Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyopo mezani. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai wa kuwa Bungeni wakati huu. Pia, nawashukuru sana Wapiga Kura wa Urambo na Wananchi wote wa Urambo kwa kweli, wananipa ushirikiano mkubwa. Nawashukuru sana na pia, ninaishukuru familia yangu kwa ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu ya kuishukuru Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kazi kubwa inayoifanya. Kama vile sisi Urambo tuna miradi mikubwa ya Maji ya Lake Victoria, umeme, barabara na mengi ambayo naishukuru sana Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mipango, wote wanafanya kazi kubwa wakisaidiana na Makatibu Wakuu. Kwa kweli, suala la kupata fedha siyo mchezo. Hongereni wote mlioko katika Wizara hizi mbili, za Mipango na Fedha, kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kutaka kuiinua nchi yetu kiuchumi. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kikao hiki au tuseme hoja hii iliyoko Mezani lengo lake kubwa ni kuona jinsi gani ambavyo nchi yetu inaendelea kiuchumi. Kwa msingi huo na mimi pia, ninaangalia, je, Wilaya yetu ya Urambo au Jimbo la Urambo linaendeleaje kiuchumi? Ni mambo gani ambayo yanaweza kutusaidia na sisi, kama Wilaya au Jimbo la Urambo, tukachangia katika uchumi wa nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ninaloona mimi ambalo ninaiomba Serikali itusaidie, ili na sisi tutoe mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, ni Mradi wa Maji ya Lake Victoria. Watu wa Urambo wakishapata maji watatulia na kufanya kazi nyingine ambazo zitawasaidia kuendelea kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni Mradi Mkubwa wa Kituo cha Kupozea Umeme cha Uhuru. Naishukuru sana Serikali imefanya kazi kubwa na imefikia hatua kubwa, lakini ombi letu sisi ni kwamba, kile kituo cha kupozea umeme kikamilike, ili watu waweze kufanya kazi zao; wanaouza juisi, wanaosaga unga na kadhalika. Umeme siyo kwa ajili ya kuona tu, lakini pia, ni kujiendeleza kiuchumi. Kwa hiyo, tutashukuru sana kama mradi wetu wa kituo cha kupozea umeme utakamilika haraka kwa kadiri itakavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi, kama Wananchi wa Urambo, zao letu kubwa tunalolitegemea ni tumbaku. Tunaishukuru Serikali kwa kutupa ruzuku hata kwenye mazao mengine, lakini ombi letu kubwa, hasa kwa upande wa zao la tumbaku, ni mbolea iwe imefika kabla ya Mwezi wa Nane. Kwa hiyo, ni matarajio yetu kwamba, kwa sasahivi mbolea iko njiani, karibu ifike kwenye maeneo ambayo tunahitaji mbolea kwa sababu, karibu tutaanza kuandaa mabedi ambayo ndiyo tunapanda mbegu za tumbaku. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali mbolea ifike kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, wakati huohuo tunaiomba Serikali katika kutoa mbolea ya ruzuku, basi itusogezee vituo, ili wananchi wasiende kuifuata mbali. Kwa sababu, kuna wakati mwingine wanakwenda kule wanakuta mbolea imekwisha inabidi walale, lakini wakiwasogezea karibu maana yake ni kwamba, wakulima watakwenda kununua mbolea na kurudi nyumbani kwao bila kupata usumbufu wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo katika kuuza tumbaku zipo kampuni ambazo zinalipa vizuri sana na tunazipongeza, zipo kampuni zinazonunua tumbaku zinalipa vizuri na kwa wakati. Nichukue nafasi hii kuiomba Serikali kutusaidia kwa kampuni zile ambazo karibu miaka mitatu sasa hawajawalipa wakulima tunaomba watusaidie jinsi ya kubana hizi kampuni ambazo hazijalipa wakulima ziwalipe wakulima ili nao wajiendeleze katika njia nyingine za kujiendeleza kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo niwaombe Serikali kwa niaba ya Wananchi wa Urambo kwamba zao letu lingine pamoja na tumbaku zao letu lingine ni asali kwa kufuga nyuki. Nimekuwa nikisimama hapa Bungeni kuiomba Wizara ya Maliasili na Utalii lakini sasa naiomba Serikali kwa ujumla iangalie jinsi ambavyo inaweza kutusaidia sisi hasa kwa upande wa wakulima wanaotegemea kufuga nyuki kwa kuweka mizinga yao ndani ya pori.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo niiombe bado Serikali iangalie uwezekano pamoja na kuishukuru Serikali kwa kutupa Hifadhi ya Mto Ugalla lakini bado tunaiomba, Wananchi wa Urambo tumegewe eneo hasa kata zile zinazohusika zipate eneo la kuweka mizinga yao kama walivyozoea. Habla haijawa Hifadhi ya Mto Ugalla wananchi walizoea kufuga nyuki, wanaweka mizinga yao, wanapakua asali wanauza lakini walipokuja kubadilisha sasa kufanya Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla imekuwa vigumu wananchi kupeleka mizinga yao na kuweka mule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado narudia kuiomba Serikali tunaombe tukatiwe eneo katika pori lile la Hifadhi ya Mto Ugalla ili na sisi tuweke mizinga yetu tuendelee kuuza asali kama njia mojawapo ya kuijiendeleza kiuchumi. Pia ninaiomba Serikali pia kwamba wanapoangalia upanuzi wa barabara watuangalie na sisi, barabara inayotoka Usongelani kwenda Tutuo kwenda Sikonge ili ijiunge na barabara kubwa zinazokwenda Mkoa wa Mbeya na Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo nichukue nafasi hii...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sitta ahsante kengele ya pili.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ahsante.