Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nampongeza Waziri wa TAMISEMI kwa kazi nzuri anazozifanya. Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri sana pamoja na Naibu Mawaziri wake. Mheshimiwa Waziri kila Wizara anayopelekwa ana-fit, anafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu wanafanya kazi nzuri sana. Ninawapongeza Mawaziri wote wakiongozwa na jembe Mheshimiwa Jenista Mhagama, wanafanya kazi nzuri sana sana. Wanatembelea wanazunguka Wilaya zote nchi nzima kukagua miradi ya maendeleo, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia Mkuu wangu wa Mkoa Yahya Nawanda kwa kazi nzuri anazozifanya. Anafanya ziara mkoa mzima, anazunguka kijiji kwa kijiji kusikiliza kero na kutatua kero za wananchi. Hongera sana kwa RC wa Simiyu anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais wangu kipenzi Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa Daraja la Busisi Kigongo, sasa limefikia 85%. Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri sana na daraja hilo litafungua uchumi wa Kanda ya Ziwa na nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuboresha Hospitali ya Muhimbili. Inapandikiza figo, inafanya upasuaji wa kichwa na inafanya upasuaji wa moyo. Haya magonjwa wananchi walikuwa wanaenda kutibiwa India, sasa hivi wanatibiwa hapa hapa Tanzania na watu kutoka nchi za nje wanakuja kutibiwa hapa. Hongera sana Mheshimiwa Rais kwa kuupiga mwingi. Mheshimiwa Rais ni nahodha, akanyage twende, asibabaike mtu mzima hatishiwi nyau nyau. Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri, tupo naye bega kwa bega na tutapambana iwe jua iwe mvua, lazima apate ushindi wa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye Mkoa wangu wa Simiyu. Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 440 kwa ajili ya mradi wa maji na mradi huo umeanza. Mradi huo ukifika wananchi wa Simiyu tutanufaika. Tulikuwa na shida sana na maji, tulikuwa kwenye orodha ile ya mikoa tisa ambayo imekaribiwa na ukame, lakini sasa hivi tunajivunia hilo. Mheshimiwa Rais ametoa fedha, mradi huo umeshaanza na ukifika tutalima kilimo cha umwagiliaji. Nani kama Mama Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

WABUNGE FULANI: Hakuna. (Makofi/Kicheko)

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, huyu huyu Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne katika hospitali ya mkoa. Jengo la mama na mtoto zuri ghorofa la kisasa limekamilika, jengo la kufulia limekamilika, jengo la kusafishia vifaa limekamilika, jengo la mochwari limekamilika. Nani kama mama Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

WABUNGE FULANI: Hakuna. (Makofi/Kicheko)

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Itilima ametoa zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na ununuaji wa vifaa tiba. Ombi kwa Wilaya ya Itilima, Hospitali ya Wilaya ya Itilima haina uzio, tunaomba Serikali itujengee uzio. Haina korido za kupitisha wagonjwa, tunaomba Serikali itujengee korido za kupitishia wagonjwa. Vilevile haina nyumba za watumishi wa afya, tunaomba Serikali itujengee nyumba za watumishi wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna Kata ya Nhobora, Kata ya Nhobora ni kubwa ina watu wengi, haina zahanati wala kituo cha afya. Naiomba Serikali ilete pesa itujengee kituo cha afya au zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda Hospitali mpya ya Bariadi DC; Bariadi DC tumepata shilingi bilioni tatu. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais, hospitali ina kila kitu na inafanya kazi, lakini tuna ombi kwa Bariadi. Bariadi kuna Kituo cha Afya Ng’wang’wali na Ngulyati. Tuna upungufu wa nyumba za watumishi na wodi za kulaza wagonjwa. Pia, kwa Bariadi tuna upungufu wa magari ya kubeba wagonjwa. Tunaomba Serikali ituletee magari ya kubebea wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda Busega. Wilaya ya Busega Mheshimiwa Rais ametupatia shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Busega. Tunaiomba Serikali kwa Busega, tuna Kituo cha Afya Kiloleni hakina wodi za kulaza wagonjwa na hakina nyumba za watumishi. Kituo cha Afya Badugu hakina nyumba za kulaza wagonjwa na hakina nyumba za watumishi. Tunaomba Serikali ituletee fedha ili tuweze kujenga hizo nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda Maswa; Hospitali ya Maswa imeboreshwa sana na tunaishukuru Serikali ina wodi zote, ina theater, ina jengo la dharura, nani kama Mama Samia Suluhu Hassan? Ombi kwa Maswa, tuna Vituo vya Afya Maswa, Badi, Shishiyu, Malampaka, Mwabayanda havina jokofu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ibaini vituo vya afya vyote nchi nzima na hospitali za wilaya ambazo hazina jokofu ili ziweze kupeleka, kifaa hiki ni muhimu sana. Naishukuru Serikali, nilisimama mwaka jana hapa nikaomba generator, Hospitali ya Wilaya ya Itilima ilikuwa haina generator na vituo vya afya. Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu, imeleta generator kwenye vituo vya afya na hospitali za wilaya tena mpya za kisasa, hongera sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo niliyotaja ni machache tu, pesa zilizoingia Mkoa wa Simiyu zimeingia kama mvua. Zaidi ya shilingi trilioni moja zimeingia Simiyu kwa ajili ya maendeleo. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mazuri ya kisasa, yana vioo na vigae. Wanafunzi wanaosoma shule hiyo hawatamsahau Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani wanafunzi walikuwa wanaanza kidato cha kwanza kwa awamu, lakini sasa hivi wanaanza pamoja. Namshukuru kwa elimu bila malipo kuanzia kidato cha kwanza mpaka sekondari. Changamoto kubwa ni walimu, tuna upungufu wa walimu. Tunaomba Serikali ituletee walimu. Tunashukuru juzi hapa tumepokea walimu 617, tunashukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda TARURA. Nampongeza Mkurugenzi wa TARURA kwa kazi nzuri anazozifanya. Ni ukweli usiopingika, mama yangu alijenga barabara kila kona kuunganisha kila kijiji. Bahati mbaya ni kitu ambacho huwezi kupinga, mvua, imeharibu barabara. Naiomba Serikali iongeze pesa ilimradi barabara hizo ziweze kujengwa upya tena kwa ajili ya mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza sana na wewe unafanya kazi nzuri sana. Ilala unafanya kazi nzuri sana, namwomba Mungu urudi tena. Nimpongeze na Spika wa Bunge anafanya kazi nzuri sana. Waheshimiwa Wabunge mimi niseme tu kwamba hakuna kama mama. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mpole, mnyenyekevu na ana upendo; asitishwe na mtu yeyote. Sisi tupo bega kwa bega na yeye, tutapambana, tutacheza vizuri na atashinda kwa kishindo. Mama yangu kura atakazozipata 2025 haijawahi kutokea toka dunia iumbwe. Kazi anazozifanya nchi nzima inajua na dunia yote inajua. Hongera sana kwa mama yetu Mungu ambariki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana na naunga mkono hoja. (Makofi)