Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa nianze kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Tanzania. Sisi kama wanadamu neno kubwa la kumwambia ni ahsante na tunamshukuru kwa mambo mema anayotutendea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukuwe fursa hii kuipongeza Wizara ya Fedha, kumpongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake lakini pia na Waziri wa Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuipongeze bajeti yetu ni nzuri na bajeti imewalenga hasa watu wa chini. Katika bajeti yetu kitu ambacho nitaenda kukiongelea kikubwa ni suala la elimu kwa Watanzania, bajeti yetu ni nzuri, fedha zinakusanywa na tunaona namna miradi inavyotekelezwa, na makusanyo yanakwenda vizuri. Lakini tuiombe Serikali yetu, tatizo kubwa la Watanzania kutokuwa na elimu, wengi wao ninadhani kwamba hawatambui fedha ambazo Serikali inazozitumia kwenye miradi mbalimbali inapata wapi fedha hizo? Ninadhani kwamba, kama Serikali itawekeza zaidi kwenye suala zima la kutoa elimu kwa Watanzania kuonesha namna gani Serikali inaweza kupata fedha na kutekeleza miradi ya wananchi, imani yangu kubwa kwamba, wananchi na kwenye suala la utekelezaji wa makusanyo tutazidi kupanda zaidi ya hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Watanzania kwenye suala la ukusanyaji wa mapato bado elimu kwao ni ndogo. Rai yangu kwa Serikali, maoni yangu kwa Serikali, natamani sana kuona kwamba mkakati wa muda mfupi uliopo bado hatutoweza, kila siku tutakuwa na kazi ya kuelimisha Watanzania kwenye suala la ukusanyaji wa mapato lakini kama tukianza kujipanga na kujisahihisha, wapi kama Watanzania tunakosea, wapi kama sisi viongozi tunakosea, eneo kubwa ambalo tumeshindwa kuwekeza ni kwenye kuwekeza kwenye elimu kwa Watanzania, ili uweze kupata kile ambacho tunakitaka lazima tuwekeze kwenye elimu. Wananchi wa Tanzania uelewa wao kwenye suala la kodi umekuwa wa tofauti. Kama sisi Watanzania na viongozi tukiamua kusema tuanze kuwekeza chini, naamini kwamba kwa miaka ijayo, miaka kumi na tano, ishirini Tanzania itakuwa haina shida kwenye suala la makusanyo ya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye upande wa dini ya kikristo wanaanza kumwekeza mtoto kwenye Sunday school kuanza kumfundisha mapema kuelewa dini yake, lakini kwenye upande wa dini ya kiislamu mtoto anaanza kupelekwa chuo madrasa ili mtoto aanze kupandikiza zile mbegu mapema na mtoto anapokuwa anakuwa anajielewa kwamba yeye ni nani na yupo wapi, na hili suala la Tanzania kwenye ukusanyaji wa kodi lazima tukubali, ndani ya shule toka mtoto yupo mdogo aelimishwe nini maana ya kulipa kodi, na namna ya kumfundisha mtoto ni njia ndogo tu kwamba ukinunua, ukichukuwa ukipewa risiti inamaanisha kodi inakusanywa ndani ya Serikali, wewe utapata madaftari, wewe utapata sare za shule utaendelea kusoma bure wewe na wanaokuja pia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninadhani sasa ni muda wa Serikali kuwekeza kwenye elimu, tuwekeze kwenye elimu na uelewa uliokuwepo ndani ya Taifa letu ni mdogo. Hata leo ukisikia migogoro iliyokuweko ya wafanyabiashara tatizo elimu tu, uelewa umekuwa mdogo kwenye suala la ulipaji wa kodi. Tuangalie nchi za wenzetu, leo akija mgeni ndani ya nchi ya Tanzania, siku moja nilikutana na mzungu anakuja amemaliza kununua kitu amepewa risiti anaichunguza risiti. Anaulizwa unaichunguza nini anasema nataka nione kodi ya Serikali ipo wapi kwenye risiti? Tunatamani na sisi kama Tanzania wananchi wanaoishi ndani ya Tanzania tuwe na uelewa mmoja kwenye suala la ulipaji wa kodi. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri, tutatumia muda mkubwa ili Taifa litukumbuke, lazima tukumbuke kuanza na vizazi vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tukiwa kama viongozi tuanze na watoto wetu majumbani kuwaelimisha nini faida ya kulipa kodi. Pia tuwe na mikakati maalumu kuweka vitu kama hivi vidogo ndani ya shule zetu tukasema labda leo kuna kipindi mwisho tunaelimisha kuhusu suala la ulipaji wa kodi. Ni kitu kizuri, tutakuwa na kizazi ambacho kinaelewa nini maana ya kulipa kodi na kila anayekuwa anaelewa kwamba ili Taifa litumie, ili Serikali iwe na mikakati mizuri lazima liwe na fedha; na fedha hiyo sisi ndiyo tunaotakiwa tulipe kodi ili tuweze kuliendesha Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuishukuru bajeti imepiga hatua kubwa, ukiangalia kwenye suala la mikopo, mikopo yetu ni himilivu na tunavyokwenda kila siku bado mapato yetu yanaendelea kupanda. Niwape siri Watanzania, ni mtu mmoja ambaye ana uwezo wa kutunza bajeti vizuri, ni mama. Mama siku zote ana uwezo mkubwa wa kutunza bajeti na hili wanaume hawana ubishi nalo, wanajua, hata wao muda wanapoishiwa mifukoni mwao huwa wanasema vipi huko, hali ikojeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tauhida, ahsante, kengele ya pili.

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLONS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii. (Makofi)