Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu. Nashukuru kwa afya ambayo tumejaliwa na Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nitoe pole kwa Watanzania wote ambao wamekumbwa na janga hili la mafuriko wakiwemo wananchi wa Rufiji, poleni sana. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi na liweze kupita salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami natamani kutoa mchango wangu kwenye mambo kadhaa. La kwanza, naomba nianze na ahadi za viongozi; Wilaya ya Chemba mwaka 2020 Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alifika Wilaya ya Chemba, akatuahidi kupata stendi ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifuatilia suala la ujenzi, TAMISEMI walitupa maelekezo tutafute eneo, tufanye usafi na tuweze kufanya mambo mengine ya awali. Yote hayo tumeyafanya, lakini mpaka sasa TAMISEMI bado mko kimya. Mheshimiwa Waziri mara kadhaa nimeuliza swali hapa na mmeendelea kutuambia liko kwenye mchakato. Naomba utakapokuja kuhitimisha hoja yako, wananchi wa Chemba wanatamani kusikia Stendi ya Wilaya ya Chemba inakwenda kujengwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine pia ni ujenzi wa soko. Hali kadhalika tulikuwa na ahadi hiyo ya soko, nalo mpaka sasa ni kimya. Tayari eneo tulishalitenga na fidia tulishalipa. Tunasubiri TAMISEMI mtuambie soko Wilaya ya Chemba linajengwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie suala zima la upungufu wa walimu na watumishi wengine wa kada zote. Elimu ndiyo kila kitu katika maisha yetu. Upungufu wa walimu umekuwa ni changamoto kubwa sana kwenye halmashauri zetu na kwenye shule zetu. Jana Mheshimiwa Simbachawene ametutangazia kwamba Serikali inakwenda kuajiri katika ajira 46,000; 12,000 ni za walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ajira hizo kidogo zilizotoka, bado tunahitaji Serikali iwekeze kwenye elimu hususan kwenye suala zima la walimu. Kwenye Wilaya ya Chemba kuna upungufu wa walimu 998. Shule za msingi tuna upungufu wa walimu 729 na shule za sekondari tuna upungufu wa walimu 269. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye ajira 12,000 tusaidie Wilaya ya Chemba kwani tunateseka. Matokeo ya kimkoa Wilaya ya Chemba, sisi ni wa mwisho, lakini Kitaifa pia Wilaya ya Chemba ni wa mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunatia huruma sana na inasikitisha. Kwa sababu gani? Watumishi walimu ni wachache, lakini pia hata walimu wetu wanapopangwa kwenda kwenye shule zetu, Wilaya ya Chemba ina mazingira magumu sana. Miundombinu ya barabara hatuna, miundombinu ya maji hakuna, hospitali hakuna. Kwa hiyo, walimu wanapoletwa kwetu wanaripoti, wanakaa mwezi mmoja wanaomba kuhama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishawahi kuomba hapa ndani nikamwambia Mheshimiwa Waziri tusaidieni hawa walimu wanaokwenda na watumishi mbalimbali wanaoenda kwenye halmashauri ambazo zina miundombinu siyo rafiki, tuwape basi hata motisha ya kukaa kule. Wawe na posho ambayo itawatia moyo kwa ajili ya kukaa kwenye hayo mazingira magumu kwa sababu sisi sote ni Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hao Watanzania walioko huko kwenye mazingira magumu wanahitaji pia nao kupata huduma ya Serikali, Serikali yao inatakiwa iwahudumie. Kwa hiyo, nimwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja, hili suala la watumishi aone ni namna gani tunawawezesha watumishi wetu wanaokwenda kwenye mazingira magumu angalau waweze kupata posho ya kujikimu, kumpa motisha kuweza kufanya kazi kwenye yale mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni madai ya watumishi. Nilizungumza hapa mwaka 2023, nilizungumza mwezi wa Pili na leo nalisema tena. Watumishi wetu wana hali ngumu, pamoja na mambo mengine yote waliyonayo hii stahiki yao ambayo wanadai ambayo wameifanyia kazi, hivi ni kwa nini hatutaki kuwalipa? Serikali shida ni nini? Hawa watu hawaombi hisani, ni haki yao. Wamefanya kazi kwenye Taifa lao, wameihudumia nchi yao, kwa nini hatuwalipi madeni yao? Kama haiwezekani, basi tuwaambie kwamba jamani madeni yenu sameheni, muwe kama mmetoa msaada kanisani au msikitini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwatendei haki hao wananchi wetu. Watanzania wenzetu ambao wanalitumikia Taifa hili, kufundisha, kutibu, kufanya kila kitu, wanadai haki zao, hatutaki kuwalipa. Huku tunawanyima hizo stahiki, ukija huku mmewabana