Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana tena sana kwa kupata fursa ya kuchangia Bajeti ya TAMISEMI. Ni nadra sana kwangu kuchangia TAMISEMI, lakini leo inanipa fursa nzuri ya kutaka kuchangia, nawe umenipa nafasi hii ya kuchangia, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuleta hapa leo tukiwa tuna uhai na uzima, tunapumua vizuri na Mwenyezi Mungu awajalie huko ambao wametangulia mbele za haki, awalaze mahali pema peponi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba nipongeze zaidi na kuomba machache. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais. Kusema kweli katika kipindi ambacho bajeti ya TAMISEMI imekuwa ngumu, ni bajeti ya mwaka 2023/2024. Kwa sababu gani? Kwa sababu miundombinu mingi imeharibika, lakini pamoja na uchache wa bajeti, mmeweza ku-manage, hongereni sana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa considerate. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niwape pole sana waliopata maafa ya mafuriko na mengine mengi, lakini nikupe pole sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa kwa kukutana na majanga ya mafuriko katika Jimbo lako. Insha’Allah Mwenyezi Mungu awajalie wale waliopoteza maisha kwa wale watoto wetu wapendwa wa Mkoa wa Arusha, Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ni mama, ni mzazi, ni baba yetu. Ni baba kwa cheo chake, kwa sababu gani? Kwa sababu katika kipindi chake cha miaka mitatu ameweza sana kujali maslahi ya watoto wetu wa Taifa hili ambao ndiyo msingi wa maendeleo ya baadaye. Amejali vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amejali kwa kuhakikisha kwamba pesa nyingi ameipeleka chini kwenye huduma za jamii. Leo hii hapa Bungeni unaona kila mmoja anayesimama hapa hata kama atasema changamoto, lakini atapongeza. Hatupongezi kinafiki, hatupongezi kiuchawa, tunapongeza kwa sababu tumefanya ziara, tumeona mambo mazuri ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya huko chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona hospitali zinazojengwa, tunaona shule za msingi ambazo sasa hivi watoto wetu wanakanyaga tiles na wana-slide madirisha ya vioo. Yote haya ni Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mwenyezi Mungu anasema asiyeshukuru kwa kidogo hawezi kushukuru kwa kikubwa kamwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kushukuru huko, nashukuru pia kwa TAMISEMI au Serikali kukubali kuhakikisha au kurekebisha sheria na kanuni zinazoendesha CSR. Naomba niwapongeze sana Serikali kwa sababu bei nyingi ambazo tunapewa na kwa vitu ambavyo vinatakiwa vifanyike, hazina uhalisia. Unaweza ukaambiwa pad shilingi 8,000 wakati mtaani tunafahamu pad ni shilingi 3,500 au 3,000 au 2,500. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kuwa mmeamua kwenda kuangalia, basi mkaangalie uhalisia au namna gani mtaweza kuunda vizuri sheria hizi au kanuni hii ya CSR ili iweze kunufaisha nchi yetu na Taifa letu kwa ujumla. Nataka niwaambie watu kwamba, nilipofika hapa Bungeni nilianza kuwa katika Kamati ya Katiba na Sheria. Mwenyekiti wangu alikuwa Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa. Kaka yangu umekuwa una-support kubwa sana na watu wenye ulemavu, naomba nikupongeze kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa kila nikisimama kuzungumza masuala ya watu wenye ulemavu umekuwa ukikazia sana na kitu pekee pia ulikuwa unaomba zaidi ulikuwa unaomba takwimu za watu wenye ulemavu. Tunashukuru Sensa ya mwaka 2022 leo hii tuna takwimu za watu wenye ulemavu. Takwimu hizi zitaenda kufanya nini? Zinaenda kusaidia Serikali kutengeneza mikakati na mpango wa kusaidia watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba sasa hivi watu wenye ulemavu ni asilimia 11 ya population yote. Ni watu wengi sana asilimia 11.2, watu wenye ulemavu ni wengi mno. Serikali lazima mjipange mjue namna gani ya kuweza kusaidia watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Mchengerwa kwa sababu ulikuwa Mwenyekiti na ulikuwa ukisimamia masuala yote ya watu wenye ulemavu, lakini leo hii