Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Geita na Mkoa mzima wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naomba nitumie fursa hii kwanza kutoa pole kwa wananchi wa Mgusu ambako mvua kubwa na mafuriko yamechukua watoto wawili wa shule, na pia kwenye Kata ya Nyankumbo ambako pametokea landslide ndogo ingawa imeharibu mashamba, hapakuwa na madhara makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampa pole Mheshimiwa Mchengerwa kwa mafuriko Jimboni kwake na wananchi wote katika nchi nzima ambao wamepata aina hiyo ya matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwanza kwa kazi nzuri anayofanya na kwa kuendelea kuipa Halmashauri ya Mji wa Geita fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kuzungumza kwenye suala la elimu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali tumejenga shule za sekondari nzuri na tumebadilisha mtaala sasa kwamba watoto watakaoanza darasa la kwanza wataendelea hivyo mpaka sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza eneo hili kwa takwimu. Tangu mwaka 2020 mpaka leo sisi Halmashauri ya Mji wa Geita tumejenga shule 14 za sekondari. Katika shule 14 za sekondari tukapokea walimu 49, katika hao walimu 49 tuliopokea kuna zaidi ya walimu 25 waliostaafu lakini hizi shule 14 zilihamisha walimu kutoka shule nyingine.
Mhesimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maana yake kuna shule ambazo tulihamisha walimu. Ukichukua walimu tuliowapokea, ukachukua walimu waliostaafu ina maana kwa miaka minne tumepokea walimu 25, tuna upungufu wa walimu 422. Kwa hiyo, tunapopongeza kujenga shule nzuri ni sawasawa na kuwa na computer halafu haina software, huwezi kuitumia. Tuna majengo yanang’aa lakini hayawezi kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye shule ya msingi, tumejenga primary 13 na tumejenga shule hizi siyo kwa bahati mbaya. Geita Mjini ina watu takribani 400,000. Influx ya watu wanaoenda kutafuta kazi kwenye migodi ni kubwa. Kwa hiyo, pia idadi ya watu inaongezeka kila siku. Kwa hiyo, tumejenga shule 13, tukapokea walimu 51 kwa miaka minne. Katika hao waliostaafu 37, waliokufa saba, waliofukuzwa kazi kwa sababu mbalimbali 46, jumla 93.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukichukua tuliowapokea 51 kutoa 97 unapata minus tangu mwaka 2020, upungufu walimu 800. Sasa nilishangaa sana maamuzi ya TAMISEMI ya kusambaza walimu halafu wakasema mijini hatupeleki walimu, sijui takwimu walizipata wapi kwa sababu kwa takwimu hizi zinakwambia tuna negative. Ina maana tangu mwaka 2020 hatujaajiri walimu na waliopungua ni wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naiomba sana Wizara ya TAMISEMI. Hata kama tungetaka kupunguza gharama huwezi kupunguza gharama kwa ku-compromise muda wa mwanafunzi anayekaa shuleni. Huyu mwanafunzi asipopata elimu yake darasa la kwanza, la pili na la tatu kwa kiwango kinachokubalika hata ukimpelekea walimu wengi darasa la tano na la sita hawawezi kumsaidia kitu chochote. Huyu mwanafunzi asipopata walimu wa kutosha form one, form two hata ukipeleka walimu amefika form three huwezi kusababisha masomo aliyoshindwa kuyapata akiwa form one na form two aweze kuyapata. Kwa hiyo, maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba tunawadhulumu hawa watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, mwaka juzi tulipata fedha za kujenga shule mpya ya sekondari. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, shilingi milioni 470 hazikutosha, tukaelekezwa halmashauri tuongezee tukaongezea. Kwenye component ya majengo palikuwepo na majengo kwa ajili ya kupeleka computer.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshauri Mheshimiwa Waziri, kwenye shule zote za sekondari ufanyike mchakato wa kujenga lab ya computer na wasaidiwe kupata software ambayo itawezesha baadhi ya masomo wakaweza kujihudumia wenyewe kwa kutumia computer zilizopo, isiwe shule mpya peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekamilisha shule ya wasichana kwa pesa ambayo tumepewa na Mheshimiwa Rais, zaidi ya shilingi bilioni tatu, na muda wowote inaweza ikaanza, lakini hatuna walimu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue jambo hili kwa umuhimu wake mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Geita Mji imeomba kuwa Manispaa kwa muda mrefu sana. Geita Mji kitakwimu mwaka huu 2024/2025 tunaokwenda sasa tumepangiwa kukusanya shilingi bilioni 19; mwaka 2023/2024 tulipangiwa kukusanya shilingi bilioni 14 tutafikia asilimia 100; mwaka 2022/2023 shilingi bilioni 12; mwaka 2021/2022 shilingi bilioni 10. Hakuna mwaka ambao tumekusanya chini ya malengo. Maana yake nini? Ukitazama trend ya mapato, tunazidi baadhi ya mikoa, tunazidi baadhi ya manispaa na tunazidi baadhi ya halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kigezo ambacho tulipewa ni kuhakikisha kwamba ule mji wetu umepimwa. Tumepima tayari, kipato chetu kinaruhusu, miundombinu ndiyo hiyo, tuko kwenye satellite cities.