Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza, nianze na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa. Ameruhusu fedha nyingi sana kwa ajili ya uwekezaji kwenye Mashirika na Taasisi mbalimbali za Serikali. Kwa hesabu za Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 75.79 kwenye Mashirika mbalimbali ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na katika uchambuzi wa Kamati yetu tumeangalia sana mashirika mbalimbali ambayo Serikali imewekeza mitaji, lakini tumeona baadhi ya mashirika utendaji wake wa kazi au uendeshaji wa mashirika hayo umekuwa ukisuasua sana. Jambo ambalo limeondoa kabisa tija ambayo tulikuwa tumeitarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kutoa mfano wa mashirika hayo machache, yapo mengi lakini machache, mojawapo ni: Shirika la TANOIL hii ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC); Shirika lingine ni TTCL; na lingine ni Bodi ya Mkonge. Haya ni mashirika ambayo uendeshaji wake umekuwa wa kusuasua sana. Kwa miaka mitatu mfululizo Mashirika haya yamekuwa yakitengeneza hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mashirika ya namna hii hayatufikishi kule ambako tulikuwa tunatarajia. Hayana uwezo wa kutoa mchango katika kuinua uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina iweke usimamizi wa karibu sana kwa mashirika kama haya ili lile lengo tulilokusudia, lengo ambalo Serikali na lengo ambalo Mheshimiwa Rais angetarajia la kuongeza uchumi wa Taifa letu liweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tumeliona ni hali ya tegemezi wa ruzuku ya Serikali, Mashirika mengi bado yanategemea ruzuku hayawezi kujiendesha yenyewe. Hii inatokana na ukweli kwamba hayaendeshwi vizuri. Kuna udhaifu kwenye management, kuna udhaifu kwenye Bodi za Mashirika haya. Kwa hiyo, mashirika haya yameendelea kutegemea Serikali bila ruzuku ya Serikali hayawezi kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika hayo ambayo nimeyataja ni kati ya hayo ambayo yanaendelea kutegemea ruzuku ya Serikali. Ukiangalia Ripoti ya Msajili wa Hazina ya mwaka 2022/2023 inasema kwamba utegemezi wa mashirika mbalimbali umeongezeka ambapo kwa miaka mitatu mfululizo umekuwa kwa 21.2% kutoka shilingi bilioni13.2 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 17.4 kwa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kuwekeza kwenye mashirika kama haya lilikuwa ni kwamba yaendeshwe vizuri ili ule utegemezi wa ruzuku uendelee kupungua kila mwaka. Sasa jambo hili limeshindikana baadhi ya mashirika yameshindwa kabisa kutekeleza utaratibu huu. Kwa hiyo, yameenda yanaendelea kupokea ruzuku na kusababisha mzigo kwa Serikali. Fedha ambazo zingeenda kufanya majukumu mengine zinaendelea kupelekwa kwenye mashirika kama haya ambayo kimsingi hayafanyi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza ningeshauri Serikali iangalie mashirika kama haya kama hayawezi kujirekebisha, kama hayawezi kufanya vizuri basi hakuna sababu ya kuendelea kuyapa ruzuku. Fedha hizi ambazo zinatolewa kwenye mashirika haya ziweze kufanya kazi nyingine za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba ya Serikali isimamie kwa karibu mashirika haya ikiwezekana baada ya muda mfupi yajikwamue yaweze kujiendesha yenyewe bila kutegemea ruzuku ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida nyingine ambayo tumeiona ni upungufu wa mitaji ya uendeshaji, yapo mashirika ambayo hayana fedha kabisa ya kujiendesha yanaendesha mashirika yao kwa madeni. Wanashindwa kabisa kulipa hata fedha za watoa huduma, fedha za wakandarasi wao ni kwa sababu hawana mitaji na ningeweza kushauri ikiwezekana watafute njia mbadala. Zipo Taasisi za kifedha ambazo zinatoa mikopo, lipo soko la hisa, wanaweza kutumia utaratibu wa PPP wakaweza kupata mitaji ili waweze kujiendesha wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika kama hayo ambayo nimesema hayana pesa kabisa yanaendeshwa kwa shida na kwa madeni ni pamoja na TTCL, MSD (Bohari ya Dawa), Benki ya maendeleo (TIB) na kuendelea. Mashirika haya hayana fedha yanaendeshwa kwa madeni, matokeo yake hatuwezi kupata ile tija ya uwekezaji ambayo ilikuwa imekusudiwa. Kwa hiyo, tunashauri wazingatie sana ikiwezekana watafute fedha katika vyanzo ambavyo nimevitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hali mbaya ya ukwasi kwa baadhi ya Taasisi hizi, hazina fedha kabisa. Taasisi kama hizi kama Serikali haiwezi kuwasaidia basi tujue kabisa haziwezi kuendelea. Ukiangalia hesabu zao wana mizigo ya madeni, wao wenyewe wapo hoi. Kwa hiyo, nadhani tusiendelee kuweka fedha nyingi kwenye mashirika kama haya ama tubadilishe management yake, tuweke watu wengine ambao wanaweza kuwa na uwezo wa kuendesha mashirika haya vizuri badala ya kuendelea kuwatumia wale wale ambao hawafanyi vizuri hilo ni jambo muhimu sana. Kupitia Ofisi ya TR, Serikali itafute management yenye uwezo, bodi zenye uwezo ili kusimamia mashirika haya ili yajiendeshe kwa faida na ile tija tunayo kusudia tuweze kuiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu mashirika mengi ambayo yanaonekana kama yana mitaji mikubwa sana kwenye hesabu zao. Ukienda kuangalia hesabu kama ya TTCL utakuta ina mtaji mkubwa lakini kinazalishwa kutokana na hiyo mitaji ni kidogo sana. Unakuta ama wana majengo ambayo hayapangishwi, wana ardhi ambayo haijaendelezwa, wengine wana mitambo ambayo imepitwa na wakati kwa sababu ya mabadiliko ya teknolojia lakini imeendelea kuonekana kwenye hesabu zao kwamba hawa watu wana mtaji mkubwa, lakini mitaji hiyo haizalishi kile ambacho kilitarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo wanaingia gharama ya uendeshaji, gharama ya kutunza hayo majengo, gharama ya kutunza viwanja kulipia kodi, gharama ya kutunza mitambo ambayo haiwezi kuzalisha tena. Kwa hiyo, ninashauri hatua zichukuliwe na mashirika haya ikiwezekana watunze au watumie mitaji ambayo inazalisha badala ya kuendelea kuingia hasara ya uendeshaji wa mitaji ambayo haifanyi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri sana jambo hili Serikali iliangalie kwa karibu kupitia Msajili wa Hazina, yale mashirika ambayo yana mitaji mikubwa haizalishi chochote ile mitaji ama iuzwe ili tusiendelee kuingia gharama ya kutunza majengo ambayo hayawezi kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)