Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hizi Kamati zetu zote tatu. Wakati Wenyeviti wa Kamati wanasoma taarifa zao hakuna Kamati hata moja haijazungumzia suala la madeni iwe kwenye taasisi, iwe kwenye halmashauri na Wabunge wanajua siku zote kwenye Bajeti za Wizara mbalimbali tumekuwa tukizungumzia suala la madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi huu ni mwaka wangu wa 14 nikiwa humu Bungeni, haya mambo yamezungumzwa sana bado hatujaona jitihada za dhati za kukomesha madeni. Nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa aliyesoma kwenye Kamati ya PAC amezungumzia suala la deni la TANESCO tumelisema sana hili na tukasema hili Shirika mwisho wa siku linakuja kuwa muflisi na hiyo ni TPDC bilioni 713 bado madeni mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaenda kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji tumezungumzia Serikali namna inavyodaiwa na mamlaka zake za maji na mimi nilichangia na tukasema hizi mamlaka zitashindwa kujiendesha. Leo kwenye taarifa hapa imesema, Mwenyekiti wa PIC amezungumzia hapa madeni mbalimbali na akatolea mfano, TTCL, POSTA, NFRA na maeneo mengine. Lazima tuwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha tunashughulikia changamoto mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa upande wa Kamati ya LAAC madeni kwenye halmashauri ni bilioni 887, madeni ya wazabuni ni bilioni 38.233. Wazabuni wa nchi hii wamekuwa wakitembea kulalamika wanatakiwa walipwe. Wazabuni wa nchi hii ni wananchi wetu wanaotupa huduma. Sasa mtu anakuja kukuhudumia ubwabwa, anakuja kukujengea barabara unakaa zaidi ya miaka mitatu humlipi huyu mtu amekopa benki, umeenda kuweka mafuta petrol station humlipi zaidi ya miaka mitatu. Hebu sisi tuvae viatu vyao, siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni nani hapa atafanya biashara mtu aje amkope akae zaidi ya miaka mitatu asilipe? Kuna akina mamantilie, watu wanakopa benki wafanye kazi na halmashauri zao, wafanye kazi na Serikali yao, wachangie uchumi wa nchi yao tuwalipe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye madeni ya watumishi yasiyo ya mshahara maana madeni ya malimbikizo ya mishahara kwenye halmashauri ni takribani bilioni 11, marupurupu mengine ya watumishi bilioni 44 kwenye halmashauri. Hawa watumishi ndio tunatarajia tukipeleka pesa kwenye halmashauri zetu za miradi ya maendeleo ndiyo wasimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watumishi hawawezi kugoma wanagomea mioyoni. Ogopa sana mtu anafanya kazi kwa stress anadai mshahara mdogo halipwi kwa wakati. Halafu unamshushia trilioni ya shilingi, kwa nini tusitengeneze mazingira ya watu kuchukua rushwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunazungumzia Serikali ilipe madeni, halmashauri hizi zisimamiwe zilipe madeni ya watumishi. Sisi Kamati yetu wakija pale tunajua wana uwezo wa kudai ji-commit hapa ndani ya miaka miwili lipa madeni and then halmashauri kusanya, endelea kufanya kazi za maendeleo. Hivi vitu si vizuri, havileti picha nzuri kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na suala la madeni tulishakubaliana kuhakikisha pesa zinazotengwa kwenye halmashauri za maendeleo ziende kwenye maendeleo. Kuna halmashauri ambazo zinapeleka 20% kutokana na uwezo wake, nyingine 60%, nyingine 40% na nyingine 70%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunazungumzia halmashauri 55 tulizokutana nazo kati ya 184 hazijapeleka fedha za maendeleo bilioni 38.836. Waheshimiwa Wabunge, tupo hapa kuhakikisha wananchi wetu wanapata maendeleo, tunapitisha bajeti hapa kuna matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo. Ndio maana mkienda Majimboni mnalalamikiwa