Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba hii nzuri ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Napenda kutangulia kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Wabunge wengine wote kutoa shukrani na pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Mchengerwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Manaibu wake, Mheshimiwa Dkt. Dugange na Mheshimiwa Zainab Katimba pamoja na timu yote ambayo inafanya kazi TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana vilevile na Waheshimiwa Wabunge wote kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mwenyewe kwa mwelekeo wake katika kuhakikisha kwamba anapeleka fedha nyingi zaidi katika halmashauri. Kama alivyosema Mbunge mmoja hapa, ni kweli sisi tushindwe tu. Kila halmashauri, kila Jimbo, kila wilaya kuna miradi ya kutosha kuisemea, kujisemea, kujipigia kampeni na kumpigia Rais wetu kampeni kwa sababu kazi iliyofanyika ni kubwa sana katika maeneo yote; elimu, afya, TARURA na kadhalika, pamoja na changamoto nyingine zote ambazo zimetajwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuelezea kidogo kuhusu elimu kwa sababu kama tunavyofahamu wote hapa shule zetu za awali mpaka Form Six zinamilishwa na Serikali kupitia TAMISEMI na sisi Wizara ya Elimu vilevile tuna jukumu kubwa la elimu. Kwa hiyo, suala la uratibu kati yetu sisi hapa ni muhimu sana. Napenda kulieleza hili kwanza kwa sababu kuna Mbunge mmoja kaeleza vizuri sana hapa, kwamba tuimarishe ugatuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawahakikishia kwamba kuna uratibu mzuri sana unafanyika kati ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Elimu. Napenda sana kumshukuru ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa kwa kweli kwa kufanya kazi kwa karibu sana na sisi, na sisi kufanya kazi kwa karibu sana na yeye na wataalam wetu kuhakikisha kwamba tunasukuma maendeleo ya elimu na hasa mageuzi ya elimu ambayo tunajua yako njiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nielezee kidogo mambo mawili katika mageuzi ya elimu na jinsi ambavyo ukaribu wetu utatusaidia kusonga mbele. Kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge, Bunge lako Tukufu linafahamu kwamba Mheshimiwa Rais wetu alivyohutubia Bunge hapa tarehe 22 mwezi Aprili, 2021 aliahidi Watanzania kupitia Bunge hili kwamba Serikali yake itafanya mageuzi makubwa sana katika elimu. Kazi hiyo imeanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mawili makubwa kati ya mengine yote ambayo yanafanyika, ningependa niyataje. Moja, elimu ya sekondari kuanzia sasa hivi itakuwa na mikondo miwili; mkondo wa elimu jumla na mkondo wa elimu ya amali. Elimu ya amali ni kile ambacho tunakiita ufundi na ufundi stadi. Ufundi ni mambo ya uhandisi na kadhalika na ufundi stadi ni pamoja na kilimo, michezo, muziki na kadhalika. Kwa hiyo, element moja kubwa sana ya mageuzi ni hiyo mikondo miwili, nitaelezea baadaye kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kwamba, ikifika 2027 elimu ya lazima Tanzania itakuwa miaka kumi, kwamba mtoto lazima akae shuleni kuanzia Darasa la Kwanza mpaka afike Form Four kwa lazima. Sasa nitaeleza jinsi ambavyo tumeratibu pamoja na wenzetu wa TAMISEMI kuhakikisha kwamba haya tutayafanikisha na kama wanavyosema Waswahili, penye nia pana njia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuanze na elimu ya amali. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amesema, tayari tumeshafanya mpango, fedha zipo kwa ajili ya kujenga shule 100 za elimu ya amali. Hapa labda nifafanue, ni shule 100 za elimu ya amali nyanja ya uhandisi kama ilivyo Tanga Tech, Ifunda Tech, Bwiru Tech, Mtwara Tech na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana timu zetu zitaondoka kwenda kukagua shule za ufundi duniani huko kuhakikisha kwamba hata tunachokitoa sasa hivi Tanga Tech, Moshi Tech na kadhalika, tunakiboresha kuendana na hali halisi ilivyo sasa hivi. Katika hizo shule 100, Mheshimiwa Waziri ameahidi kwamba 26 zitakuwa tayari kuchukua wanafunzi ikifika 2025. Ujenzi wa shule 100 unaanza mara moja katika maeneo yote. Sehemu ambazo zimechaguliwa za awali ni katika zile wilaya au halmashauri ambazo zina jimbo zaidi ya moja halafu VETA imeenda kwenye jimbo moja, jimbo lingine halikupata VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mwelekeo wetu ni kwamba wale Waheshimiwa Wabunge ambao walikuwa na mvutano mkubwa, mmoja kapata VETA, mwingine hakupata VETA, Mheshimiwa Mchengerwa na