wewe umepewa rungu sasa kusimamia, I mean kutenda. Sasa upo kwenye nafasi ya kutenda. Ninakuomba sana kaka yangu kwa mapenzi uliyonayo kwa watu wenye ulemavu, naamini kabisa unaenda kutenda haki. Unaenda kusimamia maslahi ya watu wenye ulemavu kwenye nyanja tofauti tofauti, tukianzia kwenye upande wa Ofisi za Watu Wenye Ulemavu katika Halmashauri zako. Hili jambo Mheshimiwa Waziri Mkuu alilitoa kama mwongozo. Sasa basi tengenezeni mwongozo wa maandishi. Serikali itambue kwamba kila halmashauri inapaswa kuwa na Ofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnaweza mkashangaa kwa nini tunalilia Ofisi? Tunataka watu wenye ulemavu wajue eneo lao la kupeleka malalamiko yao na changamoto zao na kupata maelekezo juu ya asilimia mbili na kutambua fursa zilizopo za watu wenye ulemavu. Tunahitaji Ofisi Mheshimiwa Mchengerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya mafuta ya watu wenye ulemavu, nataka nijue, usimamizi wa fedha zile uko vipi? Mpaka sasa bado sijapata majibu ya namna gani au mmeshatengeneza mafuta haya au vipi? Sijapata majibu. Ninaomba leo hii katika Wizara yako, basi nipate majibu mazuri ya watu wenye ualbino wanapata vipi mafuta katika halmashauri zao? Kwa sababu fedha zimetoka na nina uhakika mwaka huu pia mtatenga fedha kwa ajili ya kununua mafuta ya watu wenye ulemavu au kwa ajili ya kutengeneza kwa urahisi, kwa bei ya chini mafuta ya watu wenye ulemavu ili yaweze kupatikana kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyosema kuhusu mafuta, naomba mnielewe jamani. Sisi watu wenye ualbino ili tuishi, tutembee, tufanye kazi zetu tunahitaji kupaka mafuta, siyo tu baby care, tunahitaji kupaka mafuta ya kuzuia mwanga wa jua. Hii inatuboreshea afya zetu inatulindia ngozi zetu. Kwa hiyo, nawaomba sana mnielewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni bahati iliyoje, namshukuru Mheshimiwa Rais sana, sana, sana kwa kutambua tena umuhimu wa vijana, amemteua rafiki yangu Mheshimiwa Zainab Katimba. Mheshimiwa Zainab Katimba ni mfano mzuri wa binadamu ambaye anapenda watu wenye ulemavu. Mimi ni rafiki yake na anafahamu changamoto zetu nyingi kwa sababu nimekuwa nikizungumza naye mara kwa mara. Anafahamu na kujua changamoto na matatizo ya watu wenye ulemavu na ninaamini kabisa atakuwa msaada kwake tosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Rais hajakosea kwa sababu amemweka mtu ambaye ni mtendaji kazi mzuri, hodari na mchapakazi, mwenye huruma. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana kumteua rafiki yangu Mheshimiwa Zainab Katimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisipozungumza jambo hili nitakuwa sijatendea haki hii bajeti. Naomba pia niipongeze Serikali kwa miundombinu ya watu wenye ulemavu katika shule pamoja na vyoo vya watu wenye ulemavu shuleni.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KHADIJA S. TAYA: … lakini ombi langu la mwisho kabisa kwa Serikali…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa…
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa…
MHE. KHADIJA S. TAYA: … ombi langu la mwisho, la mwisho kabisa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, ngoja basi niseme.
MHE. KHADIJA S. TAYA: … ni kuongeza idadi ya…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, mimi nasemea hivi…
MHE. KHADIJA S. TAYA: …ya wafa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, acha niseme basi.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa.
NAIBU SPIKA: Kwa vile hoja yako ni muhimu na umelia sana, nakuongeza dakika moja. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amejenga miundombinu ya shule pamoja na vyoo vya watu wenye ulemavu, tunaomba tuongezewe idadi ya walimu wanaofundisha watoto wenye ulemavu. Tunakuomba sana Mheshimiwa Mchengerwa liangalie hilo ili tusipate shida ya kutambua kwamba huyu amefaulu tumpeleke shule hii au tumhamishe huku. Shule hizi muhimu jumuishi zikipata walimu wazuri, watu wenye ulemavu wanaenda kuelimika na umasikini unaenda kwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)