Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia bajeti ya Serikali. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai tupo hapa tunachangia bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nianze na shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwa watanzania hususan kwenye mambo mbalimbali ya elimu, afya, miundombinu pia mpaka juzi amedhihirisha upendo wake kwa watanzania kwa kuunda Tume ya Haki Jinai ambayo inamwezesha kila mtanzania kupata haki yake. Mheshimiwa Rais anahitaji pongezi kwa sababu ni kwa mara ya kwanza nchini kwetu Tanzania inaundwa Tume ya Haki Jinai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo ningependa kujielekeza kwenye suala la miundombinu nchini Tanzania. Sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi tunaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara kutoka Tabora kuja Mpanda kwa kiwango cha lami. Pamoja na hizo shukrani tunamshukuru pia kwa ujenzi wa Bandari ya Karema kule kwenye Ziwa Tanganyika ambayo itawezesha meli kutoka Congo kuja kutua kwenye Bandari ya Karema na pia itaweza kubeba mzigo kutoka Karema - Mpanda hadi kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo ninayo maombi kwa Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Maombi yetu ni suala la kufungua Mkoa wa Katavi, pamoja na hizo barabara ya Tabora - Mpanda, bado Mkoa wetu wa Katavi haujafunguka kwenda kwenye Mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tupewe barabara ya kutoka Kibaoni kuja Stalike ambayo ina kilometa 71, lakini kwa sasa hivi ujenzi wa barabara hiyo umesimama kwa sababu ya ukosefu wa pesa, hata Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alikwenda pale akawatoa wafanyakazi ambao ni wabovu lakini bado barabara hiyo imesimama. Ombi langu kwa Serikali itupe pesa barabara yenye kilometa 71 Kibaoni - Stalike iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la pili, tunaomba tupewe barabara kutoka Kibaoni – Usevya - Majimoto mpaka Inyonga, Inyonga pale wanakuja kuungana na barabara ya lami ambayo inatoka Tabora-Mpanda. Barabara hii ni muhimu kwa sababu inabeba mazao yanayotoka kwenye Bonde la Mwamapuri, bonde hilo lina kilometa takribani hekta 18,000 ambazo zinatoa mpunga unaolisha nchi jirani za Congo, Rwanda, Burundi lakini na nchini kwetu Tanzania. Hivyo basi, upo umuhimu wa kuijenga barabara hii ya kutoka Kibaoni – Usevya - Majimoto mpaka Inyonga kwa kiwango cha lami, barabara yenye urefu wa kilometa 165 ili tuweze kufanya biashara vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo ombi la barabara nyingine ya kutoka pale Mpanda Mjini kwenda mpaka maeneo ya Karema ambako tumejenga Bandari ambayo iligharimu takribani bilioni 47, fedha za kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara kutoka Bandarini kuja Mpanda Mjini haina lami, ni barabara ya vumbi. Hivyo basi, azma ya kujenga Bandari inaweza isifanikiwe vizuri kama hatutaweza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Ombi langu; ninaiomba Serikali ijenge barabara hii ambayo ina takribani kilometa 125.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine ni la ujenzi wa barabara ya kutoka pale Vikonge – Luhafwe mpaka Uvinza ili Mkoa wetu wa Katavi uweze kuungana na Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la tatu ni la barabara ya kutoka pale Mpanda Mjini kupitia Ugala ambako kuna daraja linajengwa. Hivyo tunaomba fedha za daraja hilo ili liweze kukamilika na barabara hiyo iweze kutoka Mpanda – Ugala – Kaliua – Kahama mpaka Nyakanazi ili tuweze kupata wafanyabiashara kutoka Rwanda na Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maombi ya barabara hizo sisi tunapenda kusema ahsante kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa fedha ambazo zimekuja kwenye Mkoa wetu huu wa Katavi kwa kipindi cha miaka mitatu. Ombi letu ni kukamilishiwa huu usafiri ili Mkoa wetu wa Katavi uweze kufunguka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine ambalo ningeweza kuliomba kwa Serikali ya Awamu ya Sita, tungeomba pia tukamilishiwe baadhi ya miradi. Kwa mfano tunao mradi wa kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika kuja pale Mpanda Mjini. Mradi huo wa kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika kuja Mpanda Mjini utaweza kunufaisha mikoa ya jirani kama Mkoa wa Rukwa pamoja na vitongoji ambavyo vinapita pembeni mwa mradi huo. Mradi huo ni mkubwa, bado haujaanza, lakini uko kwenye kufanyiwa tathmini. Tungeomba, ili kutatua tatizo la maji kwenye Mji wa Mpanda Mjini tunahitaji maji yavutwe kutoka Ziwa Tanganyika. Sasa hivi maji yaliyopo hayatoshelezi kwa sababu wananchi wameongezeka. Kama sensa ilivyopita mwaka jana, Mji wa Mpanda umekua na wananchi wameongezeka, hivyo mahitaji ya maji ni makubwa, yaliyopo hayatoshelezi na yanatoka kwa mgao kwa siku moja moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ombi lingine ambalo ningeiomba Serikali ya Awamu ya Sita tunaomba ule Mradi wa Umwagiliaji wa Mwamapuli ambao uko kwenye Halmashauri ya Mpimbwe utekelezwe. Mradi huu ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye aliwaahidi wananchi wa Mwamapuli…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbogo….
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono hoja.