Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimi nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja iliyopo mezani. Nimetumia muda mrefu kusoma Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025. Nilijipa muda pia wa kupitia bajeti yetu na sasa naomba nichangie.

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo naomba niliweke bayana hapa kupitia kwenye mpango huu, bahati nzuri Profesa Kitila ni Kaka yangu na ni rafiki yangu wa karibu, sasa katika mambo ambayo ninaweza kuyasema leo hii, nilichokiona kipya, maana yake awali niliwasifia lakini leo napata mashaka kidogo. Katika mpango huu nilichokiona kipya pekee ni kwamba kuanzisha kitu kinachoitwa KPI (Key Performance Indicators) hii ndiyo jambo jipya, kinyume cha hapo kwenye huu mpango ni kazi iliyofanywa ya kukusanya taarifa za Wizara zote na kuweka kwenye kitabu kimoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikapata mashaka kidogo leo kumetokea nini, kaka yangu Mkumbo na ameingia kwenye mtego wa namna hiyo, sasa naomba niseme machache kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo awali namshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama, akiwa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, niliwahi shauri Serikali namna gani tunaweza kuachana na mfumo wa OPRAS na tukaja na mifumo ambayo itaweza kupima watumishi wetu wa umma na taasisi zake za umma. Serikali ilisikia mchango wangu na ikabadilisha ikaachana na OPRAS ikaja na mfumo wa PEPMIS na PIPMIS. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, PEPMIS kwa maana ya Public Employees Performance Information System (Mfumo wa Upimaji Utendaji Kazi wa Utumishi wa Umma) na PIPMIS kwa maana ya Public Institutions Performance Information System (Mfumo wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma). Kilichosahaulika ni PEPMIS, namshukuru Mungu leo kuona kwenye mpango, Mheshimiwa Waziri wa Mipango kaleta KPI. Sasa jambo hili nimshauri pia Waziri mwenye dhamana ya Utumishi na Utawala Bora wa sasa, Mheshimiwa Jenista aliweza kukubaliana na hoja ya kuachana na OPRAS akaja kwenye mifumo hii ya upimaji utendaji kazi wa watumishi wa umma na taasisi. Sasa Mheshimiwa Simbachawene Kaka yangu ni muhimu sasa ukawa pamoja na Waziri wa Mipango kwenye mfumo huu wa KPI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, KPI ndiyo inayoweza kupima utendaji kazi tunafahamu, ngazi ya Wizara Mawaziri wanapimwa na vyombo lakini KPI ni mfumo mzuri na watanzania wangejua. Kwa hiyo KPI ikianza kwenye ngazi za Wizara, Mkoa mpaka Wilaya, Wakuu wa Wilaya pia wapewe KPI, Wakurugenzi wa Halmashauri wapewe KPI, hii itatusaidia kuamsha ari ya utendaji kazi wa watumishi wetu wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini nimesema eneo hili ninampongeza, kwa sababu mimi nafahamu eneo hili linakwenda kubadilisha fikra na tabia za mazoea kwa Wakuu wa taasisi za umma kufanya kazi kwa mazoea.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa pili ninasema tu, Kaka yangu Kitila umeingia kwenye mtego ambao sikutegemea uingie, umeweka KPI, nilikuwa naangalia sekta hii ambayo nina maslahi nayo mapana sekta ya ardhi. Nimesoma kwenye mpango wako kwenye sekta ya ardhi umeeleza pale nikawa najiuliza hii kama ni copy na ku-paste, kwa sababu sijaona unakwenda kumpimaje huyu Waziri wa Ardhi, mwisho wa siku kwenye utekelezaji wa majukumu yake?

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalani naomba ninukuu ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/2025, ilani inaelekeza kwenye Sekta ya Ardhi, kwamba inaelekeza Serikali kupanga matumizi bora ya ardhi katika Wilaya 54 zenye miradi ya kimkakati pamoja na vijiji 4,131. Baadaye inaendelea kusema kwamba, kusimamia na kuratibu uandaaji wa ukamilishaji wa mipango kabambe (Master Plan) ya Miji mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mpango huu unampimaje huyu, unampimaje? Kwa sababu naona kilichowekwa humu ni taarifa yake yeye kuja kwenye mpango! Sasa ninakuomba huu mtego Kaka yangu nakuamini sana uwezo wako, niombe hapa usiingie kwenye huu mtego wa kukusanya taarifa za Wizara mbalimbali na ku-compile kwenye kitabu kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mipango jukumu lake ni kuainisha malengo na kukabidhi Wizara za Kisekta, halafu unapima kupitia malengo uliyotoa kwenye Wizara za Kisekta, hiyo ndiyo unaweza kumpiama. Sasa nimeeleza hapa kwa habari ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, sasa je, vijiji elfu nne na kitu vyote vipimwe unampimaje na sasa tumebaki mwaka mmoja? Kwa hiyo, ninakushauri tu kwamba unakwenda eneo ambalo nadhani linaweza likashindwa kutusaidia Watanzania kwenye Wizara yako ya Mipango na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine niendelee kwenye eneo la bajeti yetu. Nchi yetu wote tunafahamu ni nchi maskini, sasa kupanga ni kuchagua, napata changamoto kweli, kama nchi hii inachangamoto ya miundombinu ya barabara kila kona, kila kona barabara ni shida, hivi ni kweli tunakwenda kupeleka shilingi trilioni sita kujenga viwanja vya ndege? Barabara ndiyo siasa, sasa niwaombe Wabunge wenzangu na niiombe Wizara ya Fedha katika hili. Nitoe mfano, leo hii unajenga kiwanja cha ndege Shinyanga, Mwanza to Shinyanga kilometa 150. Viability of the project, investment Vis-à-Vis viability tunataka ku-achieve nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo fedha inayopelekwa pale ingejenga barabara ngapi nchini, sasa nimezungumza hapa kupanga ni kuchagua. Kwa hiyo ndugu zangu Wabunge wote humu tunazungumza barabara, wanaozungumza viwanja vya ndege nadhani ni wachache sana, hivi hatuwezi kutafakari katiki hili? Kwa hiyo, nachelea kuunga mkono hoja hasa Wizara ya Fedha, kama mimi barabara yangu ya Morogoro - Njombe border, mikataba imesainiwa kilometa 100 mpaka leo Mkandarasi hajapewa fedha malipo ya awali tu shilingi bilioni tisa hajalipwa, leo nikubali kujenga viwanja vya ndege kwa wengine, nikubaliane na hoja ya Wizara ya Fedha, sitawatendea haki wananchi wangu wa Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hili siungi mkono hoja ya Wizara ya Fedha mpaka nione kwenye majumuisho Waziri wa Fedha ameainisha namna gani anakwenda kuachana na vitu, lazima tuchague barabara ndiyo msingi wa wananchi wote nchini. Kwa hiyo kwa habari ya viwanja vya ndege sisemi visijengwe, tusubiri kidogo tukamilishe barabara, kwa sababu nchi nzima kuna kero za barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine niende kwenye sekta ya mifugo, samahani naomba niseme...

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili, tunachangia kwa dakika nane leo. (Kicheko)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja Mpango lakini bajeti ya Wizara ya Fedha nadhani mpaka clarification ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ahsante. (Makofi)