Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia na nitaanzia pale ambapo mjumbe mwenzangu alipoishia ili niendelee. Katika hizi hotuba ambazo zimesomwa hapa, suala la madeni na kikubwa mimi nitaenda kwenye madeni madogo madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi tujiulize kwa sababu, upo utaratibu mzuri ambao Serikali imeshauweka kwamba, Halmashauri yoyote ikikusanya mapato yake ina percent ya kutumia na ya kupeleka kwenye miradi ya maendeleo, 40% kwa 60%. Zipo Halmashauri nyingine zinapewa %30 kutokana na ukubwa wa mapato yake, nyingine zinapewa mpaka 80%, lakini bado Serikali kuu inaongeza ruzuku kwenye matumizi ya kawaida, shilingi milioni 79 kwa mwaka huu uliofanyiwa ukaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ukiangalia sisi Kamati yetu ya LAAC tukapita, Halmashauri 55 bado zinadaiwa na wale wazabuni wadogo wadogo, hawa wanao-supply stationaries, chakula na wanaowapa mafuta. Halmashauri zile zinadaiwa shilingi bilioni 29, sasa total ya madai yote inakuwa shilingi bilioni 87, lakini kwa zile 55 tulizoangalia ni shilingi bilioni 29. Sasa unajiuliza, hawa wana ile 60% ya kwao ya kuendeshea shughuli zao, ikiwa ni pamoja na kulipia chakula, kulipa mafuta na stationary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye miradi ya maendeleo inaeleza kabisa fedha ya ufuatiliaji isizidi asilimia tano ya ile fedha nzima ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa. Kwa hiyo, kule kwenye miradi ya maendeleo kumeshaji-set kwenyewe, kwamba, atakwenda kuangalia kituo cha afya, shule inavyojengwa kwa kutumia zile fedha, asitumie zile fedha zaidi ya asilimia tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta Halmashauri ile imetumia zile asilimia tano, imetumia ruzuku iliyoletewa na Serikali kati ya hii 79, imetumia ile 60% waliyokusanya wenyewe na bado imewakopa mama ntilie chakula, haijawalipa. Hizi hela za OC zinakwenda wapi? Yaani hiki ndiyo tunachoiomba Serikali irudi kule chini, itupe mchanganuo, hizi hela za OC huwa zinakwenda wapi kwenye halmashauri zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Halmashauri moja katika Mkoa wa Iringa, siyo Manispaa ya Iringa, mama ntilie anadai zaidi ya shilingi milioni 150 amelisha chakula kwa mwaka huu wa fedha, nafikiri anaitwa Turumba Food and Catering. Shilingi milioni 150 wamekula chakula kwenye vikao vyao, mama yule anadai shilingi milioni 150, sasa wamemwacha wamehamia tena kumfilisi mwingine na hii ndiyo trend kwenye Halmashauri nyingi. Tunawauliza hao wanaowadai bado wanawahudumia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hapana. Sasa ina maana sisi tunapeleka hizi fedha au Serikali inapeleka hizi fedha ikachechemue ule uchumi wa watu wetu wa chini, kumbe zinaishia hapa juu kwenye Halmashauri, watu wetu hawapati na ndiyo maana malalamiko ya hali ngumu. Watu mifukoni hatuna kitu, yanakuwa makubwa. Kwa hiyo sasa tunaomba hii ikaangaliwe, OC zinatumika vipi, ile inayopeleka Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna issue ya ceiling. Kuna Halmashauri nyingine ukiangalia CAG anasema zinatakiwa zikusanye shilingi bilioni 911, zimekusanya shilingi bilioni 912, lakini Kigamboni wamekuja tumewahoji kwenye Kamati yetu, Kigamboni wamewekewa ceiling ya shilingi bilioni 11, lakini wao wamekusanya shilingi bilioni 13, wana-exceed shilingi bilioni mbili. Kwa hiyo, Halmashauri nyingine zina uwezo wa kujitanua, zikatanua yale mapato yake, lakini zinabanwa na ceiling ambayo Serikali sijui, Wizara ya Fedha sijui, ni Sheria za Umoja wa Mataifa au whatever, IMF wanatubana kwa hiyo, wale wanashidwa kuongeza effort kwenye kukusanya mapato. If that is the case, basi tuangalie namna, tutatumia akili gani, ili kuona zile halmashauri zikusanye mapato zinavyoweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya NHIF. Kwanza NHIF yenyewe inajiendesha kwa hasara sasa hivi. Nilipata mtu mmoja aka-calculate akasema, tukitaka NHIF ijiendeshe labda kila anayechangia sasa aongeze asilimia 2.2 ya mchango wake ndiyo itafika kwenye balance ya kwamba, inazalisha faida kwa hiyo, maana yake ni ipo chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini NHIF inadai kila Halmashauri wanawakata hela; mmeshindwa kujaza