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kukuomba, hakuna sababu kwa sababu kuifanya Geita kuwa Manispaa hakuongezi gharama yoyote kwa Serikali. Tuna Mkurugenzi yule yule, tuna Mkuu wa Mkoa mzuri anakaa pale pale, tuna Mkuu wa Wilaya mzuri anakaa pale pale, kinachobadilika ni jina tu Halmashauri ya mji kwenda Manispaa ya Geita Mjini. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwamba kuna mradi wa Barabara za TACTIC unaendelea, pale tunajenga takribani kilometa 18. Mji wa Geita unabadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara tunajenga kwa fedha zetu wenyewe. Kila mwaka tunajenga zaidi ya kilometa mbili kwa fedha zetu wenyewe za mapato ya ndani, lakini tunajenga barabara kwa CSR. Kwa mwaka tunajenga takribani kilometa nne za lami kwa mapato yanayotokana na Halmashauri ya Mji wa Geita. Mji wetu unabadilika, tunaweka taa kwenye miji, hatuna sababu kwa nini Serikali inasita kutupatia Geita Mji kuwa Manispaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kama kuna kigezo kingine kipya labda, lakini idadi ya watu, miundombinu na ukusanyaji wa mapto tunaamini hatuiongezei gharama yoyote Serikali. Sisi hatuombi kupewa sijui Halmashauri mpya; wanaoomba Halmashauri mpya ni Busanda na Geita, sisi tunaomba tupewe hadhi ya kuwa Manispaa kwa sababu sifa tunazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la tatu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, alifanya ziara Geita na ninamshukuru kwa sababu kipekee ulitupa heshima kubwa. Tulikuwa hatupo, tulikuwa tumeenda kwenye michezo Rwanda, akanipigia simu akaniambia anakwenda Geita akaomba nimweleze changamoto zilizokuwa pale Geita Mjini, nikamweleza ni barabara. Tunashukuru mradi wa TACTIC unaoendelea na tunashukuru sana kwa kweli Engineer Seff na timu yake wanafanya kazi yake vizuri, tatizo kubwa nadhani ni uchache wa pesa zinazotengwa. Geita Mjini pale Makao Makuu ya Mkoa kilometa 17 tunazozijenga ni kama asilimia moja ya mahitaji ya Mji wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ule mji upo kwenye gradient ya mlima, kwa hiyo eneo lote la chini mvua zinaponyesha, maji yanajaa kwenye nyumba za watu. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, naamini ana kumbukumbu maombi niliyomwomba ukiacha ya walimu na watumishi, tulimwomba barabara muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mji wetu ule unakua, lakini mji wetu uko kwenye mlima na unajaa maji na ni Makao Makuu ya Mkoa. tunate Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya mzuri sana. Sasa anapofanya ziara kule, anakwenda kukwama kwenye matope katikati ya mkoa. Ni aibu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, tumezungumza hapa kuhusu sheria ya CSR. Kwanza naishukuru sana Kamati na Wizara kwa mapendekezo yake. Kwa ujumla wake sisi ni halmashauri ya kwanza ambayo tumefanya vizuri sana kwenye CSR, lakini tumefanya vizuri kwa nguvu kubwa na kula hasara kubwa. Kwenye miradi yote tuliyofanya hakuna mradi unaokamilika hata kama mtatenga fedha za kutosha. Kwa nini? Kwa sababu kanuni inatutaka halmashauri kuwa watazamaji kwa takribani asilimia 80.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtaandaa BoQ mkishawapelekea walete material, waweke nini, matokeo yake kuna sehemu cement ni nyingi kuliko mchanga, sehemu nyingine matofali ni mengi kuliko mawe na kuna sehemu fundi amemaliza, lakini hakuna fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwa ku-review hii kanuni ili tuwezeshe halmashauri kutangaza na kumpata mkandarasi halafu wao walipe. Sisi hatuhitaji tuwe na fedha, wao wakae nayo, lakini walipe, na hivyo tutaondoa hata usumbufu wa sasa hivi ambapo tunajenga uwanja miaka mitano hatuwezi kumaliza. Ninakushukuru sana. (Makofi)