Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa afya njema na kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu. Pia, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, ndugu yangu Mchengerwa pamoja na Manaibu wake wawili Dkt. Dugange pamoja na Zainab Katimba, kwa kweli, wanafanya kazi kubwa. Niwapongeze pia, timu nzima ya Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu waliotangulia kusema kwamba wanamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambazo anazifanya kwenye Nchi ya Tanzania kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Mimi kama Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale na wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale tunamuunga mkono na tunampongeza sana kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi chake cha miaka mitatu, ameweza kutupatia fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo kwa Wilaya ya Nyang’hwale upande wa afya, maji, elimu, umeme, barabara, minara ya simu, kilimo hata VETA ametujengea. Tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 40 na zimekwenda kwenye miradi ya maendeleo, Mama ameupiga mwingi, Mama hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mkuu wa Mkoa wetu wa Geita, Martin Shigella, tunamwita ni mtambo wa maendeleo. Nampongeza sana vilevile Mkuu wa Wilaya yangu, Mama ambaye anajisimamia, Grace Kingalame na Katibu Tawala naye ni mwanamama anaitwa Kigua Omary, naye pia namuunga mkono kwa kazi nzuri, Mwanamama huyu anajisimamia. Pia, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale naye ni mwanamama Bi. Husna Tony, akinamama hawa, wanafanya kazi kubwa, nawapongeza sana akinamama hawa kwa kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mchango wangu ni kushukuru na kuomba, mambo ambayo nataka niyaombe leo ni machache na la kwanza, niliomba kujengewa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Busolwa. Ombi hilo lilikubaliwa na tukatengewa milioni 520 ili ujenzi huo uanze lakini hadi leo hii ujenzi huo haujaanza. Namkumbusha Mheshimiwa Mchengerwa ahakikishe ahadi hiyo anakwenda kuitekeleza kwa sababu wananchi wanausubiri kwa hamu Mradi wao huo wa Kituo cha Afya cha Busolwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, shilingi milioni 500 hizo tunaamini kabisa hazitatosha, lakini ni mwanzo mzuri, tunazisubiri kwa hamu. Kwa mwaka huu wa bajeti hii ambayo tunaenda kuipitisha, tunaomba basi fedha hizo ziweze kutoka ili kituo hicho kiweze kujengwa. Tuna vituo vya afya vinne lakini vituo vitatu vina shida ya magari ya kubebea wagonjwa, kwa hiyo, tunaomba kwenye bajeti hii tuweze kupata magari haya ya kubebea wagonjwa kwenye Kituo cha Afya cha Nyang’hwale, Kituo cha Afya cha Nyijundu na Kituo cha Afya cha Kafita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli changamoto hiyo ni kubwa, wagonjwa wetu wanapata shida, tuna gari moja ambalo lipo kwenye Kituo cha Afya Kharumwa ndilo hilo linakwenda huku na huku, kwa hiyo, tunaomba sana Waziri aliangalie hilo kwa jicho la tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, atenge fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ya zahanati ambayo wananchi wetu wamejitolea kwa nguvu zote kujenga maboma hayo wakitegemea kwamba Serikali inakuja kukamilisha na ndivyo tulivyokuwa tunawaambia. Kwa hiyo, tuna majengo mengi ya zahanati kwenye Wilaya yetu ya Nyang’hwale yanahitaji kumaliziwa. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri, aliandike hilo na ahakikishe kwamba anawaunga mkono wananchi wetu ili hata tukiwaomba tena nguvu zao kwenye miradi mingine, wasisite. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atoe fedha kwa ajili ya kumalizia maboma ya madarasa kwenye shule za misingi, sekondari na nyumba za walimu. Majengo haya yapo, wananchi wamejitolea, na ni kweli kwamba yanahitaji umaliziaji kutokana na fedha za Serikali, kwani halmashauri haitaweza. Kwa hiyo, naomba sana alichukue hilo, ahakikishe anatutengea fedha angalau hata kama ni shilingi bilioni mbili au tatu ziweze kusaidia kukamilisha maboma hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto upande wa watumishi. Ukweli Wilaya ya Nyang’hwale tuna upungufu mkubwa wa watumishi kwenye sekta ya afya, elimu na maeneo mengine. Tunaomba kwa hiki kibali ambacho ameenda kukiomba kwa ajili ya watumishi, ahakikishe anatupunguzia kero hiyo kwenye Wilaya yetu ya Nyang’hwale kwa sababu upungufu ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, namwomba Mheshimiwa Waziri, kuna mradi fulani ambao ulianzishwa, mpaka kufikia leo ni takribani miezi 20 imepita, mradi huu ni wa ujenzi wa kilometa moja ya lami pale Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale, lakini miezi 20 hiyo kilometa moja haijakamilika. Ukiongea na mkandarasi, anasema fedha sina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe lami hiyo kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale inakamilika. Leo tuna miezi 20, kila nikisimama hapa Mheshimiwa Waziri ananiambia tatizo kubwa ni fedha, fedha ikipatikana tutamalizia. Naomba alichukue kwa uzito wake, ili hiyo lami ya kilometa moja iweze kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache, naomba maombi yangu yachukuliwe kwa uzito wake ili nami nihakikishe kwamba mwaka 2025 nina vitu vizito vya kuzungumzia pamoja na kwamba Mheshimiwa Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan ameshafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)