hamtimizi ahadi. Watendaji wa Serikali hii wanakula pesa za miradi ya maendeleo. Wanatumia pesa zao za OC, wanatumia pesa za miradi ya maendeleo bilioni 38, tujiulize zingejenga shule ngapi? Tujiulize zingejenga hospitali ngapi? Hizi nazo wanatumia zao na bado pesa za miradi za maendeleo wanaenda kuzitumia kwa ajili ya kununua bagia, sambusa na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri tu za Jiji la Dar es Salaam; Jiji la Dar es Salaam kwa miaka mitatu haijapeleka fedha za maendeleo bilioni 21, Singida haijapeleka fedha za maendeleo bilioni mbili, Kigamboni bilioni mbili, Chato bilioni moja. Sasa hawa wananchi watapataje maendeleo na wakurugenzi wapo na wamekuja kwenye kikao wanakiri kwamba tulitumia kwenye matumizi mengine. Serikali inapeleka ruzuku na bado wanakusanya pesa zao za matumizi ya kawaida wanakula na wanakula fedha za wananchi, pesa zao za miradi ya maendeleo zinazotokana na kodi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mambo kama wawakilishi wa wananchi tupo hapa kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, haya mambo siyo ya kuyafumbia macho. Unakuta Mkurugenzi anafanya kosa hili anahamishwa anapelekwa kwenye halmashauri nyingine. Sasa unajiuliza analindwa na nani? Nani anakula naye? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye fedha za asilimia kumi. Mwaka jana tulizungumza, leo pesa ambazo hazijakusanywa (chechefu) shilingi bilioni 79 na CAG alikuwa anatuambia ameamua kwa Mkoa wa Dar es Salaam afanye ukaguzi maalum, wakati anaenda kuhakiki zaidi ya vikundi 49 vilikuwa vikundi hewa. Shilingi bilioni 79 za Watanzania, kuna baadhi wameunda vikundi hewa, hawa Maafisa Maendeleo wa Jamii hawa, hii kamati ya kutoa mikopo; na tunasikia sasa hivi Serikali inataka kufungua dirisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuweke kanuni na hawa wanaotoa ndiyo chanzo cha tatizo, wanaunda vikundi vyao na ninyi wenyewe Wabunge hamjui. Ukienda Kinondoni tu kuna shilingi bilioni sita zipo nje, Temeke shilingi bilioni tano, Ubungo shilingi bilioni 4.8, Kibaha shilingi bilioni moja, Kigoma shilingi bilioni moja na hizi ni chechefu. Kwa mfano, kwa Jiji la Ilala tu mbali ya hizi chechefu kuna shilingi bilioni 19 zipo nje. Kama hizi zimeshindwa kukusanywa, hizo zilizo ndani ya muda zitakusanywa? Je, huo mpango wa kuhakikisha mnataka kutoa mabilioni mengine ya shilingi bila kutibu tatizo hili na hawa watu wapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulienda kutembelea kikundi kimoja, wale vijana wakasema hata hapa tulipo ni kwa mama maendeleo. Alituambia tujikusanye, tumepata shilingi milioni 35; ndani ya miaka mitatu wamerudisha shilingi laki tano. Tukaambiwa pale wanatengeneza mradi wa kutengeneza chaki, hakuna hata maboksi 100, shilingi milioni 35 haionekani na huyo mtu bado yupo kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mambo hatuwezi kuyafumbia macho. Hata kama hela ya Serikali haiumi, jamani hii ni Tanzania yetu, hii ni Tanzania yetu. Hizi pesa tumepewa tuzilinde, tuzikusanye, ili tusonge mbele, sio kila siku tung’ang’anie kuzungumzia jambo moja. Hapa Mwenyekiti wakati anasoma, mtu kabisa hapeleki michango ya PSSF…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Hitimisha Mheshimiwa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu hapeleki michango ya PSSF halafu penalty inakuwa kubwa. Nilikuwa naangalia karibia shilingi bilioni tatu haijaenda kwenye Mifuko. Wastaafu wanatembea na bahasha, maskini wanachangisha wakope wakalipe zile hela za haki zao, ili waweze kupata mikopo. It is not fair, sio sawa. (Makofi)

MWENYEKITI: Kengele ya pili tayari Mheshimiwa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)