Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami pia niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye imempendeza yeye, sisi waja wake kujadili bajeti hii ya Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kipekee kabisa niungane na wenzangu kutoa shukurani zangu za dhati kwa Rais wetu, Mama yetu Mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote nyakati ngumu huwa zinazalisha viongozi ambao Taifa ama jamii husika haijapata kufikiri kwamba inao na katika nyakati hizo ambazo siyo za kawaida, zinahitaji maamuzi ambayo siyo ya kawaida ili jamii na Taifa lipate kwenda mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu na Mkoa wangu wa Morogoro unapitia kipindi kigumu ambacho hatujawahi kupitia katika historia. Tangu Desemba tumekuwa na mafuriko wilaya moja mpaka nyingine na hata juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa Morogoro katika Wilaya ya Kilombero katika Majimbo ya Mlimba na Ifakara kushuhudia kadhia ya mafuriko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa, namshukuru Mama yetu, Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kusimama na wananchi wa Mkoa wa Morogoro katika nyakati ngumu kabisa ambazo hatujawahi kushuhudia katika uhai wetu. Kipekee kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ndugu yetu Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na Menejimenti ya TAMISEMI kwa kusimama na wananchi wa Mkoa Morogoro, kwa kusimama na wananchi wa Tanzania katika kipindi kigumu ambacho sisi kama wawakilishi wa wananchi tumepata kukishuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mtovu wa fadhila nisipomshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Ndugu yetu na kaka yangu Kigoma Malima, Ndugu yangu Shaka Hamdu Shaka, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Kamishina Haji Mussa. Kwa kweli amani ambayo sisi Wabunge tunayo humu ndani kimsingi imetokana na wao kutimiza wajibu wao katika nafasi yao ya kiutawala na kiutendaji. Wametimiza wajibu wao na wameitendea haki dhamana ambayo wamepewa na Taifa letu. Kwa hiyo, ninawashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi, tarehe 05 Desemba tulishuhudia madhara makubwa ambayo yaliyowakuta ndugu zetu wa Hanang na kwa bahati mbaya au nzuri siku ile mimi nilikuwa Rufiji nikiungana na Waziri Mchengerwa katika Tamasha. Kadhia ile ilipotokea tulifikiri kwamba Rufiji na Morogoro ziko mbali, lakini muda si muda na sisi pia tumeenda ku-experience madhila yale. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wote wa Tanzania ambao wamepata madhara ya mafuriko, kuvunjika kwa mindombinu, pia majanga ya njaa na vitu vingine kutokana na kadhia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kumshukuru Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, sisi Wanamikumi tuna sababu za ziada za kumshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na timu yake. Kwa kweli, jimbo hili lilikuwa linaitwa jimbo la giza, kwa sababu 2020 katika vijiji 58 ni vijiji 25 tu vilikuwa na umeme na ni vijiji 23 tu vilikuwa na mawasiliano, lakini kulikuwa na kata zaidi ya tatu ambazo zilikuwa hazifikiki kwa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyozungumza tunaenda kukamilisha vijiji vyote kwa kuviwekea umeme, na pia tunaenda kukamilisha mawasiliano katika kata karibia zote na tunaenda kuhakikisha tunajenga barabara katika kata zote. Mafanikio haya hayawezi kupita kimya kimya, hivyo naungana na wananchi wote wa Tanzania kuishukuru Ofisi ya TAMISEMI kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2024/2025 katika ukurasa wa nne, pale kumeainishwa vipaumbele vya maendeleo na wanasema kwamba walitilia maanani maoni na ushauri wa Wabunge. Maeneo ambayo yaliainishwa ni miundombinu, kilimo, mifugo, uvuvi, nishati na utalii kama maeneo ya kimkakati ya ku-boost uchumi wetu, lakini pia kuwaondolea umaskini wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii ambayo inaendelea ya uvunjifu wa miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko kwa sababu ya mafuriko ambayo yanaendelea, bila shaka yanaenda kuhatarisha utekelezaji wa malengo na vipaumbele hivi ambavyo vimeorodheshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hatua