fomu, mmekosea kujaza fomu, nimesikia hapa nimeambiwa na Benjamin kumbe wanakosea kujaza fomu mpaka wanadaiwa penalty ya shilingi bilioni tatu. Sasa mimi najiuliza na ukiangalia makosa yenyewe, kosa lenyewe tumeliona juzi pale; NHIF wanasema dawa au huduma iliyotolewa kwenye kituo cha afya haikutakiwa kutolewa kwenye kituo cha afya, kwa hiyo, hiyo huduma tunawakata hela. Vifaa tiba kwenye nchi hii vinapelekwa na Serikali. Mnapelekaje dawa mnayojua haitakiwi kutumika kwenye vituo vya afya ili NHIF wazikate halmashauri? Kwa hiyo, wanadumaza huduma za afya kule chini. Sasa hivi tunajua vituo vya afya vimejengwa, vya kisasa, lakini wenzetu wa NHIF waende kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kutibiwa siku moja, daktari kani-diagnose akaniambia nataka nikutibu, nikufanyie operation hii. Wao wakasema haiwezekani, sisi kwenye mikataba yetu hatuna operation ya hivyo, labda ufanye operation ya analogy. Sasa, yaani kule kuna madaktari, sisi tukiwa diagnosed na madaktari wetu, madaktari bingwa wenye huduma za kisasa wao hawataki wanataka kuturudisha kwenye huduma according to wao wanavyotaka na ndivyo wanavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi NHIF hawajui kwamba, leo hii katika vituo vya afya tunafanya operation za akinamama wajawazito? Halafu unamshtaki nesi kwa kutoa matibabu ambayo hayakutakiwa kutibiwa kwenye kituo cha afya, ilitakiwa kuwa hospitali ya wilaya, hawajui leo tuna Madaktari Bingwa kwenye hospitali za wilaya? Kwa hiyo, halmashauri nyingi zimepigwa penalty ya kukataliwa zile fedha, sio kweli. Tunataka Wizara ya Afya wakakae na NHIF warudishe fedha za watu, waache uporaji. Halafu hii Serikali ni yetu, watu tunataka tuwahudumie wananchi wetu, sio suala la penalty. Wenyewe zikirudi huko juu wanafanya nini? Ziende zikatibu wananchi kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuja kwenye suala lingine. Pamoja na mambo haya niliyoyaongea, CAG safari hii amefanya kazi kubwa sana. Amefanya ukaguzi wa ufanisi kwenye masuala ya afya ya akili kwenye nchi hii. Sasa wote mtakuwa mmesoma fedha, mmesoma kampuni, mmesoma nini, hamjasoma afya ya akili. Tatizo kubwa ni afya ya akili. CAG amesema kabisa, mtu yeyote mwenye afya nzuri ya akili anaweza ku-contribute vizuri kwenye nchi yake, kutoa mchango sahihi kwenye jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna watendaji ambao hawatoi michango sahihi kwa sababu, huduma za afya ya akili hazijawekewa msingi kwenye nchi hii. Leo hii tumekwenda kukagua shule moja Chaduru huko, watu wamejenga msingi, kozi ya msingi wa jengo inakwenda kozi 18. Fedha yote imeishia kwenye msingi, huyo mtu ana afya nzuri ya akili? Anatoa mchango gani kwenye hii nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua kabisa thamani yangu. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, mwanamke, unalazimisha nikatibiwe kwenye analogy, ili nife? Halafu utanipata wapi mtu kama mimi kwenye nchi hii? Sasa hawa wenzetu nao wana afya nzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani afya ya akili hata humu ndani tukisema watu wanafikiria ni mambo ya uchizi. Sio mtu amekuwa kichaa, lile ni tatizo tayari. Afya ya akili ni ustawi tu wa akili zetu na CAG kasema kumbe kuna Sheria ya Afya ya Akili ya Mwaka 2008, Kipengele cha 31(1)(b), kinataka Wizara iunde Baraza la Afya ya Akili Nchini, ili kutoa huduma za kisaikolojia na huduma saidizi. CAG kasema kama hatutoliangalia hili watu watazidi kupata matatizo mengi, watashidwa ku-perform katika ile standard tunayotaka wa-perform, vijana wetu watazidi kulewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unashangaa humu ndani leo hii watu wamekwenda kutoa huduma za afya ya akili wamewaangalia wazee, wamewaangalia watoto wale waliopata mimba za utotoni, watoto wa mazingira magumu na wamewaangalia watu wenye ulemavu. Tuulizane humu ndani, kati ya wazee wetu wa zamani waliokuwa wanachukuwa majembe wanakwenda kuchimba barabara, wanajitolea na sisi leo tunajengewa barabara za lami, tunamwaga takataka, tunataka Serikali ituzindulie, nani ana afya mbaya ya akili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini ukawaangalie wazee badala ya uanze kutuangalia sisi kwanza afya zetu zikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala ni sheria. Tunataka Baraza la Afya ya Akili Nchini hii liundwe. Sheria inaelekeza tangu Mwaka 2008, ili vijana wetu wapate support ya ushauri. Tunasema si kwamba, mambo hayaendi kule chini, mambo yanakwenda, mikopo inakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, wenzangu wameongelea hiyo 4:4:2 inakwenda kwenye vikundi, lakini vikundi vile vikipewa mikopo tumeshaambiwa mikopo ile hairudi. CAG anasema, ili mtu aweze kurudisha mkopo lazima akili yake iweze ku-perform, yaani a-produce productively siyo tu suala la kwenda kazini, anakwenda kazini anazalisha kwa tija?