Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Mheshimiwa Mchengerwa, Waziri wetu wa TAMISEMI. Kwanza kabisa, naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nimekuwa Mbunge tangu mwaka 2005 lakini nataka nikiri na nisipolisema hili nafsi yangu itanisuta sana. Hakuna awamu ambayo Halmashauri ya Jimbo la Solwa tumepata fedha kama Awamu yake hii ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata sekondari mbili mpya, hakuna wananchi kuchangishwa na hakuna wananchi sijui kubeba nini. Zimekuja fedha kamili, tumeziweka kwenye Kata ya Usule na Kata ya Puni. Ndiyo kata mbili katika kata 26 katika Jimbo la Solwa ambazo zilikuwa hazina sekondari. Leo tuna sekondari mpya, wanafunzi wameanza kusoma, safi kabisa, wala hakuna shida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine nitazisema baada ya kusema haya mengine ya kumshukuru Mheshimiwa Rais. Tumepata shule za msingi mpya mbili ambazo tumezipeleka kwenye Kata ya Mwakitolyo na Kata ya Salawe kwa sababu idadi ya watu katika kata hizo ilikuwa ni kubwa mno. Mwakitolyo peke yake ilikuwa na wakazi 38,000, ndiyo maana shule moja mpya ya msingi tumeipeleka pale na nyingine tumeipeleka katika Kata ya Salawe yenye watu zaidi ya 32,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anafanya mambo mazito ndugu zangu. Hakuna siasa ngumu kama siasa ya nchi kama hii. Katika nchi maskini ambazo sasa hivi tunatoka, tuko kwenye uchumi wa kati ni siasa ngumu sana. Kwa kazi anazozifanya Mheshimiwa Rais, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono, tumpongeze na tumpe moyo wa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitazama tulikotoka mwaka 2005, Wabunge wote tulioko hapa na hii Awamu ya Sita, kama 2025 Mungu atakupa uhai na kama bado una nia ya kugombea, kwa nini usirudi kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Kazi kubwa unaifanya, yaani ushindwe wewe tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni umeme katika vijiji 126. Sasa hivi nina vijiji 115, nimebakiza vijiji 11 tu na vyenyewe viko vinatekelezwa. Katika awamu hii hii na katika bajeti hii inayoishia sasa hivi ni vijiji 70 kwa mpigo. Mheshimiwa Rais ametupatia fedha kutoka 2005, sijawahi kupata fedha kama hizi. Sasa tunakwenda kumaliza matatizo katika vijiji vyetu 126. Tunakwenda awamu ya kutoka kwenye vijiji kupeleka kwenye vitongoji vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ndiyo usiseme. Nilishawahi kuchangia hapa, ni vijiji zaidi ya 87. Tukipata 22 namsubiri tu Mheshimiwa Aweso atuletee kibali vijiji 22 Tinde Parking tumalize twende kwenye vijiji zaidi ya 105. Tumepata vifaa vyote kwenye hospitali ya wilaya. Yaani sasa hivi mgonjwa akija kwenye hospitali ya wilaya, hakuna sababu tena ya kumpeleka kwenye hospitali nyingine ya mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye zahanati, sasa hivi tuna zahanati 38. Tumejenga zahanati tatu mpya na sasa hivi zahanati tano ziko katika mpango mzima wa kukamilika, zaidi ya mwezi mmoja au miwili tutakuwa tumekamilisha. Changamoto namba moja ni watumishi kwenye zahanati hizo. Sasa hivi kwa namna ambavyo tumejipanga katika Jimbo la Solwa, katika halmashauri yetu tunakwenda kwa speed ya kila mwaka visipungue vijiji kumi. Sasa speed tunayokwenda nayo ni kasi mno kuliko speed ya Serikali inavyotuletea watumishi kwenye maeneo haya ya zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mchengerwa alione hili. Kuna vijiji vitano tunahitaji watumishi pamoja na vijiji vitatu, tuseme ni zahanati nane. At least kwa kila zahanati, basi tupate waganga au watumishi watatu ili tuweze kuzifungua ziweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika shule za msingi, pale Kata ya Tinde kuna Tinde A na Tinde B, na Kata ya Tinde ina watu wengi sana. Hizo shule mbili za msingi zina wanafunzi wasiopungua 1,800, wakati mwingine wanafika hadi 2,000. Changamoto kubwa ni wanafunzi wanaotoka maeneo ya huku kuvuka barabara ile. Nafikiri wengi mmepita pale kwenye junction ya Tinde, wanaotoka kuvuka barabara ya kutoka Mnadani halafu wanakuja kuvuka barabara inayotoka Dar es Salaam kwenda Shinyanga, wanafunzi wengi wamekoswakoswa na ajali. Hiyo namba moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili, wanafunzi wanabanana sana sasa hivi. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mchengerwa, hili ombi namba moja, anisaidie nipate fedha tupeleke kwenye Kata ya Tinde ili tujenge shule ya msingi mpya. Tumeshapata eneo pale Mnadani, yaani akileta fedha tunapeleka pale tunajenga, tunawapunguzia wanafunzi huku na tunapunguza hatari kubwa sana ya wanafunzi kuweza kupoteza maisha yao pale wanapovuka barabara ya lami kutoka Mnadani, na hii barabara inayotoka Dar es Salaam kuja mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna changamoto ya upungufu wa walimu. Katika shule ya msingi tuna upungufu wa majengo 77 na nyumba za walimu kama 26. Ukiniuliza kwa namna ambavyo naiona, nimwombe sana Mheshimiwa Mchengerwa, nikipata shilingi bilioni tano nakamilisha majengo katika sekondari, kwa maana nyumba za walimu, majengo shule ya msingi zote pamoja na maboma ya shule ambayo ni 77 na nyumba za walimu 26, tutakamilisha zahanati na majengo yote yaliyobakia 54. Nipe shilingi bilioni tano tu, nakuomba sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri katika kila bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja, mkiwa na bajeti maalum kabisa ya ukamilishaji wa majengo, shule ya msingi, sekondari na zahanati kwa nchi nzima mtakuwa mnatupunguzia kazi kubwa sana. Sisi tuko tayari, Mfuko wa Jimbo unafanya kazi, wananchi wanachangia vizuri, wala hawana tatizo. Tumefika vizuri tu majengo yote hayo yako lintel, yanastahili kabisa ukamilishaji ili yaweze kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tuna barabara, kutokana na athari za mvua hizi hazipitiki. Kwanza pole sana Mheshimiwa Mchengerwa, huko katika jimbo lako na nchi nzima, kuna maeneo mengi kutokana na hali ya mvua haikwepeki, Mungu katuletea mvua, ni neema, na kwa upande mmoja imeleta matatizo lakini kwa upande mwingine ni neema, lakini athari zake ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua halmashauri yetu imeleta maombi huko TARURA ili kuomba shilingi milioni 850 na tumeletewa shilingi milioni 100. Haitoshi sana, lakini utaona namna ambavyo utaweza kutusaidia sana ili tuweze kurekebisha barabara zetu ambazo zimepata athari za mvua hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kabisa tumeshaleta maombi yetu kwa ajili ya hii bajeti kuu. Tukipata hizo fedha, zinatosha kabisa kwenda kurekebisha barabara, hasa hasa barabara kuu. Barabara kubwa kabisa katika Jimbo la Solwa upande wa vijijini lile linalotoka Didia kuja Solwa. Hii barabara imeharibika sana, na ni barabara muhimu sana kwa sababu inaunganisha zaidi ya kata nane za wakulima tu. Yaani wanalima kilimo ambacho watu kutoka Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya wanakuja kwenye eneo hilo kununua mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jengo letu la halmashauri tulipata fedha mwaka 2022, lakini bahati mbaya mkurugenzi au uongozi wa wakati ule, siwezi kuulaumu sana, lakini fedha zetu zilichukuliwa na Serikali Kuu, zilirudi kwa makosa madogo madogo ya hapa na pale. Tulishaandika barua ya kuomba fedha hizo ili ziweze kurudi, ni shilingi 732,000,000. Tukapata fedha shilingi milioni 300, fedha hizo ilikuwa ni kwa ajili ya furniture, lakini kwa kuwa fedha zile shilingi milioni 732,000,000 zilirudi Hazina, tukaziombea hizi za furniture shilingi milioni 300 tuendelee na ujenzi ili tukamilishe jengo la Halmashauri ya Shinyanga DC. Serikali imetukubalia na sasa hivi nampongeza sana Mkurugenzi, anaendelea na anakamilisha jengo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Mchengerwa kama tutapata fedha ambazo zilirudi huko, shilingi 732,000,000 jengo hilo tunakwenda kulikamilisha pamoja na furniture na kila kitu ili sasa sisi Waheshimiwa Wabunge pamoja na Madiwani katika Halmashauri yetu ya Shinyanga DC tuweze kufanya kazi vizuri. Mimi yangu ni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa nyingine ni kwenye Sekondari ya Imisela. Mradi wa SGR ulipita kwenye kata moja inaitwa Kata ya Imesela, ukabomoa nyumba tatu za walimu katika sekondari na ukabomoa nyumba ya Mwalimu Shule ya Msingi Imesela. Wakafanya tathmini na katika tathmini ile walifanya tathmini ya nyumba tatu kwa shilingi milioni 78, kitu ambacho ni kidogo sana na hata hivyo bado fedha hazijaja. Wakasema watamlipa Mkurugenzi ili sisi tuendelee na ujenzi, kwa maana ya kujenga nyumba mpya za walimu katika Sekondari ya Imesela.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ahmed.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja, lakini naomba sana Mheshimiwa Mchengerwa tuzingatie tupate hizo fedha ili nyumba za walimu ziweze kujengwa. (Makofi)