timu ya TAMISEMI inawapelekea shule ya ufundi kwa maana ya elimu ya amali ya uhandisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, fedha zipo. Penye nia pana njia. Januari tunaanza kuchukua katika shule 26, huo ni upande wa elimu ya amali. Sasa upande huu mwingine wa kuchukua wanafunzi wote wasome mpaka form four, kazi hii imefanyika kwa muda mfupi na timu ya TAMISEMI na timu ya Wizara ya Elimu. Kitabu hiki kimeainisha shule zote hapa nchini. Kimeangalia ni shule zipi za msingi zina eneo la kutosha na watu wa kutosha kuongezea kujenga shule ya sekondari katika eneo lile lile; kimeangalia ni shule ngapi za sekondari ambazo zina eneo la kutosha na watu wa kutosha kujenga shule ya msingi kwa sababu itabidi tuwe na shule ambazo hapo hapo unapoanzia darasa la kwanza mpaka la sita wakati huo na form one mpaka form four.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu hiki kinaenda kufanyiwa uhakiki, naamini na Waheshimiwa Wabunge watapata fursa ya kuangalia na fedha tumekubaliana kwamba tutaharakisha matumizi ya fedha za mradi wa BOOST na mradi wa SEQUIP tuweze kumaliza kutumia zile fedha mapema kuliko ilivyopangwa ili ikifika 2027 tayari tuwe na miundombinu ya kutosha kwa ajili ya kuchukua wanafunzi wote kuanzia darasa la kwanza mpaka form four. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu hiki vilevile, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba kimeeleza na changamoto nyingine za walimu humu ndani ambazo Wabunge wengi sana wameeleza, uhaba wa walimu. Kimechanganua uhaba wa walimu vizuri na kuna mikakati pamoja na ajira ambazo sasa hivi zimeanza kuongezeka. Kwa mfano, kuna mkakati wa mwongozo wa kuwa na walimu wa kujitolea na taratibu za kupata walimu wa kujitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna utaratibu katika sera mpya sasa hivi kwamba kila atakayemaliza ualimu atakuwa na wajibu wa kwenda kufanya kazi ya ualimu mwaka mmoja kama ambavyo ukimaliza degree ya udaktari unaenda kufanya udaktari kwa mwaka mmoja, chini ya uchunguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, itapunguza uhaba wa walimu na pia itatusaidia kuhakikisha kwamba tunawafahamu wale walimu vizuri zaidi, tunaangalia maadili yao na uwezo wao wa kufundisha kabla ya kuja kuomba shughuli za kuweza kuajiriwa. Kwa hiyo, taarifa zote hizi humu zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema kazi ya mageuzi ni kubwa, ni mlima mrefu. Wakati taarifa ilipokamilika, Rais wetu alivyopelekewa mezani kwake, sisi wengine tukawa tunafikiria kwamba atasema subirini hapa kuna SGR, kuna bwawa la Mwalimu Nyerere, kuna miradi mingi, barabara za TARURA na kadhalika. Mheshimiwa Rais alisema; “Haya mageuzi yatagharimu fedha nyingi. Najua mtaanza kuja sasa kutaka fedha.” Akanyamaza kwa muda, tukajua limeondoka hilo, akasema; “lakini ni mageuzi mazuri, katekelezeni, tutapata fedha.” Tukajua waswahili wanavyosema, hiyo imeenda. Kwa hiyo, utekelezaji unaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, mwaka huu tayari tumeshaanza utekelezaji wa mafunzo ya amali, lakini kwa shule za Serikali zilikuwa ni shule 28 tu zime-qualify, shule binafsi tunazo 68. Kwa hiyo, jumla ni shule 96. Hatutaki kukimbiza kuliko kujenga uwezo wa kufundisha elimu ya amali kwa namna inavyotakiwa. Pia hatutaki kwenda taratibu sana halafu baadaye watu wakachoka, wakasema mnazungumza tu hatuoni matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Mheshimiwa Mchengerwa na Manaibu wake na timu yake yote, kwa sababu pasipo Ofisi ya Rais, TAMISEMI kulibeba hili na kulichangamkia, sisi tungebaki kuongea sera kila siku hapa. Tungeongea sera, ingefika siku moja watu wangesema tumechoka kusikia maneno, tunataka vitendo. Sasa hivi tunaona vitendo vimeanza na napenda kuwaahidi, kwa kushikamana sisi pamoja, chini ya uongozi wa Rais wetu, tutatoboa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri nakushukuru, isipokuwa nakuomba katika huo mpango mpya wa sera mpya ya walimu ambao mtawapa mwaka mmoja kuwachunguza, hawa ambao sasa hivi wapo kazini vilevile muwatazame na muwa-accommodate nao waajiriwe.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, labda nifafanue kidogo. Kwenye sera, utaratibu wa kuajiri walimu upo, bado hatujaanza kuutekeleza. Kwa hiyo, ajira zinazoendelea sasa hivi ni kwa utaratibu wa kawaida, hatimaye tutakuja kutoa mwongozo kwa kukubaliana na TAMISEMI na Utumishi taratibu za…
NAIBU SPIKA: Ahsante, nakushukuru.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.