za kawaida ambazo zinapaswa kuchukuliwa. Moja, ni kuhakikisha kwamba TARURA ambao ni Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini wanapata fedha za dharura kwa wakati. Pili, bajeti hii ambayo inaendelea ni lazima tufunge mikanda kuhakikisha kwamba fedha zote zinaenda. Wapewe ruhusa ya kutangaza tender, waendelee na mchakato wa ujenzi wa ku-restore maeneo yote muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipofanya hivyo, kuna hatari kwamba bei ya pembejeo inaenda kupanda katika maeneo yote ya vijijini. Kupanda kwa bei ya pembejeo katika maeneo ya vijijini kutokana na uharibifu wa miundombinu na gharama za usafiri kuongezeka, zitasababisha wakulima wetu kutotumia pembejeo, na hivyo mavuno kuwa madogo ambayo yanaenda kusababisha njaa. Kusababisha njaa maana yake kunaenda kuongeza bei ya vyakula mijini, hilo linaenda kuongeza mfumuko wa bei na kupunguza uwezo wa mwananchi wa kuweka akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiliachilia hilo, maana yake tunaenda ku-compromise na ukuaji wa uchumi, tunaenda ku-compromise na vita dhidi ya umaskini na wananchi wetu na tunaenda ku-compromise na ukuaji wa pato la Taifa na hivyo kuja kushindwa kutimiza malengo ambayo tumejipangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuzuia yote hayo, ni vizuri sasa kupeleka fedha kwa wakati, kuunganisha miundombinu kati ya mashamba na masoko, na mashamba na viwanda ili mwananchi asafirishe mazao yake kwa uhakika na pia apate pembejeo kwa wakati. Kwa kufanya hivi, tutamnusuru huyu maskini ambaye Taifa linapanga kumtetea na kuona namna ya kumkwamua katika changamoto za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya TAMISEMI ni kubwa. Moja ya kazi kubwa ya TAMISEMI ni kuratibu shughuli zote za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, lakini bado Wizara hii haijatendewa haki ama hatujaitendea haki na ndiyo maana kuna trend ambayo tunaona kwamba kila mmoja ananyofoa jukumu lake badala ya ku- decentralise anaenda ku-centralise.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwananchi wa kijijini ambaye katika msingi wa Katiba yeye ndiye ametoa mamlaka kwa Serikali kuendelea kushika dola, anakosa mahali pa kusemea. Ndiyo maana Taasisi muhimu kama RUWASA ambazo zinashughulikia maji vijijini, Taasisi kama REA ambayo inashughulikia nishati kwa maana ya nishati ya kupikia, nishati ya kuendeshea vyombo pia na nishati ya umeme, taasisi hizi zinapaswa kufanya kazi kwa karibu na TAMISEMI ama kuwa chini ya TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuziweka hizi taasisi katika Wizara ambazo zinasimamia sera, maana yake tunakosa uwezo wa mwananchi mmoja mmoja kuhoji katika vikao vya kijiji, kata na Mabaraza ya Madiwani na hivyo kwenda ku-miss main point ambayo ni kumwondoa mwananchi na ku-transform uchumi wetu kupitia sera ya D by D. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunaona kwamba hata bajeti ya TAMISEMI mara nyingi imekuwa compromised kwa sababu ya vikao, semina na makongamano ambayo havihusu TAMISEMI moja kwa moja. Barua na maelekezo yamekuwa yakitoka kuwaelekeza Wakurugenzi kugharamia semina na mikutano ambayo inaandaliwa na taasisi nyingine ambazo zina bajeti yao, zina mipango yao na kalenda zao. Hivyo, kwenda ku-compromise fedha za maendeleo katika halmashauri zetu kugharamia mikutano na semina ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa umefika wakati wa kuimarisha Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kumpa mwananchi sauti. Sasa wakati umefika wa kuimarisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Katika hilo kama tunazungumzia sekta ya utalii, idara ya uratibu wa sekta ni lazima isimamie na bahati mbaya imekufa. Kama TAMISEMI ndiyo mratibu mkuu wa shughuli zote za kimaendeleo, ni vyema idara ya uratibu wa sekta ikarudi TAMISEMI kusimamia sekta zote mtambuka kama uvuvi, kilimo, ushirika na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumaliza kwa kusema kwamba nasimama na Mama Samia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango mzuri.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mikumi tunasimama na Mama Samia. Naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)