Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi nichangie hoja ya Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango katika Bajeti Kuu ya Serikali. Nitangulie kusema kwamba ninaunga hoja mkono bajeti hii ipite, ila naomba nisiunge hoja mkono katika hoja ya kuweka kodi katika gesi asilia inayotumika katika magari. Ninaunga hoja mkono bajeti lakini katika hili siungi hoja mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ya matumizi ya gesi asilia katika magari bado ni changa na haiwezekani sekta changa uanze kuiwekea kodi. Maana yake ni kwamba itakuwa ni kama kujipiga risasi mguuni, na kwa jinsi hiyo kujipungunzia mwendo katika safari ya matumizi ya nishati safi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha utakapokuja kuhitimisha tafadhali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mapendekezo yangu binafsi kodi hiyo kwenye matumizi ya gesi asilia katika magari iondolewe. Kwa sababu magari ambayo sasa hivi yanatumika ni magari madogo madogo ya uber, hata haya light vehicles hayajaanza kutumia. Kwa hiyo, tunataka kuwa-tax wanaotumia uber? Hapana. Hiyo kodi ninasema iondolewe na wala siungi hoja mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze katika…
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunapambana kupata clean energy, na unapoongezea kodi kwenye gesi tayari una-encourage deforestation mahala ambapo tulikuwa tumekwishaanza kuhama. Naunga mkono hoja hii, ninamjulisha mwongeaji kwamba na mimi tutasimama pamoja na yeye ili kuzuia kabisa jambo hili lisitokee. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Profesa, taarifa hiyo?
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea. Ninaendelea kusisitiza kwamba hoja ya kuweka kodi katika gesi asilia ya magari no. It is a big no. Hiyo iondolewe. Nakushukuru sana, Mheshimiwa Askofu Gwajima, kwa support. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze katika Mpango, na Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo ambao sasa unatekelezwa, una vipaumbele ambavyo mojawapo ni kuendeleza rasilimali watu na Mheshimiwa Waziri amekiri kabisa kusema kwamba rasilimali watu ni nguzo katika kujenga uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunatambua kwamba rasilimali watu ni nguzo, ninaomba tunapokwenda kutekeleza bajeti hii twende tukaufanye utumishi wa umma uwe wa kuheshimika. Twende tukaufanye utumishi wa umma uweze kuwa na watu waliokuwa na hamasa ya kazi na motisha ya kufanya kazi. Katika hili tujenge utaratibu wa mwendelezo wa utekelezaji wa maono, njozi pamoja na mipango mikakati ya Wizara pamoja na taasisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta kwamba kiongozi fulani hivi anakaa katika nafasi yake ya maamuzi kwa muda wa mwaka, anaondolewa, miaka miwili anaondolewa. Sasa tunasukumaje maendeleo iwapo hakuna muendelezo na mara nyingi kunakuwa na kukatikakatika kwa kuendeleza mipango ya taasisi husika. Lakini pia wakati mwingine, mtumishi anapoonekana kwamba ana ujuzi na uwezo mzuri mara nyingi hapewi nafasi, ataondolewa na utamkuta mtumishi huyo anapelekwa mahali ambapo hata si eneo lake la umahiri, na hii imekuwa ikikatisha tamaa sana watumishi na kwa jinsi hiyo wanashindwa kuwa sehemu ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kukuza uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi hiyo naomba tunapoendelea kutekeleza bajeti hii hebu watumishi wa umma wapewe nafasi yao ya kufanya maendeleo yao ya nchi kwa kukaa katika nafasi hizo lakini pia kupewa heshima ya utumishi na wala sio kubezwa wakati mwingine kwa sababu wameonekana kwamba wana ushindani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine napenda kuchangia kuhusu mpango wetu unatamka habari ya kwamba kuangazia maendeleo ya viwanda kama sehemu ya kukuza uchumi. Pamoja na kwamba Serikali sio ambayo inayojenga viwanda, lakini ningetamani kuona kwamba mwaka wa fedha unapoanza, Serikali ifanye survey, tathmini ya kuona kwamba ni viwanda vingapi, katika maeneo gani tunavitarajia. Hii sentensi ya ujumla ujumla tu kwamba maendeleo ya viwanda na hatujafanya survey ni kwamba hatujajipa kipimo fulani ambacho mwaka unaokuja tutajipima kwamba tulipanga kuwa na viwanda kadhaa katika maeneo kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatuweki mkazo huo maana yake ni kwamba mwisho wa mwaka hatutaweza kujipima. Kwa hiyo, ningetamani sana Mheshimiwa Waziri wa Mipango inapokuja katika maendeleo ya viwanda awe ameshafanya survey maoteo ni yapi ili tunapofika mwisho wa mwaka tuseme tulitamani viwanda 50 katika maeneo kadhaa; je, tulifikisha lengo au hatukufikisha? Lakini tukienda kwa ujumla jumla hivi itafika mwisho wa mwaka hatuwezi kujifanyia tathmini ya kile ambacho tumekipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika mojawapo ya viwanda ambavyo mpango umevizungumzia na nanukuu maelezo ya Waziri Prof. Mkumbo kwamba, “tusipoteze nafasi ya kuwa na kiwanda cha kutengeneza betri za magari ya umeme kwa sababu malighafi ya madini ya Nickel graphate na rare earth itachimbwa hapa siku za karibuni”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba sana katika hili Serikali ifanye kila inaloweza kuvutia teknolojia hii mahali hapa. Yawezekana tukasema lakini tukashindwa kutekeleza, kwa sababu gani? Wachimba madini mara nyingi wana offtake agreements, anachimba kwa sababu anajua mnunuzi yupo wapi? Kwa hiyo, isije ikafika wakati anasema mimi ninachimba kwa sababu wanunuzi wangu wapo na hivyo anapeleka nje. Kwa hiyo, Serikali ifanye kila inaloweza, kuhakikisha kwamba inavutia kiwanda hiki hapa ili sisi Tanzania na nchi nyingine za Afrika zisiendelee kuwa mahali ambapo madini yanakuwa malighafi kwa ajili ya viwanda vya nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaposema kwamba Serikali ifanye kila inaloweza maana yake ni kwamba Waziri wa Mipango, Waziri wa Madini na Mheshimiwa Rais na watu wengine wote ambao ni wahusika wafanye kila wanaloweza ili kuweza kuvutia kiwanda hiki na hatimaye isije ikawa ni missed opportunity. Isije ikawa ni nafasi ambayo tena tutaona malighafi zetu za madini zinatumika kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi na kuwanufaisha watu wengine. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Profesa.
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, haa! Muda umeisha? (Makofi)