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakwenda Milembe, dawa ya afya ya akili iliyopo Milembe ni moja tu, ya aina moja, wakati ubongo una sehemu tatu na sehemu zote zikiathirika zinahitaji matibabu tofauti. Tunaomba suala hili lichukuliwe kwa uzito, tutapunguza matatizo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawacheka wenzetu si ndiyo? Tunaona wenzetu sijui vijana wao wamefanyaje, wameingia humu wanaleta vituko, wanaleta maandamano na sisi tusipohangaika na kuwaweka vizuri vijana kwenye akili tuna changamoto kubwa; CAG amesema suala hili limesababisha tukakosa ushauri wa kisaikolojia na vijana wengi wameingia kwenye ulevi uliokithiri, ni nani hapa sio shahidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unachukua kabisa kijana, umepanda bodaboda unaona kabisa huyu tukifika ni kudra za Mwenyezi Mungu. Watoto wadogo, leo tuna viongozi ambao sasa hivi ukienda kwenye mitaa ya mijini kote kuna casino zimewekwa kila mahali. Wanaotoa vibali ni wasomi wa nchi hii ambao wanajifanya wana afya ya nzuri ya akili, kutuletea casino kwenye makazi ya watu, watoto wanashinda wanakimbia humo, wanakunywa, wanavuta bangi, hawana akili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema suala la afya ya akili tuanze kufundishwa sisi tulioko juu. Huku ghorofani kukishakuwa kumechanganyikiwa hata tufanyaje, ndiyo maana leo watu wanatafuta, kila zikipelekwa fedha za madarasa hazitoshi, tumeongeza wanasema hazitoshi. Kituo cha afya mara ya kwanza tumepeleka shilingi milioni 470 hazitoshi, tumepeleka shilingi milioni 580 hazitoshi, tunataka shilingi milioni 640. Tunapeleka shilingi milioni 640 hazitoshi. Mtu anajenga nyumba, anajenga shule mahali penye mwinuko, anatafuta level ya mlima kuanzia kule chini mpaka apate level ya pale juu, halafu ndiyo ajenge darasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani kama huyu mtu ana akili timamu kwa nini asijenge kwa leveling? Waheshimiwa, si tulikuwa Rwanda hapa? Si tuliona zile nyumba zao zilivyo juu ya milima, hivyo? Sasa wangekuwa wanatafuta level wale, mpaka wakakutane kule juu, hela yote shilingi milioni 600 si inaishia huko? Huku juu Wizara, wenzetu TAMISEMI, kule kwenye wasomi tunawashukuru, hivi hawajui nchi hii kama kuna Southern Highlands of Tanzania? Tuna ukanda wa ziwa, tuna ukanda wa kati, hawajui? Wametoa ramani zote za flat rate, afya zao zikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Afya jambo hili siyo la kulifanyia mzaha. Kampeni zenyewe, Marekani wameanza kampeni za afya ya akili tangu Mwaka 1958 na unakuta wale ma-first ladies kama akina nani, ndiyo wanakuwa ma-organizer wa zile kampeni. Sisi hatufanyi kampeni, tunasubiri siku ya kujinyonga duniani ndiyo tunafanya kampeni ya afya ya akili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka hizi kampeni ziwe intensive, watu wajue. Humu ndani mimi nakutana na watu, siwezi kuwataja ninyi jamaa zangu, Waheshimiwa wenzangu, muda wenyewe tuliopo sio mzuri tutalipuana vichwa, lakini wengi wao humu na ninyi pia, hamuelewi. Mkiniona mimi mnaniambia balozi wa afya ya akili, mnafikiri balozi wa machizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio maana yake. Nawaambia kila siku suala la afya ya akili ni ustawi wa akili ya mtu kichwani.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuja ukichaa, tayari ni tatizo. Niombe sana, CAG ametusaidia, ametoa mapendekezo ya namna ambavyo tunaweza tukashughulika na suala la afya ya akili, kutojibu hoja za CAG ni kukosa afya ya akili. Wajibu hoja za CAG, anawasaidia wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)