kwenye kikokotoo, waende wapi hao watu? Mnataka waende wapi? Nilishawahi kusema humu ndani, kama tunaona hiki kitu ni sawa, hebu tuanze humu ndani sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusilipwe humu ndani. Kama kikokotoo pia tunakiona ni haki, hebu tuanze safari hii, mwakani mwezi wa Sita kikokotoo kituhusu, tuanze nalo humu ndani. Si tunaona ni haki, na ni sawa na hakina shida! Tuanze na sisi Wabunge kutunziwa fedha zetu tuwe tunapewa kidogo kidogo, kwa sababu tunapokosa Ubunge pia tunakuwa na maisha magumu zaidi kuliko hata hao watumishi tunaosema kwamba walipwe tuwatunzie fedha zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu nyingine ni suala zima la uchakavu wa miundombinu kwenye hospitali zetu, vituo vya afya, zahanati; na pili, majengo ya shule kwa maana ya madarasa, ofisi za walimu, lakini baya zaidi vyoo shuleni. Mpaka leo bado tunahangaika na suala zima la ujenzi wa vyoo. Naomba miradi yote inayokuja kwenda shuleni, madarasa yanayojengwa tuambatanishe na suala zima la ujenzi wa vyoo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga shule nzuri sana safari hii, lakini bado suala la vyoo ni changamoto. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba suala hilo la vyoo pamoja na uchakavu wa miundombinu ya madarasa kwenye shule mbalimbali mlichukulie hatua. Kuna shule nyingine ambazo madarasa yake, yaani mlango na dirisha havina tofauti. Kengele ikigongwa, mtoto mwingine anatokea dirishani, mwingine anatokea mlangoni. Kwa hiyo, inakuwa haieleweki mlango uko wapi, wala dirisha liko wapi? Kwa hiyo, tuwasaidie katika hizo shule ambazo mindombinu yake siyo rafiki sana, mweze kufanya huo ukarabati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo natamani kulisema siku ya leo ni suala zima la posho za Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Vijiji. Tulisema hapa, tunashukuru Serikali iliwarudisha Madiwani wetu, wanalipwa na Serikali Kuu, lakini tuliomba Madiwani hawa waongezewe posho, kwa sababu leo ukiangalia kwa uhalisia Wabunge tunaohudhuria kwenye halmashauri hatufiki hata nusu. Wanaosimamia halmashauri zetu na mipango yetu yote ni Madiwani wetu kule chini. Miradi mbalimbali inapopelekwa kule chini Wenyeviti wetu wa Wijiji ndio wanaosimamia ile miradi kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mwenyekiti wa Kijiji unamlipa posho shilingi 10,000 kwa mwezi, hivi wewe Mbunge leo nikupe shilingi 10,000 hata hapo canteen huwezi kunywa chai. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, suala la posho kwa Wenyeviti wa Vijiji mliangalie upya. Shilingi 10,000 imeshapitwa na wakati, ongezeni kiwango na ninapendekeza Wizara waone sasa hivi maisha yamepanda. Kwa sababu Madiwani tulishawatoa kwenye halmashauri, basi angalau Wenyeviti wapate shilingi 50,000 au shilingi 100,000 ili iweze kuwasaidia na wao kujikimu na majukumu makubwa wanayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika Madiwani, tuliomba hapa kwamba baada ya kuwatoa huko, Serikali ione namna ya kuwaongezea hao watu posho. Waongezeeni na wao posho. Leo shilingi 350,000 kwa maisha yaliyopo siyo sawa sana. Tuwaone na wao kwa sababu ndio watumishi na ni watendaji kule chini wanaotusaidia majukumu yetu mbalimbali. Tuone na wao wanastahiki ya kuweza kupata kipato ambacho kitawasaidia katika kutimiza wajibu na majukumu yao mbalimbali kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni hospitali yetu ya wilaya. Tuna mortuary iko pale, lakini ile mortuary haina majokofu. Tunaomba sana, wananchi wetu pale wanapata tabu, ndugu zao wanapofariki wanatakiwa kuchangia fedha ya kutoa mwili Hospitali ya Wilaya ya Chemba kupeleka Kondoa. Sasa imefikia hatua wananchi wanaiba maiti zao wanaondoka nazo kinyemela kwa ajili ya kuepuka gharama za kubeba mwili kutoka pale wilayani kupeleka wilaya nyingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba sana na hilo pia utuone watu wa Wilaya ya Chemba kwenye suala zima la uwepo wa jokofu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nilitamani sana kulisemea suala zima la magari kwa Wakuu wa Wilaya. Wakuu wetu wa Wilaya walio wengi nchini hawana magari. Kwa hiyo, naomba pia Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie, Wakuu wetu wa Wilaya wasio na magari wana mkakati gani wa kuwawezesha ili waweze kupata magari? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, muda wako umekwisha.