunatakiwa kujenga kwa shilingi milioni 20, haiwezekani darasa hili likajengwa kwa shilingi milioni 40, haiwezekani. Kisa kwa sababu ni mfumo wa CSR, hii haikubaliki.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kumpa taarifa mzungumzaji. Kwa mujibu wa engineering profession hakuna mahali popote inaposemwa ni lazima darasa lijengwe kwa shilingi milioni 20 hakuna mahali popote. Thamani ya jengo lolote linalojengwa inatokana na hali halisi ya sehemu husika. Hakuna standard ya darasa kujengwa kwa shilingi milioni 20 Tanzania nzima, ni hilo tu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Amandus.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei hiyo taarifa kwa sababu hata kama ni variation haiwezi kuwa mara tatu ya ile bei halisi iliyopo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba vituo vya afya tunajenga kwa kiasi gani. Haiwezekani kituo cha afya cha Serikali kinajengwa kwa shilingi milioni 560 pale Nachingwea halafu kwa sababu kimejengwa kwa CSR kijengwe zaidi ya shilingi bilioni moja, haikubaliki. Ndiyo maana tunasema tuone na tupitie sheria zetu kama zina mianya ya wao kujipangia wanavyotaka. Sijasema hapa kwamba darasa linajengwa kwa shilingi milioni 20 kama ambavyo Mheshimiwa mtoa taarifa amesema. Nimesema ni kati ya shilingi milioni 20 na 25. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama inakwenda zaidi ya hapo inaweza ikawa variation, lakini si kwa kiasi hicho.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)