Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Ofisi hii muhimu sana ambayo inagusa maisha ya wananchi wetu hasa sisi Wabunge wa vijijini. Tunaitegemea sana Ofisi hii kwa mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na cabinet yake yote na Mawaziri wote na wasaidizi wake, kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini bila kumsahau Jemedari wetu, Mheshimiwa Rais wa Nchi yetu kwa jinsi ambavyo anaitendea haki nchi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita zaidi kwenye suala moja kubwa la ugawaji wa maeneo ya kiutawala. Tunapoomba suala hili, maombi kwa ujumla yanakuwa kama mepesi mepesi, lakini sisi wengine katika suala hili la ugawaji wa maeneo ya kuitawala, tunaomba kwa sababu wananchi wetu wanapata tabu sana. Maeneo mengine ya vijijini ni makubwa sana, kiasi kwamba, eneo la kata ni sawa na baadhi ya wilaya katika maeneo mengine. Sasa wananchi wetu wanakosa kupata fursa ya huduma nzuri ambazo Mheshimiwa Rais wetu ametupatia kwa sababu ya umbali na ukubwa wa maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanapata tabu sana kufuata huduma muhimu mahali zilipo ndani ya kata yake tu au ndani ya kijiji chake kwa sababu ya ukubwa wa eneo. Kwa hiyo tunapomwomba Mheshimiwa Waziri na hasa Mheshimiwa Rais kwa sababu hii ndiyo Wizara yake kuhusu kugawa maeneo naomba lichukuliwe kwa umuhimu wa kipekee kabisa. Hii ni kwa sababu nia yetu ni kutaka wananchi wafaidi haya mema ambayo mama yetu ametufanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano tu wa kata yangu moja, Kata ya Mwangeza. Kata hii ukitoka mwisho wa kata kwenye Kijiji kinaitwa Hilamoto ukaenda mpaka mwisho Kijiji kinaitwa Endasiku ni takriban kilometa 70. Sasa watu hapa wana majimbo yao na wilaya zao wanaweza waka-imagine kilometa 70 inamaanisha nini ndani ya kata moja. Kata kama hii kwa mujibu wa sensa hii iliyopita juzi, ina watu 32,520, hiyo ni kata moja. Kata hii ina vijiji sita tu na vitongoji 46. Kwa mfano, ukitoka Kitongoji kinaitwa Midibwi kwenda kupata huduma kwenye makao makuu ya kijiji ni kilometa 24 na hizo kilometa 24 hawezi kwenda straight. Inabidi kwanza atoke aende makao makuu ya kata, kilometa kama 10, halafu kutokea hapo aanze kwenda kijiji kingine kwenye makao makuu ya kijiji chake kilometa nyingine 14. Ndipo anatengeneza 24, kufuata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaposema tugawanyiwe maeneo nataka mpate picha na hii ni mfano wa kata moja. Naamini hata Wabunge wengine katika maeneo yao watakuwa na mfano kama huu. Kwa hiyo tunapoomba watugawanyie tunaomba wachukulie kwa umuhimu. Hebu wafanye reseach, hivi hawa watu wanavyoomba kugawanyiwa maeneo ni nini hasa wanaomba? Hizi shida zetu zinatofautiana, sehemu nyingine zimevuka mipaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hili la kugawa halijafanyika kwa miaka mingi sasa. Sasa hivi tunakwenda kwenye uchaguzi, ina maana kwamba tukipita uchaguzi wa vijiji, vitongoji na mitaa mwaka huu maana yake hiyo ndiyo imetoka moja kwa moja mpaka uchaguzi ujao. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Rais kupitia Waziri wake Mheshimiwa Mchengerwa, ombi hili la ugawaji wa maeneo aliweke katika vipaumbele vyake mama yetu ili wananchi waweze kuyafaidi mambo mazuri aliyotufanyia kwa sababu wanashindwa kuyapata kutokana na umbali. Mtu anaamua tu asiende kupata huduma ya hospitali, ajifungulie nyumbani kwa sababu ya umbali. Kwa hivyo, naomba sana jambo hili lichukuliwe kwa umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kupitia mchango wangu leo, niombe maombi maalum kwa Mheshimiwa Mchengerwa, aifikirie kata hii, tunaomba angalau atugawanyie kata hii na Kata ya Mwangeza ili zitoke kata tatu. Itoke Kata inaitwa Endasiku, makao makuu yake Ikolo na Kata yenyewe ya Mwangeza ibaki, lakini pia itoke Kata nyingine mpya inaitwa Dominiki. Hizi kata tatu angalau sasa zitakuwa na msawazo wa vijiji na atupandishie vijiji. Kuna Kitongoji kinaitwa Matele kina kaya 317, hiki sasa kiwe kijiji. Kuna Kitongoji kinaitwa Mzanga kina kaya 285, hivi ni vitongoji, hapo kuna mwenyekiti wa kitongoji ambaye hana hata mshahara ndiye anayetakiwa ahudumie hizi kaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba haya maombi ayachukue kama maombi maalum tafadhari ili atugawie hii kata katika uchaguzi huu. Angalau akitupandishia na hivi vijiji basi tutakuwa sasa kuna msawazo wa kimaendeleo ambao tunaweza tukaupata kwa wananchi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kata hii ndiyo wanayoishi wale watu wa Hadzabe wale ambao bado wanakula mizizi na matunda porini kule, sasa hebu fikiria na huduma zinakuwa ngumu namna hii. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nimekaa hapo makusudi kabisa, hata muda ukiniishia alichukue hili kama ombi maalum la kuigawa Kata ya Mwangeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna vitongoji vikubwa, kwa mfano, Kitongoji cha Tatazi kiko Kata ya Mpambala, kiwe Kijiji, wameomba kwa muda mrefu. Kitongoji cha Irama kipo Kata ya Kikhonda, kiwe Kijiji; Kitongoji cha Zinzilu na Madada viko Kata ya Ilunda, ni vitongoji vikubwa, yaani ukienda hauamini kama ni kitongoji. Kitongoji cha Mlumba, Kata ya Kinyangiri na Kitongoji cha Nyeri, Kata ya Iguguno. Hivi vikiwa vijiji huduma hizi ambazo mama ametupatia zitafika vizuri na utawala utakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, namwomba Mheshimiwa Waziri, umefika wakati sasa wa kuwafikiria hawa viongozi wanaotuongozea hivi vijiji na hivi vitongoji, kuwe na posho maalum. Najua vijiji na vitongoji 12,000 angalau kuwe na kaposho maalum cha kuwafanya waweze kufanya kazi hizi za kusimamia, wanafanya kazi kubwa sana. Hii miradi mingi, fedha nyingi tunazopeleka huko chini zinasimamiwa na hawa watu na hii inasababisha ndiyo wanajiingiza kwenye migogoro ya ardhi kwa kutoa ardhi hovyohovyo tu na kupata virushwa, hii ni kwa sababu hawana chochote. Naamini kama kutakuwa na kaposho maalum angalau kwa mwezi, hawa Wenyeviti wa Vijiji wataepukana na hii migogoro ya ardhi na watafanya kazi kwa moyo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado niko hapohapo halmashauri, niwaombe ndugu zangu wa TAMISEMI waongee na watu wa Utumishi. Hii kada ya Mtendaji wa Kata kuwa inaajiriwa na Utumishi ufanisi wake umekuwa mdogo, kwa sababu, Utumishi wanapeleka vijana kutoka maeneo mbalimbali kwenda kuwa Watendaji wetu wa Kata. Kuna vijana wengine tangu wanazaliwa yuko pale Kinondoni, anasoma primary Kinondoni, sekondari Kinondoni, vyuo viko Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kabisa anapata ajira ndiyo anapelekwa Mwangeza kule kwetu Kijijini Endasiku akawe Mtendaji wa Kata, kwa mara ya kwanza anaenda kushuhudia watu wanaokunywa maji wanachangia na fisi kwa sababu bado visima havitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii imekuwa kama mlango wa kuingilia tu kupata ajira, baada ya hapo, anaanza process za kuhama na ndiyo maana mpaka leo Kata nyingi zina Makaimu, Makaimu, Makaimu. Kwa sababu, hili dirisha la Watendaji wa Kata limekuwa kama ni kiingilio tu kwenye Mfumo wa Serikali, baada ya hapo wanaanza kutafuta recategorization, wanatafuta kuhama, ndiyo maana mpaka leo watendaji hawatoshi. Kama ikirudishwa halmashauri, linapotoka tu tangazo kwamba kuna kazi ya Mtendaji wa Kata anatakiwa Kata mbili za Mkalama, Kata ya Mwangeza na Kata ya Mpambala, Mtendaji anatakiwa. Pale tu anapoanza kutuma maombi lazima aulize hii Mwangeza iko wapi, hii Mkambala iko wapi ataji-tune kabisa, anajua ninapoomba, nitakwenda wapi. Kwa hiyo, anapoomba ile kazi anajua kabisa, kama anaona kabisa haya maisha hatayaweza wala hataomba, kwa hiyo, ataomba akijua anaenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo hata anapoajiriwa mtu atakaa yale maeneo, Utumishi waendelee kama wanavyofanya kwenye vijiji. Watendaji wa vijiji wameshapeleka kule, madereva kule, hata hii ya kata niwaombe Utumishi wana kazi nyingi mno kuthibitisha watu, kupandisha watu, yaani nyingi, hebu hii kada ya Mtendaji wa Kata, niwaombe TAMISEMI wakae na Utumishi wairudishe hii kada kwao, watu waombe kazi hii ya Utendaji wa Kata kwenye halmashauri zetu, wawe wanajua haya mazingira. Hawa watu ni muhimu sana ndiyo wanaosimamia fedha zote za maendeleo huko chini, shule zetu, dispensaries zote, ndiyo ma-governor wetu kule. Katika sehemu nyingine Mtendaji wa Kata ni kama Mkuu wa Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kata hii niliyokuwa naisema hapa ya Mwangeza kilometa 70 mpaka DC aje ni lini. Kwa hiyo, niombe hii kada irudi halmashauri, ajira watu waombee halmashauri ili tuwachague sisi wenyewe. Utumishi wapeleke tu watu wakasimamie kama kazi imefanyika kwa haki na vitu vingine, lakini iombewe katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru muda umeisha...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ya pili hiyo.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Nimwombe sana Waziri, ombi langu la kuigawa Mwangeza tafadhali alifanyie kazi. Ahsante sana. (Makofi)